Somo la 7: Safari ya Kwanza ya Paulo ya Kimisionari

(Matendo 13)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, wakati mwingine ni vigumu kuwa kiongozi wa kanisa? Je, upinzani na kupachikwa majina ni jambo linalokatisha tamaa? Somo letu juma hili linahusu safari ya kwanza ya Paulo ya Kimisionari. Tutajifunza kuhusu milima na mabonde ya kazi yake. Hata hivyo, hitimisho lenye kutia moyo katika Matendo 13 ni hitimisho lake: “Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.” Hebu tuzame kwenye somo letu ili tujifunze jinsi tunavyoweza kujawa furaha na Roho Mtakatifu!

 

  1.    Antiokia

 

    1.    Soma Matendo 13:1. Je, unashangaa kwamba Sauli (ambaye baadaye aliitwa Paulo) anatajwa miongoni mwa manabii na walimu wanaoongoza katika Antiokia? (Amekubalika na kanisa la awali licha ya yeye kulitesa hapo kabla.)

 

    1.    Soma Matendo 13:2. Utakumbuka katika masomo yetu ya nyuma kwenye kitabu cha Matendo tuliona kwamba viongozi wanachaguliwa kwa njia mbalimbali. Barnaba na Sauli wanachaguliwaje kwa ajili ya jukumu hili? (Roho Mtakatifu anafanya uchaguzi wake yeye mwenyewe.)

 

      1.    Unadhani hilo lilitendekaje? (Tunaambiwa kwamba Roho Mtakatifu “alisema” na kisha tafsiri ya Kiingereza inayaweka maneno hayo kwenye alama za kudondoa. Lazima watafsiri waamini kwamba Roho Mtakatifu alizungumza nao kwa sauti.)

 

      1.    Roho Mtakatifu alizungumza na kundi gani? (Biblia haisemi, lakini kuna uwezekano wa aina mbili. Uwezekano wa kwanza ni kwamba “wao” inalirejea kanisa. Inawezekana kundi la pili ni manabii na walimu wanne waliobainishwa hapo awali. Walikuwa wakiabudu, na Roho Mtakatifu akanena nao.)

 

    1.    Soma Matendo 13:3. Kundi liliwapeleka wapi Barnaba na Sauli? (Biblia haibainishi hadi hapo baadaye. Kusema kweli, sidhani kama Barnaba na Paulo au kanisa walifahamu hadi kufikia hapa.)

 

      1.    Leo, safari tunayotaka kuitafiti inajulikana kama safari ya kwanza ya Paulo ya kimisionari. Hii inatufundisha nini kuhusu kuyatenda mapenzi ya Mungu katika zama zetu? (Mungu atatuongoza ikiwa tuko radhi. Tunaona kwamba Sauli (Paulo) hakupanga hii safari ya kwanza ya kimisionari, badala yake Roho Mtakatifu aliianzisha safari na kuwachagua nani wa kwenda.)

 

  1.   Kipro

 

    1.    Soma Matendo 13:4. Safari ya kuelekea Kipro ilichaguliwaje? (Biblia inatuambia kuwa “walipelekwa na Roho Mtakatifu.” Roho Mtakatifu anachagua mahali pa kwenda!)

 

      1.    Je, Roho Mtakatifu yu hai kanisani kwako? Ikiwa sivyo, mambo yako sahihi yanatendekaje?

 

    1.    Soma Matendo 13:5. Kwa nini wanaanza kupeleka injili katika masinagogi ya Wayahudi? (Hili ni jambo tulilolijadili kwenye masomo ya awali kwenye mfululizo wa masomo haya. Ukristo ni utimilisho wa unabii wa Kimasihi na huduma ya patakatifu ya Agano la Kale. Ni utimilifu wenye mantiki wa Kiyahudi. Kwa upande wa uelewa, Wayahudi wepesi wa kutambua wako mbele ya Mataifa. Ni sawa na kuanza kufundisha wanafunzi wa madarasa ya juu ambao uelewa wao ni mkubwa.)

 

    1.    Soma Matendo 13:6-7. Neno “mchawi” linamaanisha mtu atendaye maajabu (mchawi). Nadhani linatafsiriwa mchawi kwa sababu ya kile anachokizungumzia Paulo baadaye kumhusu. Tunafahamu nini, kwa kiwango kidogo, kuhusu huyu mchawi? (Yeye ni nabii wa uongo. Anafanya biashara kwa udanganyifu.)

 

      1.    Huyu mchawi anashikilia wadhifa gani mkubwa? (Yeye ni mshauri wa afisa wa Kirumi anayeshughulikia na kuangalia masuala ya kisiwa.)

 

      1.    Tunajifunza nini kuhusu Sergio Paulo, afisa wa Kirumi? (Ana akili, mwerevu, na mwenye tamaa ya kuisikiliza injili.)

 

        1.    Anaweza kuwa mwerevu kwa kiasi gani ikizingatiwa kwamba anashauriwa na mtu mdanganyifu?

 

          1.   Je, kuna lolote la sisi kujifunza katika jambo hili?

 

    1.    Soma Matendo 13:8. Hii inatuambia nini kuhusu asili ya uchawi wa Bar-Yesu? (Anafungamana na Shetani.)

 

    1.    Soma Matendo 13:9-10. Vipi kuhusu kutumia njia ya upole kwa wadhambi? Je, Yesu hakuwa mfano wa hilo? (Tunatakiwa kutofautisha kati ya wadhambi wa kawaida na wale walio maadui wa injili. Tunaweza kupambana moja kwa moja na maadui.)

 

      1.    Tunaona hadhari gani kuhusu kuwaita maadui wa Mungu? (Kifungu kinasema kuwa Paulo “alijawa Roho Mtakatifu.” Tunatakiwa kuwa na uhakika kwamba Roho Mtakatifu ndiye anayeelekeza kwa kutumia lugha kali kama hii.)

 

    1.    Soma Matendo 13:11. Unadhani Paulo anawazia nini anapotangaza hii hukumu kwa Bar-Yesu? (Hiki ndicho haswaa kilichomtokea Paulo!)

 

      1.    Unadhani kwamba Mungu anayawazia matokeo yale yale kwa Bar-Yesu? (Utaona kwamba yeye ni kipofu kwa muda mfupi tu. Inaonekana kufanana sana na kile kilichomtokea Paulo. Kamwe hatusikii habari za Bar-Yesu tena, hivyo hatujui lolote.)

 

    1.    Soma Matendo 13:12. Kifungu hiki kinasema kwa nini Sergio Paulo aliamini? (Imani yake haifungamani na kumpofusha Bar-Yesu. Badala yake, kifungu kinasema kuwa “aliyastaajabia mafundisho ya Bwana.” Ilikuwa ni mafundisho, na si muujiza.)

 

  1. Antiokia, Mji wa Pisidia

 

    1.    Soma Matendo 13:13-15. Angalia jinsi walivyolishikilia “kanisa.” Kwanza, wana desturi ya kusoma torati, kisha wanawapa wageni nafasi. Je, unaweza kufanya hivyo kanisani kwako? (Siwezi kufanya hivyo. Nakumbuka mara nyingi sana mgeni kuja kwenye darasa langu la Shule ya Sabato na kutoa maoni yasiyo sahihi. Kama maoni yana matatizo, itakuwa vibaya sana kumpa mgeni nafasi ya wazi. Huenda ndio maana viongozi waliomba tu kupewa “neno la kuwafaa watu.”)

 

      1.    Unadhani kwa nini jambo hili lilitokea hapa? (Ushawishi wa Roho Mtakatifu.)

 

    1.    Soma Matendo 13:16. Nani yupo kwenye umati huu? (Wayahudi na Mataifa walioabudu katika sinagogi.)

 

    1.    Tutaruka mjadala wa Matendo 13:17-38 kwa sababu unahusu masomo mengine ya injili ya Paulo yanayonukuu historia ya Uyahudi na vifungu vya Biblia vinavyounga hoja yake kwamba Yesu ni Masihi. Hata hivyo, ni vyema ukasoma hubiri la Paulo.

 

    1.    Soma Matendo 13:38-39. Hii inahitaji badiliko gani la imani? (Lazima wampokee Yesu ili dhambi zao ziweze kusamehewa. Wanachokiamini sasa hakitawahesabia haki.)

 

    1.    Soma Matendo 13:40-41. Je, manabii walitabiri kuwa Yesu atatenda jambo lisiloaminika? (Soma Habakuki 1:5-6. Hiki ndicho kifungu anachokinukuu Paulo. Cha kushangaza, kinazungumzia uvamizi wa Babeli na si ujio wa Yesu.)

 

      1.    Hebu tujadili jambo hili. Je, ni sahihi kuchukua kauli ya Biblia ambayo iko nje kabisa ya muktadha na kuitumia kwenye hoja yako?

 

      1.    Nani aliyeangamiza hekalu la kwanza? (Watu wa Babeli.)

 

        1.    Kwa nini Mungu aliruhusu hekalu lake la kwanza liangamizwe? (Ukisoma kitabu cha Habakuki sura ya kwanza, utaona kwamba Habakuki anamwita Mungu ili awaokoe watu wake kutoka kwenye vitendo visivyo vya haki na matendo mabaya. Mungu anajibu kwa kuwatuma watu wa Babeli wakaitekeleze hukumu. Angalia Habakuki 1:12.)

 

        1.    Nini kitalitokea hekalu la pili? (Litaangamizwa na Warumi muda mfupi ujao. Mungu anatoa hukumu kwa mji uliomuadhibu kifo. Paulo hakichukulii kifungu hiki nje ya muktadha, ni onyo dhidi ya kumkataa Mungu.)

 

    1.    Soma Matendo 13:42-43. Tukichukulia kile ambacho Paulo amewaambia hivi punde, je, hili si jibu zuri?

 

    1.    Soma Matendo 13:44-45. Jibu chanya linabadilika. Nini kilifanya libadilike? (Wivu.)

 

      1.    Kwa nini viongozi wa Kiyahudi wanakuwa na wivu? (Paulo na Barnaba wanawavuta watu wengi.)

 

      1.    Je, unawaonea wivu viongozi wa Kikristo wanaowavuta watu wengi?

 

    1.    Soma Matendo 13:46-48. Nini kiliwafanya Mataifa wawe wasikivu wa injili zaidi?

 

    1.    Soma Matendo 13:49-52. Kwa nini wanafunzi wanajaa furaha? (Hili ni somo tunaloweza kujifunza. Walikuwa na furaha kwa sababu walikuwa wanayatenda mapenzi ya Mungu. Haikujalisha kwamba baadhi ya viongozi waliwatolea lugha chafu na kuwafukuza. Walikuwa wanampendeza Mungu.)

 

    1.    Rafiki, je, umetiwa moyo na somo hili? Kama ilivyo kwa Paulo na Barnaba, unaweza kukabiliana na upinzani. Unaweza kuwa na wapinzani. Lakini, ukiufuata mwongozo wa Roho Mtakatifu utajawa na furaha! Kwa nini usifanye uamuzi sasa hivi kutafuta kuyatenda mapenzi ya Mungu?

 

  1.   Juma lijalo: Baraza la Yerusalemu.