Somo la 9: Safari ya Pili ya Kimisionari

Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
9

(Matendo 15:30-16:40)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Juma lililopita tulijadili mgongano juu ya tohara. Kanisa lilitatua mgongano huo, likaweka uamuzi kwenye maandishi, na Paulo na Barnaba wakafikisha uamuzi huo kwa waumini waliopo Antiokia. Takribani mara tu baada ya mgongano kutatuliwa, mgongano mwingine uliibuka kati ya Paulo na Barnabas. Huu si ubishani wa kiteolojia, bali ni mgongano wa watu binafsi. Nini kinatokea panapokuwepo na mgongano miongoni mwa uongozi wa kanisa? Je, huu ni upungufu wa imani? Je, hii inamaanisha kuwa mtu hana vigezo vya kuwa kiongozi? Au, mgongano utarajiwe? Je, hili linaweza kuwa jambo zuri kwa kanisa? Juma hili somo letu la Biblia linajumuisha mgongano mkubwa miongoni mwa viongozi wa kanisa. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

  1.    Kurejea Kutoka Kwenye Mgongano
    1.    Soma Matendo 15:30-31. Kanisa lililopo Antiokia linauchukuliaje uamuzi wa mabishano juu ya tohara? (Washiriki wanatiwa moyo. Bila shaka, wengi wao walikuwa watu wa Mataifa.)
      1.    Katika hali ya kawaida unauchukuliaje uamuzi unaofikiwa baada ya ubishani? (Ni kawaida kutaka ubishani uishe na kutiwa moyo pale unapoisha.)
    1.    Soma Matendo 15:22 na Matendo 15:32-33. Haya ndio maelezo yetu ya kwanza kuhusu Sila. Tunajifunza nini kumhusu? (Yeye ni kiongozi, ana uwezo wa kuwatia moyo waumini, na ana karama ya unabii.)
    1.    Soma Matendo 15:35-38. Paulo ana maoni gani kuhusu Barnaba kumchukua Yohana Marko aende pamoja nao? (Soma Matendo 13:13. Hapo awali Yohana Marko alisafiri pamoja nao, lakini akaamua kwamba hataki kuendelea na safari. Inaonekana hakufurahia mambo magumu.)
      1.    Je, una huruma yoyote kwa Yohana Marko? (Mara baada ya Yohana Marko kuondoka, tunajifunza katika Matendo 14:19 kwamba Paulo alipigwa mawe – na watu walidhani kuwa alikuwa amefariki kutokana na kupigwa mawe! Bila shaka wasomaji wengi wangependa kuepuka jambo hilo!)
    1.    Soma Matendo 15:39. Watoa maoni mbalimbali wanasema kuwa Barnaba alikuwa mjomba wa Yohana Marko. Unadhani nani yuko sahihi kwenye huu ubishani? Je, Barnaba anakuwa na upendeleo kutokana na uhusiano wa kifamilia? Je, Paulo anasahau kwamba Mungu aliwapatia wanadamu nafasi ya pili ya kufanya uamuzi?
      1.    Soma Mithali 25:19. Ushauri huu unaonya nini kuhusu kumchukua Yohana Marko?
      1.    Soma Wakolosai 4:10 na 2 Timotheo 4:11. Hii inatuambia kuwa nani yuko sahihi kwenye huu ubishani kati ya Paulo na Barnaba? (Inabainika kwamba Yohana Marko anakuwa mtumishi wa kuaminika, anaaminika sana kiasi kwamba hata Paulo anamwomba usaidizi wake.)
      1.    Mambo gani mazuri yanapatikana kwenye huu ubishani? (Sasa tuna timu mbili za kimisionari badala ya kuwa na kundi moja pekee. Yohana Marko “anafanywa upya” na kuthibitisha kuwa mtendakazi wa injili wa kutegemewa.)
      1.    Mambo gani mabaya yanapatikana kwenye huu ubishani? (Hatuwezi kusema kwa uhakika, lakini Paulo na Barnaba ni watu wawili wenye uwezo mkubwa. Hilo limepotea. Huenda kuwatenganisha ni jambo jema kwa sababu linawafanya wawafunze na kuwajengea uwezo viongozi wapya wa kimisionari.)
    1.    Soma Matendo 15:40-41. Je, kanisa linachukua pande kwenye huu ubishani au linaulaani? (Hatuna taarifa za kutosha kuweza kufahamu jambo hili. Paulo anapoondoka na Sila, washiriki wanawaunga mkono.)
      1.    Hatusomi tena habari yoyote kuhusu Barnaba katika kitabu cha Matendo. Kwa nini kisa kinaendelea kwa kumzungumzia Paulo badala ya Barnaba? Je, huo ni uthibitisho wa kanisa kuchukua upande wa Paulo?
  1.   Mwafaka Mtakatifu?
    1.    Soma Matendo 16:1-3. Muda mfupi uliopita kanisa lilikuwa limetatua suala la tohara. Paulo alikuwa mmojawapo wa watu waliopaza sauti kubwa dhidi ya tohara. Kwa nini Paulo anamtahiri Timotheo? (Ukipitia upya somo letu la Matendo 15, suala lilikuwa linahusu kuwatahiri Mataifa. Hakuna kitu chochote katika Matendo 15 kiachoashiria kuwa tohara ni jambo baya.)
      1.    Je, Timotheo ni mtu wa Mataifa? (Mishna (mwaka 230BK) anasema kuwa hadhi yako kama Myahudi inategemeana na mama wako, lakini ushirikishwaji wako kikabila unategemeana na baba wako. Haiko wazi sana kuwa kanuni hii inarudi nyuma kwa kipindi gani. Mambo ya Walawi 24:10-11 inataja hali hiyo. Kwa upande mwingine, kitabu cha Walawi kinamzungumzia huyu mwana “aliyechanganya damu” kama mtu “miongoni mwa Waisraeli.” Kwa upande mwingine, inamtofautisha kati “yake na Muisraeli.” Kimsingi mama wake Timotheo hakupaswa kumwoa mtu wa Mataifa. Kumbukumbu la Torati 7:1-5.)
    1.    Angalia tena Matendo 16:3. Hii inaashiria kuwa sababu gani ilisababisha Timotheo atahiriwe? (Ushawishi rika (peeer pressure)! “Wayahudi” walimfanya Paulo afanye hivi.)
      1.    Je, Paulo ni mtu asiye na uti? Je, hana kanuni ambazo anaweza kuzisimamia? (Soma 1 Wakorintho 9:20-21. Kanuni kuu ya Paulo (miongoni mwa wale anaowabainisha) ni kuwapata waongofu kwa kuwapelekea injili.)
      1.    Kanisa la Willow Creek nchini marekani ni maarufu kwa kuwapelekea injili watu walio nje ya mfumo wa kanisa lolote. Licha ya hayo, mara kwa mara huwa ninasoma ukosoaji wa watu wanaojifunza mbinu za uinjilisti za kanisa hili. Paulo angezungumzia nini kuhusu mbinu za kanisa la Willow Creek?
  1. Safari
    1.    Soma Matendo 16:6-10. Katika matukio mawili Roho Mtakatifu anaonekana kuwazuia Paulo na wasafiri wenzie wasiende kwenye uelekeo fulani, lakini wakati mwingine anampelekea Paulo maono. Unadhani kwa nini Roho Mtakatifu anatenda kazi katika hizi njia tofauti? Kwa nini tu asipeleke maono? (Huenda Paulo anafanana nasi, si mara zote tunamsikiliza Roho Mtakatifu kwa makini.)
    1.    Soma Matendo 16:13-14. Kwa kawaida Paulo anatafuta sinagogi lililopo katika mji kama sehemu ya kuanzia kupeleka injili kwa watu wengine. Kwa nini anaanza na “mahali pa kusali” kando ya mto? (Paulo anaishika Sabato kama siku maalumu ya ibada tofauti na yeye kutafuta sinagogi lililopo katika sehemu hiyo. Pia inaashiria kuwa huenda Filipi haikuwa na sinagogi.)
      1.    Tunajifunza nini katika njia anayoitumia Paulo kuufikia mji mpya? (Anawatafuta watu ambao tayari wamemgeukia Mungu. Ana nuru ya ziada, na anaamini (bila shaka kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu) kwamba ni bora kuanza na wale ambao tayari wana uhusiano wa namna fulani na Mungu.)
  1.   Kusafirisha Watu Kiharamu
    1.    Soma Matendo 16:16-18. Hii inaibua angalao maswali mawili yanayohangaisha akili:
      1.    Kwa nini roho mchafu anatangaza wokovu?
        1.    Je, hii inamaanisha kuwa wakati mwingine Shetani anatumia njia inayoonekana kuwa chanya ili kuhafifisha injili?
      1.    Kwa nini Paulo anamtoa pepo mchafu pale tu alipokuwa amesikitika? Kwa nini asimsaidie binti mara moja?
    1.    Soma Matendo 16:19-22. Huu mfumo wa “haki” unahangaisha akili. Je, mashtaka dhidi ya Paulo na Sila ni ya kweli? (Sio malalamiko halisi ya wamiliki wa watumwa. Hata hivyo, kwa kadri ambavyo Ukristo usivyo dini iliyothibitishwa, hii ni kweli.)
    1.    Soma Matendo 16:23-25. Kama ungekuwa umepigwa kisawasawa, na kisha miguu yako ikafungwa, je, ungeendelea kuimba nyimbo za kumsifu Mungu?
    1.    Soma Matendo 16:26-28. Paulo anawezaje kuwadhibiti wafungwa wengine? (Inaonekana kuna jambo limeachwa kwenye kisa hiki. Tunaambiwa kuwa wafungwa wengine wanasikiliza nyimbo zake. Lazima palikuwepo na mazungumzo ya namna fulani kati ya Paulo na Sila na wafungwa wengine.)
    1.    Soma Matendo 16:29-31. Nani mwingine alikuwa akiwasikiliza Paulo na sila (Mlinzi wa gereza.)
      1.    Paulo alipomwambia anachopaswa kukifanya mlinzi wa gereza ili aokoke, kwa nini hakuongezea kwamba awatibu vidonda wale waliopigwa na kuifungua miguu yao? (Imani kwa Yesu ndio ujumbe wa injili.)
    1.    Soma Matendo 16:32-34. Mlinzi wa gereza anafanya nini kama matokeo ya kuongoka kwake? (Anawaosha vidonda vyao, anawapa chakula na anabatizwa. Maisha yake yanajaa furaha.)
    1.    Soma Matendo 16:35-40 na Mathayo 5:39-40. Je, Paulo anakiuka amri ya Yesu aliyoitoa kwenye Hubiri lake pale Mlimani? (Soma Yohana 18:22-23. Tunaona kwamba Yesu na Paulo wanadai haki zao kisheria. Namna tunavyopaswa kuelewa fundisho la Yesu kuhusu kugeuza shavu jingine haiko wazi kwangu ikiwa tutachukulia kwamba Paulo na Yesu walifuata fundisho hili.)
    1.    Rafiki, wakati mwingine ni vigumu kuepuka mgongano. Paulo alikabiliana nao kanisani, alikabiliana nao kwenye uhusiano wake na Barnaba, na alikabiliana na wale wanaosafirisha watu kwa njia haramu na uongozi wa eneo lake mahalia. Je, utamwomba Roho Mtakatifu ili abadili migongano unayokabiliana nayo na kuwa jambo linaloitangaza injili?
  1.    Juma lijalo: Safari ya Tatu ya Kimisionari.