Safari ya Roma

(Matendo 27 & 28)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
13

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Paulo alikata rufaa Rumi! Juma lililopita tulijifunza kwamba Paulo angeweza “asikutwe na hatia” ya mashtaka ya jinai dhidi yake – au hivyo ndivyo mahakimu walivyoambiana wao kwa wao pembeni. Lakini, Paulo alikuwa na shaka kuwa angegeuziwa kibao kwa Wayahudi, na hivyo akakata rufaa kwa Kaisari kule Rumi. Mara kwa mara wateja wangu huwa wanaona kwamba mfumo wa mahakama unafanya kazi taratibu sana kuliko matarajio yao. Paulo anaona jambo hilo hilo kwa upande wake. Juma hili tunaona ucheleweshwaji wa safari ya Paulo kwenye hatua inayofuata ya kesi yake. Hebu tuchimbue Biblia yetu na tujifunze zaidi!

 

 1.    Kuandaa Safari ya Majini

 

  1.    Soma Matendo 27:1-2. Kifungu chetu kinasema “Aristarko, Mmakedonia wa Thesalonike, akiwa pamoja nasi.” “Nasi” ni nani? (Kwa kuwa Luka ndiye aliyeandika kitabu cha Matendo, lazima hiyo itakuwa inawarejea angalao Luka na Paulo.)

 

   1.    Nani anayeshughulikia usafiri wa wafungwa? (Akida aitwaye Yulio.)

 

  1.    Soma Matendo 27:3. Mtazamo wa akida dhidi ya Paulo ukoje? (Ni mwema kwake. Ni baraka ya pekee.)

 

  1.    Hebu turuke vifungu kadhaa hadi Matendo 27:9-12 na uvisome. Ungefuata ushauri wa nani? Ushauri wa mhubiri mfungwa, au ushauri wa nahodha wa merikebu?

 

  1.    Soma Matendo 27:14-20. Je, una uzoefu wa kutoa ushauri sahihi kwa kundi la watu ambao hawakuuafiki? Na, walipoukataa ushauri wako, kitendo hicho kikakuingiza kwenye matatizo makubwa? (Hicho ndicho anachokipitia Paulo. Anaweza kufa.)

 

  1.    Soma Matendo 27:21. Je, Paulo ni mtu wa aina ya “si niliwaambia?” (Yuko hapa. Lakini, nadhani Paulo ana mtazamo mwingine tofauti na kuonesha kuwa alikuwa sahihi na wao hawakuwa sahihi.)

 

  1.    Soma Matendo 27:22-26. Je, ungemwamini Paulo endapo ungekuwa mmojawapo wa watu kwenye kundi lile?

 

   1.    Unadhani kwa nini Paulo anawaambia kile anachokifahamu? (Kinapaswa kumtia moyo kila mtu. Kwa kuongezea, kitawahamasisha kumwamini Yesu, ambaye ni Mungu wa Paulo.)

 

  1.    Soma Matendo 27:29-32. Nani anayemwamini Paulo na nani asiyemwamini? (Hapa tunaweza kuona kuwa Yulio na askari wa Kirumi wameshawishika. Mabaharia hawajashawishika. Ukweli kwamba mabaharia wanajaribu kujiokoa kwa gharama ya watu wengine inaonesha dosari ya tabia yao.)

 

  1.    Soma Matendo 27:33-37. Maana ya ndani kabisa ya mabaharia kutupa nafaka baharini ni ipi? (Wameshawishika kuwa hawatahitaji tena kula wakiwa ndani ya merikebu. Hivyo, inaonekana kwamba sasa wote wanamwamini Paulo. Hata hivyo, kwa hawa mabaharia, inawezakana waliamini kuwa watakwama miambani.)

 

  1.    Soma Matendo 27:41-43. Je, sasa askari hawamwamini Paulo? (Paulo alisema kuwa kila mtu ataokoka. Hata hivyo, alionekana kuzungumzia habari ya dhoruba. Hakusema lolote kuhusu kutoroka baadaye – isipokuwa kumhusu yeye. Alisema kuwa atasimama kizimbani mbele ya Kaisari. Kwa bahati nzuri, akida anamwamini Paulo na kumwokoa.)

 

 1.   Kisiwani Melita

 

  1.    Soma Matendo 28:1-6. Muda gani ulipita tangu watu walipodhani kuwa Paulo alikuwa muuaji na kipindi walipodhani kuwa alikuwa mungu?

 

   1.    Hii inatuambia nini kuhusu uhuru wetu wa dini? (Watu wanaweza kubadili mawazo yao haraka sana.)

 

   1.    Hii inatufundisha nini kuhusu upelekaji wa injili? (Watu wanaweza kufikia hitimisho potofu.)

 

   1.    Soma Marko 16:17-18. Kifungu kinaposema, “watashika nyoka kwa mikono yao,” je, kinazungumzia juu ya hatari za makusudi au Yesu anazungumzia hali ya Paulo? (Ishara zote hizi ni zana za msaada sana kwa wamisionari. Nadhani Yesu anazungumzia hali ya Paulo.)

 

  1.    Soma Matendo 28:7. Kwa nini jambo hili lilitokea? Paulo ni mfungwa wa Rumi anayepelekwa kushtakiwa? Kwa nini mkuu wa kisiwa anamkaribisha nyumbani kwake?

 

  1.    Soma Matendo 28:8-10. Paulo anawaponya wagonjwa wote. Huko nyuma, tuliposoma aina zote hizi za miujiza, mara kwa mara Luka anabainisha kuwa watu wengi sana wanaongolewa. Kwa nini hakuna uongofu unaotaarifiwa? Tayari watu wanadhani kuwa Paulo ni mungu, kwa hiyo haipaswi kuwa vigumu kwa wao kuongolewa. (Huenda jambo hili halikutaarifiwa. Huenda bado watu hawakuwa tayari kuamini.)

 

 1. Rumi

 

  1.    Soma Matendo 28:13-15. Hatimaye Paulo anawasili Rumi. Unadhani kwa nini Paulo anatiwa moyo kwa huku kukutana na Wakristo wenzake? (Hawajamsahau wala kumtelekeza. Badala yake, walisafiri umbali fulani ili tu kukutana naye. Wanataka kuwa pamoja naye.)

 

  1.    Soma Matendo 28:16. Unadhani hili ni jambo la kawaida? Paulo si tu kwamba anapata nafasi ya kuishi kivyake, lakini pia anaye askari mmoja pekee. Petro, kama ilivyoelezwa kwenye Matendo 12, hakuweza kulegezewa au kufunguliwa minyororo alipokuwa amefungwa kwenye chumba cha ndani kabisa cha jela, na kulindwa na askari wengi! (Hii si kawaida. Bila shaka ndio maana Liwali Festo aliandika kuwa anadhani Paulo hakuwa na hatia.)

 

  1.    Soma Matendo 28:17-20. Kwa nini viongozi wa Kiyahudi watake kwenda kwenye kikao kilichoitishwa na Paulo? Kwa nini wadhani kuwa ni jambo la muhimu kiasi cha kuwachukulia muda wao? (Ninahisi palikuwepo na idadi ndogo ya Wayahudi kule Rumi. Jamii ingekuwa na hamu ya kumsikiliza mfungwa wa Kiyahudi aliyeelimika sana na ana hali ya “ufungwa” usio wa kawaida.)

 

   1.    Paulo anayaelezeaje mashtaka dhidi yake? (Kama ya kiteolojia. “Nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli.”)

 

  1.    Soma Matendo 28:21-22. Viongozi wa Kiyahudi hawajasikia jambo lolote kumhusu Paulo, lakini wamesikia kwamba Wakristo ndio tatizo. Kama ungekuwa Paulo, je, hii ingekuwa habari njema au mbaya?

 

  1.    Soma Matendo 28:23. Paulo anawavuta watu wengi sana. Anatumia njia gani kujaribu kulishawishi kundi hili? (Anajenga hoja kutokana na kile ambacho tayari wanakifahamu.)

 

  1.    Soma Matendo 28:24-26. Je, Paulo anawatukana? (Kwa mara nyingine, anajenga hoja kutokana na kile ambacho tayari wanakifahamu. Anawakumbusha kuwa mababu zao walionywa kuhusu kutokuamini.)

 

  1.    Soma Matendo 28:27. Kauli hii ya Isaya inaweza kutumikaje? Mioyo yao ina usugu kiasi gani? Hawajawahi kumsikia Paulo hapo kabla, lakini wako radhi kwenda kumsikiliza. (“Usugu” hautokani na kuukataa ujumbe wa injili kwa kurudia-rudia, bali kwa kuridhika na imani zao za sasa. Lazima tuwe wepesi kubadilika kwenye uongozi endelevu wa Roho Mtakatifu.)

 

  1.    Soma Matendo 28:28. Hii inaweza kuwa matusi kwa Wayahudi. Je, tunapaswa kupeleka injili kwa matusi? (Paulo hakuanza kwa matusi. Lakini, yumkini rejea ya mababu zao kukataa kusikiliza ni matusi, na kauli kwamba Mataifa watafanya vizuri zaidi ni matusi!)

 

   1.    Lengo la Paulo kwa matusi yake ni lipi? (Anataka kuwaondosha kwenye ridhaa. Anataka kupenya mioyo yao migumu.)

 

  1.    Soma Matendo 28:30-31. Vipi kuhusu rufaa yake kwa Kaisari? Vipi kuhusu kesi yake? Kwa nini tunaachwa hewani kuhusu hitimisho? Au, je, hili ndilo hitimisho? (Hatusomi habari za kesi na jinsi ilivyoishia. Lakini, kwa namna fulani hivi tunalo hitimisho. Maisha ya Paulo hayaendi kama jinsi anayotaka yaende. Amewekwa kizuizini na serikali. Licha ya hayo, Paulo anaendelea kuhubiri injili “kwa ujasiri mwingi.” Hili ndilo hitimisho linalotumika kwetu sisi tunaokabiliana na magumu.)

 

  1.    Soma 2 Timotheo 4:6-8. Paulo anatarajia kuwa mustakabali wake utakuwaje? (Anaamini kuwa muda wa kufa kwake umewadia, lakini kamwe Biblia haituelezei kifo chake kwa umahsusi. Maandiko ya Eusebi yanatutaarifu kuwa Paulo alikatwa kichwa wakati wa utawala wa Mfalme Nero wa Rumi. Nero alilaani kuchomwa kwa Rumi kwa Wakristo.)

 

   1.    Je, unatazamia kipindi ambacho mabalaa yanausonga ulimwengu na Ukristo unalaumiwa kwa mabalaa hayo?

 

  1.    Rafiki, je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie uwe kama Paulo – uendelee kuwa jasiri na kuendelea kuhubiri injili hata kama nguvu za uovu zinayafanya mambo yawe magumu kwako?

 

 1.   Juma lijalo: Tunaanza mfululizo mpya kuhusu umoja ndani ya kanisa uitwao “Umoja Katika Kristo.”