Somo la 2: Sababu za Kutokuwa na Umoja

Swahili
(Kumbukumbu la Torati 28, 1 Wafalme 12, 1 Wakorintho 1)
Year: 
2018
Quarter: 
4
Lesson Number: 
2

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Kwa nini Mungu anatupatia amri zake? Je, ni jaribio ili kuona kama “tu wema kiasi cha kutosha” kuweza kuokolewa? Au, kuwa wema kiasi cha kutosha kuwa na uhusiano sahihi na Mungu? Watu wengi wanafikiria hivyo, lakini hivyo sivyo Biblia inavyofundisha. Kumbukumbu la Torati 4:5-8 inatuambia kuwa Mungu anatupatia “amri na hukumu” ili kutufanya kuwa na “hekima na akili.” Mungu anatupatia maelekezo yake maishani ili kutubariki maisha ya hali ya juu. Kuishi maisha mazuri humpa Mungu utukufu na kwetu pia. Hebu tuchimbue somo letu la Biblia na tujifunze zaidi kuhusu sheria za Mungu na umoja!

 

 1.    Kuishi Maisha ya Yaliyotukuka!

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 28:1-2. Ni nini matokeo ya kuzingatia amri za Mungu na kuzitii? (Tunatukuzwa “juu ya mataifa yote ya duniani.”)

 

   1.    Je, bado hii ni kweli? Au je, hii ni ahadi iliyotolewa kwa Israeli pekee? (Soma Kutoka 19:5-6 na Warumi 2:28-29. Katika Kutoka 19, “agano” ambalo Mungu anawaandaa watu wake ni Amri Kumi. Katika Warumi 2 tunajifunza kwamba tunakuwa Wayahudi wa kiroho ikiwa tutaishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu. Ikiwa unaamini kuwa bado Amri Kumi ni mwongozo wa maisha yako, na Roho Mtakatifu anasaidia kukuongoza kuishi maisha makamilifu, haina mantiki kuamini kwamba thawabu ya kuishi maisha makamilifu haipo tena. Badala yake, Amri ni mwongozo wa mtengenezaji (mwenye kiwanda) wa kuishi maisha ya hali ya juu.)

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 28:3-6. Hebu tujaribishe hii dhana. Je, kuwa na watoto na mazao mazuri na wanyama wazuri inategemeana na juhudi zako? Je, unaweza kuona uhusiano wa moja kwa moja na utii? (Hatuwezi kuidhibiti hali ya hewa. Kipindi cha nyuma hawakuweza kudhibiti uzalianaji. Hivyo, tunatakiwa kukiri kwamba baraka hizi sio tu jambo la kutumia nguvu – tii na ufanikiwe. Aina ya usitawi ambao Mungu anauelezea inahusisha baraka zake alizozielekeza. Mtazamo sahihi kabisa wa jambo hili ni kwamba Mungu anatupatia maelekezo ya kuishi maisha mazuri, na Mungu anaingilia kati kwa niaba yetu ili kuyaboresha zaidi.)

 

   1.    Unawafahamu watu wanaotilia shaka jambo hili? Je, hatuwakosoi viongozi wa dini wa nyakati za Yesu kwa sababu walidhani kuwa walikuwa bora kwa kuwa walitii na kubarikiwa? (Kila mmoja wetu amemwona mtu ambaye amepata mateso kutokana na kutokutii. Mchunguzi makini hawezi kukana uhusiano uliopo kati ya utii na maisha bora.)

 

   1.    Tunawaelezeaje wanafunzi, Paulo na Yesu: je, wote hawakuwa na wakati mgumu? (Walikuwa na nyakati ngumu sana, lakini nadhani pia walikuwa kwenye mazingira mahsusi na ya kipekee. Fikiria wangeweza kukabiliana na magumu gani mengine ya ziada endapo maisha yao yangehusisha kutomtii Mungu mara kwa mara?)

 

  1.    Hebu turuke hadi chini na tusome Kumbukumbu la Torati 28:9-11. Je, ungependa kuwa na “wingi wa uheri?”

 

   1.    Baadhi ya watu wanabishana kuhusu maana ya “uheri (usitawi).” Mungu anatoa usitawi wa aina gani? Je, ni kujisikia vizuri tu kuhusu utii? (Hapana. Mungu anaelezea kwa usahihi kabisa kile anachokimaanisha kwa usitawi: watoto wengi na biashara yenye mafanikio. Kama bado huna uhakika, soma Kumbukumbu la Torati 28:12.)

 

   1.    Je, unadhani kwamba utii kwa Mungu ndio “habari kubwa kutuhusu?” Je, huu si ukaribisho wa kuwa wachoyo? (Vifungu hivi vinayahusisha maisha yetu mazuri na Mungu wetu. Kwa kuishi maisha sahihi yenye matokeo mazuri, tunampa Mungu utukufu.)

 

   1.    Ninaye rafiki wa miaka mingi ambaye haonekani tena kujali habari ya kumtii Mungu. Ni mkosoaji mkubwa wa Joel Osteen, mchungaji mwandamizi wa Kanisa la Lakewood, kwa sababu ya nyumba yake. Anaishi kwenye nyumba yenye eneo la futi za mraba 17,000. Wastani wa mahudhurio katika Kanisa la Lakewood ni watu 52,000 kila juma! Ikiwa kila mchungaji angeishi kwenye nyumba ambayo eneo lake la mraba kwa futi ni 1/3 ya idadi ya watu wanaohudhuria kanisani kwake, je, hilo litakuwa tatizo?

 

  1.    Kwa kuwa somo letu linahusu kutokuwa na umoja, kuna uwezekano wa uwepo wa uhusiano gani kati ya usitawi na umoja? (Mpango wa Mungu ilikuwa ni kuwa na watu wenye mafanikio na usitawi watakaotia alama maisha ya kumfuata Mungu wa kweli wa mbinguni. Ikiwa kundi hili lina malengo yale yale na kanuni zile zile, na ikiwa wanatambua thamani ya kuwa sehemu ya hii jumuiya, hilo huleta umoja.)

 

 1.   Kugawanyika kwa Ufalme

 

  1.    Soma 1 Wafalme 11:42-43. Je, Sulemani alikuwa Mfalme mzuri?

 

  1.    Soma 1 Wafalme 12:1-4. Rehoboamu atakwenda kuchukua nafasi ya Mfalme Sulemani, lakini bado tukio hilo halijatokea. Watu wanamwomba nini kabla hawajamfanya kuwa mfalme? (Kupunguza viwango vya juu vya kodi.)

 

  1.    Soma 1 Wafalme 12:5. Unalichukuliaje jibu la Rehoboamu kwenye madai haya? (Anaonesha busara kwa kutokujibu mara moja.)

 

  1.    Soma 1 Wafalme 12:6-7. Wazee wanapendekeza uongozi wa aina gani kwa Rehoboamu? (Uongozi wa kiutumishi. Wasikilize watu nao watakufuata. Rehoboamu anaonesha kwamba anahitaji ushauri.)

 

  1.    Soma 1 Wafalme 12:8-11. Vijana wanapendekeza uongozi wa namna gani? (Kutawala kwa njia ya kutia hofu.)

 

  1.    Rehoboamu anaukubali ushauri wa vijana. Hebu tusome 1 Wafalme 12:16-20. Watu wanaitikiaje ahadi ya Rehoboamu ya kutawala kwa njia ya kutia hofu?

 

  1.    Hebu turudi nyuma na tusome kifungu tulichokiruka. Soma 1 Wafalme 12:15. Nani yuko nyuma ya huu uasi? (Mungu.)

 

   1.    Kama unataka kuelewa kikamilifu maelezo kamili ya ahadi ya Rehoboamu, soma 1 Waflame 11. Baadaye maishani, Sulemani hakuwa mwaminifu kwa Mungu. Mungu alimwahidi Rehoboamu, kama sehemu ya adhabu ya Mfalme Sulemani, kwamba Rehoboamu ataongoza makabila kumi baada ya kifo cha Sulemani.)

 

   1.    Hebu turudi kwenye suala la kutokuwa na umoja. Hadi hapa tulipofikia tunapaswa kujifunza nini? Hebu tujiulize maswali machache:

 

    1.    Je, mafanikio na utajiri vinasababisha uwepo wa umoja? (Mungu alimbariki Sulemani – kwa mujibu wa ahadi tulizozijadili katika sehemu ya kwanza. Lakini, utajiri na mafanikio ya Sulemani vilimfanya amgeukie Mungu. Matokeo yake ilikuwa ni madhara na kutokuwa na umoja kwenye ufalme wake.)

 

    1.    Tunapaswa kujifunza uongozi wa kanisa wa namna gani?  Au, je, ahadi ya Mungu kumwadhibu Sulemani inapita mambo yote tunayoweza kujifunza kuhusu uongozi? (Rehoboamu aliusikiliza ushauri wa watu waliokuwa wabinafsi na wenye kiburi. Hawa washauri vijana walinufaika na kodi kubwa waliyotozwa watu. Usitawi wa Mungu huwabariki watu wote. Pacha mwovu wa usitawi, ulafi, huchukua fedha kutoka kwa watu. Somo kwa viongozi wa kanisa ni kuwa waaminifu kwa Mungu, na kuepuka kuwatwika mzigo washiriki isivyo sahihi.)

 

    1.    Je, wakati mwingine uasi ni mpango wa Mungu? (Katika sakata hili, ilikuwa ni mpango wa Mungu. Lakini, Biblia inaonya kwa kurudiarudia dhidi ya mwasi. Mfano, Mithali 24:21-22.)

 

 1. Mgawanyiko wa Kanisa

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 1:10. Hili lina uhalisia kwa kiasi gani? Je, tunaweza tu kuwaambia watu wakubaliane na jambo? Je, panaweza kuwepo na mjadala juu ya asili ya makubaliano?

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 1:11-12. Chanzo cha tatizo ni kipi? (Watu wana viongozi wanaowapenda.)

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 1:13. Sasa Paulo anaingia kwenye hoja yake yenye mantiki dhidi ya mgawanyiko. Hoja ya Paulo ni ipi? (Kwamba sote tuna umoja katika Kristo. Wajibu wa kiongozi wa Kikristo na kuwaelekeza watu kwa Yesu, na si kuwaelekeza kwake.)

 

  1.    Tunaweza kupata fundisho gani kwenye kisa hiki ili kusaidia kuleta umoja kanisani leo? (Tunatakiwa kujikita kwenye umoja wetu katika Kristo. Mtu aliyetuongoa au aliyetubatiza hapaswi kuwa kitovu cha maisha yetu ya kiroho.)

 

  1.    Soma Matendo 20:27-31. Kuna vihatarishi gani vingine kwenye umoja? (“Mbwa mwitu wakali.”)

 

   1.    Jambo gani linahusika katika “kujitunza nafsi zenu na lile kundi lote nalo?” Je, tunapaswa kuchukua hatua madhubuti? Ikiwa ndivyo, hatua hizo ni zipi?

 

  1.    Soma Mathayo 13:24-30. Suluhisho la Yesu ni lipi?

 

   1.    Ni nini maana ya onyo la Yesu kuhusu “kuzing’oa ngano” wakati “wanakusanya magugu?” (Wakristo wazuri wanaweza wasielewe mambo yote. Kwa matatizo yaliyo mengi, ni vyema tu kuachana nayo.)

 

   1.    Vipi kama una mwalimu au mhubiri ambaye ni “mbwa mwitu?” (Hili ni tatizo kubwa zaidi kuliko tu gugu linalokua pamoja na ngano. Hii ni sawa na adui aliyepanda magugu. Kanisa halipaswi kumtegemeza kifedha adui anayepanda magugu.)

 

  1.    Rafiki, je, unauthamini umoja kanisani? Ikiwa hauuthamini, je, ni kwa sababu hutambui baraka kamili za kuwa na umoja na Yesu? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu akuoneshe mapenzi ya Mungu vizuri zaidi kwa ajili ya maisha yako?

 

 1.   Juma lijalo: “Wote Wawe na Umoja.”