Umoja Katika Imani

(Mathayo 25, Waebrania 6 & 8, Matendo 4)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
4
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Ninapowafikiria wale ambao kwa sasa ni marafiki wangu wa karibu ndani na nje ya kanisa, mawazo yao yanafanana sana na mawazo yangu. Pamoja na ukaribu sana wa makubaliano yetu, katika kila jambo pia kuna angalao eneo moja ambapo hatukubaliani. Mtu wa pekee tofauti na marafiki hao ni mke wangu, na hata kwake ninaweza kufikiria mada ambayo tunaweza tusikubaliane, lakini, kimsingi, ninakuwa na mawazo yasiyo sahihi. Wakati mwingine hatutambui kiwango cha kutokukubaliana na marafiki kwa sababu tunakuwa tu na mijadala ya juujuu. Mwishoni mwa juma lililopita, rafiki wangu alishangazwa sana na mawazo yangu nami nilishangazwa na mawazo yake. Mjadala ulinifanya nijisikie vibaya na kutafakari kama tulipaswa kujiingiza kwenye mijadala ya juujuu. Kuna msemo wa kale usemao “chuma hunoa chuma.” Je, suala la kutokubaliana si la msaada katika kuyanoa mawazo yako? Au, je, tunatakiwa kuepuka maeneo ya mjadala tusiyokubaliana? Hebu tuzame kwenye somo letu na tuone kama Biblia inatoa mwanga wowote kwenye suala hili!

 

 1.    Wanawali Kumi

 

  1.    Soma Mathayo 25:1-4. Niambie mambo yanayofanana kwa wanawali kumi? (Wote wana misheni moja. Wote wana utambulisho mmoja. Wote wanategemea kifaa cha aina moja na chanzo kimoja cha nishati.)

 

   1.    Kuna tofauti gani kati yao? (Nusu yao wanaleta mafuta ya ziada. Nusu yao wanaitwa “wapumbavu” na nusu wanaitwa wenye “busara.”)

 

  1.    Soma Mathayo 25:5-8. Kwa nini nusu ya wanawali wanaitwa “wapumbavu?” (Kwa sababu hawakuleta mafuta ya kutosha.)

 

   1.    Tunaambiwa kuwa wanawali hawa kumi walikuwa wakisubiria na wakalala. Vipi kama wangeutumia muda huo kujadili kiasi sahihi cha mafuta walichotakiwa kukibeba? Kama hawakuwa wameungana katika kusubiri na kulala, badala yake wangekuwa wanajadili akiba sahihi ya mafuta, yumkini tatizo hili lingeepukwa?

 

  1.    Soma Mathayo 25:9. Vipi kama wangetumia muda huo kujadili suala la kimaadili la kutumia rasilimali kwa pamoja. Je, huenda hilo lingeepusha tatizo?

 

  1.    Soma Mathayo 25:10-13. Kwa nini mlinzi mlangoni hawajui wanawali watano wapumbavu?

 

   1.    Mlinzi mlangoni anaposema kuwa mtazamo unaotakiwa ni “kesheni,” je, hilo liliwaelezea wanawali watano wenye busara ni watu wa namna gani? (Wote “walisinzia na kulala usingizi.” Hakuna aliyekesha, wote kwa pamoja waliamshwa na “kelele za usiku wa manane.”)

 

   1.    Ikiwa kiuhalisia “kukesha” si kuwa makini, je, inamaanisha nini? (Inamaanisha kujiandaa kwa kuwa na mafuta ya kutosha.)

 

  1.    Kwa kuwa huu ni mfano, hebu niambie, unadhani mafuta yanawakilisha nini? (Nadhani watu wengi watasema yanamaanisha Roho Mtakatifu au huenda neema.)

 

  1.    Soma Yohana 16:7-11. Huyu “Msaidizi” ni nani? (Ni Roho Mtakatifu.)

 

   1.    Ni muhimu kiasi gani kuwa na Roho Mtakatifu? Vipi kuhusu kuwa na “Roho Mtakatifu” wa ziada? (Kutokana na mfano wa wanawali, ikiwa maelezo haya yanahusu wajibu wa Roho Mtakatifu, kuwa na Roho wa Mungu ni muhimu kwa wokovu.)

 

   1.    Ni muhimu kiasi gani kuwa na umoja kwenye suala la Roho Mtakatifu? (Ni imani ya muhimu.)

 

   1.    Kwa mara nyingine, je, wanawali kumi walipaswa kutumia muda wao kwenye mjadala wa Roho Mtakatifu na kuhatarisha umoja wa usingizi na kulala?

 

    1.    Kama umejibu, “ndiyo,” je, hiyo inamaanisha kuwa si mara zote umoja ndilo lengo kuu? Au, je, inamaanisha kwamba wakati mwingine unatakiwa kupitia kwenye mjadala ili kuufikia umoja?

 

 1.   Kuhani Mkuu

 

  1.    Soma Waebrania 8:1-2 na uilinganishe na Mathayo 27:50-53. Pazia gani la hekalu linazungumziwa kwenye Mathayo 27:51? (Soma Waebrania 6:19-20. Vifungu hivi vinatuonesha kwamba wakati wa kuteswa kwa Yesu pazia la hekalu linalotenganisha patakatifu na patakatifu pa patakatifu lilipasuka vipande viwili. Tunafahamu kwamba Yesu aliingia “hekalu la ndani zaidi” (patakatifu pa patakatifu) kwa niaba (ajili) yetu kama Kuhani wetu Mkuu.)

 

  1.    Soma Waebrania 8:5. Tunafahamu nini kuhusu helaku la duniani? (Musa aliambiwa kupangilia hekalu la jangwani kwa mfano wa ubunifu wa hekalu la mbinguni. Ubunifu huu huu ulitumika kwenye hekalu la Kiyahudi la kipindi cha Yesu.)

 

  1.    Soma Waebrania 10:19-22. Hii inazungumzia nini kuhusu “pazia?” (Inaliita “mwili” wa Yesu.)

 

  1.    Angalia tena Waebrania 6:19-20 na Waebrania 8:1-2. Ukweli gani wa msingi umefunuliwa kwenye kitabu cha Waebrania? (Kafara zilizotolewa kwenye hekalu la Kiyahudi zilikuwa ni namna ya kuondoa dhambi. Hekalu la kale na kafara zake ziliashiria kile ambacho Yesu atakuwa akikifanya siku zijazo kwa ajili yetu. Yesu alitimiza ishara hiyo. Pazia lililotenganisha patakatifu na patakatifu pa patakatifu lilifutwa msalabani. Pazia halisi kwenye hekalu la duniani lilipasuka, mwili wa Yesu uliporaruliwa. Huu ndio ujumbe wa injili, kwamba kafara ya Yesu kwa ajili yetu hutupatia nafasi ya kuuendea uwepo wa Mungu. Yesu ni Kuhani wetu Mkuu anayejitokeza kwa ajili yetu mahali patakatifu sana.)

 

  1.    Si Wakristo wote wanakubaliana na suala la muda – muda ambao Yesu alianza kazi yake ya utume mbinguni kama Kuhani wetu Mkuu. Je, hili ndilo jambo la msingi ambalo umoja ni wa muhimu? Ikiwa ndivyo, kwa nini? Ikiwa sivyo, jambo la muhimu kwa ajili ya umoja ni lipi?

 

   1.    Kwenye kisa cha Wanawali Kumi, je, suala la muda lilikuwa jambo la muhimu? (Kama ungeuelewa muda halisi ungejiandaa vizuri zaidi. Lakini, hakuna hata mmoja kati ya wanawali kumi aliyepatia kwenye suala la muda. Badala yake, suala la muhimu zaidi ilikuwa ni kuwa na mafuta ya ziada – uwepo wa Roho Mtakatifu.)

 

 1. Sabato

 

  1.    Soma Mwanzo 2:1-4. Sabato ni ukumbusho wa nini? (Kazi ya Mungu kama Muumbaji wetu.)

 

  1.    Soma Kutoka 20:8-11. Kumbukizi hii ya kuitunza Sabato ni ukumbusho wa nini? (Kazi ya Mungu kama Muumbaji wetu.)

 

  1.    Soma Mathayo 27:58-64, Mathayw 28:1-3, na Mathayo 28:5-6. Nimekufanya uvisome vifungu hivi kwa sababu vina rejea mahsusi ya siku mbalimbali. Yesu alisulubiwa siku gani, na alifufuka kutoka kaburini siku gani? (Alisulubiwa siku ya Ijumaa na kufufuka siku ya Jumapili.)

 

   1.    Kwa nini Yesu alipumzika kaburini siku ya Jumamosi? (Biblia haibainishi jambo hili kwa umahsusi, lakini mantiki iliyopo ni kwamba Yesu alishangilia ushindi wake dhidi ya dhambi.  Hakuwaumba tu wanadamu, bali pia sasa amewaokoa kutoka kwenye mauti ya milele.)

 

  1.    Unapotafakari maana ya Sabato, kile inachokumbushia, je, hili ndilo jambo la imani ambalo Wakristo wanapaswa kuwa na umoja?

 

   1.    Je, hili linafanana na mjadala wetu wa awali kuhusu suala la muda? Suala la muda ni jambo la kina, makubaliano ya Wakristo yanatakiwa juu ya kitu? (Hili haliwezi kurejeshwa hadi kufikia kuwa suala la kujadilika, kwa sababu amri ya dhahiri inahusu suala la muda. “Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.” Mwanzo 2:3.)

 

 1.   Yesu

 

  1.    Soma Matendo 4:5-7. Kwa nini viongozi wa Kiyahudi waliuliza hili swali? Kwani bado hawakulijua jibu? Je, hili si swali sahihi kwa Petro kuielezea injili?

 

  1.    Soma Matendo 4:8-11. Hii inazungumzia nini kumhusu Yesu? (Kwamba Mungu alimfufua kutoka katika wafu.)

 

  1.    Soma Matendo 4:13-14. Hii inaashiria nini kuhusu sababu ya viongozi wa Kiyahudi kuuliza swali walilouliza? (Walidhani wanafunzi watawaogopa. Utaona kwamba Matendo 4:8 inasema kuwa Petro “alijaa Roho Mtakatifu.” Viongozi wa Kiyahudu walipata zaidi ya walichokitarajia.)

 

  1.    Hebu turudi nyuma na tusome kifunu nilichokiruka: Matendo 4:12. Ni muhimu kiasi gani kuelewa na kukubaliana na jambo hili?

 

   1.    Tunapozungumzia masuala ya imani ambayo lazima tuwe na umoja nayo, hili lipo kwenye nafasi gani? (Ni jambo la muhimu sana. Ikiwa hatukubaliani na jambo hili, basi hatukubaliana na mpango wa wokovu. Tumeliweka jambo la msingi zaidi kuwa la mwisho, kwa sababu imani yetu yote inapaswa kujengwa kwenye ukweli huu.)

 

  1.    Rafiki, je, unakubaliana na mambo yote tuliyoyajadili? Ikiwa hukubaliani, fanya uamuzi endapo unapaswa kuwa na mjadala wa dhati, au uutegemee umoja unaotokana na uhusiano wa juujuu. Mwombe Roho Mtakatifu akuongoze katika kubainisha masuala yanayohitaji mjadala wa dhati.

 

 1.    Juma lijalo: “Uthibitisho Makini Zaidi.”