Nayafanya Yote Kuwa Mapya
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mfululizo wetu wa masomo unairuka Ufunuo 18. Sura hiyo inatuambia kuwa kuna huzuni nyingi kwa watu wanaopata fedha na kunufaika kutokana na uovu. Kwa anguko la Babeli, wako nje ya biashara. Juma hili mambo yanabadilika. Tunaanza na Ufunuo 19 na furaha ya wale ambao sasa ni washindi kwa njia ya uwezo wa Yesu. Wameteseka sana chini ya uovu, lakini uovu unapotea kwa kasi. Hebu tuzame kwenye somo letu na tujifunze zaidi juu ya mustakabali wetu wenye furaha!
- Furahini!
-
- Soma Ufunuo 19:1-3. Tunaona muziki wenye kuchosha zaidi, sawa? (Hapana. Tunaona sifa zenye makelele.)
-
-
- Kwa nini watu wa Mungu wanampa sifa? (Mungu ametoa hukumu. Mungu ameonesha uwezo wake. Mungu amelipiza kisasi damu ya wafuasi wake. Amewala kwa “moshi” maadui wake (na wetu).)
-
-
- Soma Ufunuo 19:6-8. Sifa zenye makelele zaidi na sauti kama ya radi. Sababu ya sifa hizi ni ipi? (Ni siku ya harusi yetu na Yesu! Huu ndio wakati tutakapokuwa pamoja naye milele.)
-
-
- Nini kinatustahilisha kuingia? (Vazi la Yesu la haki. “Alipewa kitani nzuri, ing’arayo na safi ili aivae.”)
-
-
-
-
- Tunalipataje vazi hilo? (“Tunapewa.”)
-
-
-
-
- Hebu subiri kidogo! Kwenye tafsiri ya NIV kuna mabano: “Kitani safi inamaanisha matendo ya haki ya watakatifu.” Hiyo inaonekana kama vile vazi la haki linawakilisha matendo yetu! Inawakilisha kazi yetu. Tunawezaje kupewa vazi kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine tulipate kwa “matendo yetu ya haki?”
-
-
-
- Pitia Mathayo 22:1-14 na usome Mathayo 22:8-11. (Yesu alielezea mithali (mfano) hii ili kuelezea mustakabali tunaojifunza kwenye kitabu cha Ufunuo. Mfano huu unabainisha wazi kile kinachoendelea. Watumishi waliwakusanya watu (wema na wabaya) ambao hawakujua kuwa walikuwa wanakwenda harusini. Walikuwa wamevaa mavazi yao kwa ajili ya shughuli nyinginezo. Walichokifanya ni kuitikia mwaliko wa kwenda harusini na kukubali kwa kupokea vazi walilopewa na mfalme. “Matendo” yao yalikuwa ni kukubali mwaliko na vazi.)
-
-
-
- Soma Mwanzo 7:6-7. Wanawe Nuhu na wake wao waliepukaje hukumu kuu ya Mungu? (Waliingia kupitia mlangoni mwa safina. Walikubali mwaliko.)
-
-
-
- Kwa wale mnaoongea kwa chinichini kwamba “si rahisi kiasi hicho,” tafakari kile kilichotokea kabla ya gharika. Tafakari kile ambacho tumekuwa tukijifunza kabla ya Ufunuo 19. Je, huu ni uamuzi wa ghafla? (Mwizi msalabani (Luka 23:40-43) anaonesha kwamba unaweza kuwa uamuzi wa mara moja. Lakini, linalowezekana zaidi ni kwamba unatumia miaka mingi kuzikubali au kuzikataa amri za Mungu. Nadhani watu wengi wanaishi kwenye mwelekeo wa kumpokea Yesu au kumkataa. Mwelekeo huu unaakisiwa kwa jinsi tunavyoishi. Wokovu haupatikani kwa kuufanyia kazi, lakini kwa ujumla tunaishi maisha yanayoendana na kumpokea Yesu.)
-
- Yesu Mpambanaji
-
- Soma Ufunuo 19:11-15. Unaipenda taswira hii? Binafsi ninaipenda! Hii inatuambia nini juu ya Yesu Mpambanaji? (Anatoa hukumu kwa watu wabaya. Mara hii atakapokuja, mambo yako tofauti sana.)
-
-
- Tulijadili nini hapo awali kuhusu “upanga wa mdomo” wa Yesu? (Kama jinsi ambavyo Yesu alitamka na ulimwengu ukawepo, vivyo hivyo ananena na maadui wake na wanashindwa.)
-
-
-
-
- Nini kinampa Yesu mamlaka ya kuenenda hivi? (Vazi lake limechovya kwenye damu. Aliishi na kufa maisha makamilifu. Alimpatia kila mwanadamu fursa ya kupata manufaa ya kafara yake kubwa, zawadi yake kubwa. Wanadamu wanaipiga teke zawadi hiyo kwa kujihatarisha.)
-
-
-
- Soma Ufunuo 19:17-18. Nilipokuwa katika makuzi yangu tulikuwa na msemo: “Hilo ni kwa ajili ya ndege.” Ilimaanisha kuwa hakikuwa kitu kizuri sana. Je, tunaona “karamu ya Mungu iliyo kuu” iliyo “kwa ajili ya ndege?”
-
-
- Unadhani kwa nini Yohana anajumuisha taarifa hii kuhusu ndege? (Utaona kwamba “watu wote,” wale ambao wana mafanikio makubwa maishani, na wale wasio na mafanikio, wote wanashushwa na kuwa chakula cha ndege ikiwa wanaukataa wokovu.)
-
-
- Soma Ufunuo 19:19-21. Elezea hatma (mwisho) ya mnyama na nabii wa uongo tofauti na waliosalia waliomkataa Yesu? (Hii inaashiria kwamba angalao hadi kufikia hapa waovu wanaliwa, hawatupwi jahannamu.)
-
- Soma Ufunuo 20:1-3. Nini kinamtokea Shetani? (Anafungwa “kuzimu” kwa miaka elfu.)
- Milenia
-
- Soma Ufunuo 20:4 na Mathayo 19:28. Ni kundi gani hili ambalo linafufuliwa mwanzoni mwa miaka elfu, lenye “mamlaka ya kuhukumu,” na kutawala pamoja na Yesu kwa miaka elfu? (Kifungu cha nne kinaonekana kuwazungumzia wale tu “waliokatwa vichwa.”)
-
- Soma Ufunuo 20:5-6. Hii inaongezea nini juu ya kundi la kwanza ambalo ni sehemu ya “ufufuo wa kwanza?” (Hii inapanua wigo na kutuambia kwamba “mauti ya pili” haina nguvu juu yao. Hii inaonekana kama watu wa ufufuo wa kwanza ni wale wote waliookolewa.)
-
-
- Kwa kuwa ninadhani kwamba rejea ya “mauti ya pili” ni msingi wa kuelewa jambo hili, soma Ufunuo 20:14 na Ufunuo 21:8. Vifungu hivi vinakuambia nini kuhusu mauti ya pili? (Vifungu hivi vinatuambia kuwa waovu wote wanakabiliwa na “mauti ya pili” ambayo ni ya kudumu. Wenye haki, kwa upande mwingine, wanakufa mara moja tu (ikiwa watakufa). Kwa sababu hii, kundi lililopo mbinguni katika kipindi cha miaka elfu wote ni wenye haki.)
-
-
- Tayari tumesoma kwamba wenye haki “walipewa mamlaka ya kuhukumu” (Ufunuo 20:4). Hebu turuke vifungu kadhaa na tusome zaidi juu ya jambo hili. Soma Ufunuo 20:11-15. Hatma ya waovu inaamuliwaje? (Wafu wanahukumiwa “sawa sawa na matendo yao.” Kumbuka, wenye haki wapo mbinguni, na kwa dhahiri wanahusika katika kuthibitisha hukumu hii.)
-
-
- Hatma ya wenye haki inaamuliwaje? (Kama jina lako limeandikwa kwenye kitabu cha uzima, umeokolewa. Hii inaashiria kwamba waovu wanahukumiwa kwa matendo yao, bali wenye haki wanahukumiwa kwa kigezo cha endapo majina yao yapo kwenye kitabu cha uzima. Hii ni neema. Hili ni vazi la haki ya Yesu tulilopewa.)
-
- Pambano la Mwisho
-
- Soma Ufunuo 20:7-8. Watu hawa ni akina nani? Tunawezaje kuwa na pambano la pili? (Pambano lililopo kwenye Ufunuo 19 lina waovu walio hai Yesu anapokuja kuwachukua wenye haki kwenda nao mbinguni. Kisha wenye haki wanachukuliwa mbinguni na kukaa na Yesu kwa miaka elfu. Ufunuo 20:5 inatuambia kwamba ufufuo wa pili ni baada ya miaka elfu kukamilika. Waovu wanafufuliwa tena, na Shetani anawakusanya kwenye pambano la mwisho dhidi ya Yesu na watakatifu.)
-
- Soma Ufunuo 20:9-10. Ni nini matokeo ya hii vita? (Tunashinda!)
-
-
- Kifungu hiki kinazungumzia nini kuhusu moto wa jahannamu uwakao milele? (Kinatuambia kuwa waovu wote wanaofufuliwa katika ufufuo wa pili “wanateketezwa” kwa moto. Hii ni tofauti na Shetani ambaye “anateswa mchana na usiku hata milele na milele.”)
-
- Nchi Mpya
-
- Soma Ufunuo 21:1-4. Wenye haki wanakaa wapi? (Katika nchi mpya!)
-
-
- Kitu gani kinawasili katika nchi mpya kutoka mbinguni? (Yerusalemu Mpya!)
-
-
-
- Kwa nini Mungu ayaweke makao yake makuu hapa? (Hili ni tukio la kushindwa kwa uovu na ushindi wa haki. Mungu anafanya kumbukizi yetu na ya nchi yetu.)
-
-
- Soma Ufunuo 21:10-13 na Ufunuo 21:15-17. Tulijifunza jambo hili katika masomo ya nyuma. Yerusalemu Mpya inaonekanaje kwa kuzingatia vitu tunavyovifahamu sasa hivi? (Ni mchemraba mkubwa sana! Hauonekani kama taswira ya Yerusalemu Mpya ninaouona ukipakwa rangi. Taswira hizo zinaonekana kama aina fulani hivi ya mji wa kifalme. Badala yake, Yerusalemu Mpya inaonekana kama jengo lenye miliki kubwa. Inatoa maana mpya kwa Yohana 14:2: “Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi.”)
-
-
- Hili jengo la miliki kubwa lina ukubwa kiasi gani? (Lina urefu, upana na kimo cha maili 1,200 (kilomita 2,200). Popote pale unapoishi, tumia vipimo hivyo kwenye miji unayoifahamu. Nchini Marekani, jengo hili linaweza kuanzia Washington, D.C. hadi karibia na Denver, Colorado! Mji huo utafika hadi pale ambapo kwa sasa panajulikana kama anga la mbali! Kwa hesabu yangu ni kwamba nyumba yako (fleti, chumba) itakuwa kubwa. Sio futi za mraba, bali eka za mraba.)
-
-
- Rafiki, nataka kuwepo mahali pale! Nataka anwani yangu iwe “Yerusalemu Mpya, Nchi Mpya.” Ikiwa nawe pia unalitaka hilo, tubu dhambi zako sasa hivi, mpokee Yesu kama Bwana na Mwokozi wako, na ulipokee vazi lake la haki. Utakapofika mahali pale, nitafute!
- Juma lijalo tutaanza mfululizo mpya unaoitwa “Majira ya Familia.”