Midundo ya Maisha

(Mwanzo 1, Zaburi 71, Ayubu 1, Matendo 9)
Swahili
Year: 
2019
Quarter: 
2
Lesson Number: 
1

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Majira ya mwaka ni mambo ambayo nimekuwa nikijaribu kuyaepuka! Nilipokuwa mdogo niliishi Michigan. Pale Michigan tulikuwa na majira manne ya mwaka. Mapema kadri ilivyowezekana, nilihamia upande wa kusini ambapo kwa kiasi kikubwa tuliyaruka majira ya baridi.  Ninapoelekea uzeeni, ninajiambia kuwa ninasukuma majira ya mwisho maishani mwangu. Hadi kufikia hapa kwa kiasi kikubwa mambo yanakwenda vizuri kwani majira haya yanafanya kazi! Mfululizo wetu mpya wa masomo unahusu majira ya familia. Hebu tuchimbue kile ambacho Biblia inakwenda kutufundisha kuhusu mada hiyo!

 

 1.     Kuelekea Kwenye Utaratibu

 

  1.     Soma Mwanzo 1:1. Kwa nini Mungu anaanza ujumbe wake kwa wanadamu kwa namna hii?

 

   1.     Hii inazungumzia nini kuhusu mbingu na nchi? (Zilikuwa na mwanzo, Mungu alikuwepo tangu mwanzo, na aliziumba.)

 

   1.     Hii inazungumzia nini kumhusu Mungu? (Kwamba yeye ni mkubwa (mkuu) zaidi kuliko mbingu na nchi kwa sababu aliziumba.)

 

  1.     Soma Waebrania 11:3 na Zaburi 33:9. Mungu aliuumbaje ulimwengu? (Kwa kutamka!)

 

   1.     Nilipokuwa mdogo, walinifundisha jinsi ya kuandika jina langu kwa kutumia kalamu ya risasi (penseli) na karatasi. Nilipokuwa sekondari, walinifundisha jinsi ninavyoweza kuumba herufi hizo hizo kwa kubonyeza kitufe kwenye mashine ya kupiga chapa (typewriter). Maboresho makubwa! Mara ya kwanza nilipoanza mazoezi ya masuala ya sheria nilikuwa ninasoma kwa sauti kile nilichotaka kukiandika na mtu mwingine alikichapisha. Mchupo mwingine mkubwa! Mwanzoni kabisa baada ya kompyuta kuvumbuliwa nilianza kutumia imla kwa njia ya sauti. Hiyo ilikuwa bora zaidi pale ilipofanya kazi vizuri. Je, amri ya sauti kwa ajili ya uumbaji inatuambia nini kumhusu Mungu tunapoilinganisha na jinsi tunavyoumba vitu?

 

   1.     Nyumba za uumbaji zilikuaje? (Hazikuwepo. Kifungu cha Biblia kwenye kitabu cha Waebrania kinatuambia kuwa Mungu aliumba “vitu vinavyoonekana” kutokana na “vitu visivyoonekana.” Wanadamu wanatengeneza vitu vipya kutokana na vitu vilivyopo.)

 

   1.     Tunawezaje kuuelewa uwezo wa Mungu wenye kupendeza sana? (Waebrabia 11:3 – kwa imani.)

 

  1.     Soma Mwanzo 1:2. Je, hii inapaswa kuboresha fikra yetu juu ya kitu kuumbwa kutokana na kitu kisichopo? Tunalinganishaje jambo hili na Waebrania? (Tunaona kwamba kuna kitu (japo si kikubwa) kilichopo hapa. Tunaweza kuelewa jambo hili kumaanisha kuwa hapo kabla Mungu aliumba kitu kilichokuwepo, au tunaweza kuelewa “kitu kuumbwa kutokana na kitu kisichopo” kumaanisha kuwa zao la mwisho (baada ya kutengeneza kitu kutokana na kitu kisichopo) halikuwa kitu chochote kisicho na umbo, kitupu, chenye kina kirefu cha maji.)

 

   1.     Suala hili linaleta changamoto kubwa kiasi gani kwa washadadiaji wa dhana ya uibukaji? (Washadadiaji wa dhana ya uibukaji wanasukumwa sana kuelezea jinsi kitu kinavyoweza kuibuka kutokana na utupu (kutokuwepo kwa kitu). Ama mara zote “kitu” kimekuwepo, hivyo kuibua suala la jinsi kilivyotokea na kuwepo mahala hapa, au nguvu isiyo ya kawaida ipitayo maarifa yote ipo inayoweza kuumba kitu kutokana na kutokuwepo kwa kitu. Kutokana na sababu hii, washadadiaji wa dhana ya uibukaji, kwa ujumla wanaanza maelezo yao ya mianzo kwa vitu ambavyo tayari vipo.)

 

  1.     Soma Mwanzo 1:3-5. Kitu gani kinatokea kwa mujibu wa utaratibu? (Nchi inasonga kutoka kutokuwa na utaratibu hadi kuwa na utaratibu. Sio tu kwamba Mungu anatamka nuru na kuitenganisha na giza, lakini Mungu anaanzisha kipimo cha muda na kukiita jina cha kwanza kati ya vitu vingi.)

 

  1.     Soma Mwanzo 8:22. Hii inatuambia nini kuhusu mpango na utaratibu wa Mungu? (Mungu aliumba utaratibu. Anaamini katika utaratibu. Utaratibu wake ni thabiti (haubadiliki).)

 

 1.   Utaratibu wa Maisha

 

  1.     Soma Zaburi 71:6-8. Tu tegemezi kiasi gani mara tunapozaliwa? (Hili ndilo jambo baya kuhusu utoaji mimba. Watu wale wale wanaopaswa kuwalinda wasiojiweza, mama na daktari wake, wanawaua.)

 

  1.     Soma Zaburi 71:9. Ni kwa jinsi gani uzee unafananishwa na ujana? (Kwa mara nyingine, unakuwa huna ulinzi/kinga. Mtunzi wa Zaburi anamwomba Mungu amlinde.)

 

   1.     Je, ni ulinganifu wa kupendeza kwamba jamii yetu ina mvuto wa pekee katika kuwaua wazee na ambao hawajazaliwa? (Soma zaburi 71:11. Hii inaakisi ukweli kwamba watu wachoyo na waoga wanafanya hivi kwa sababu wanadhani wanaweza.)

 

  1.     Soma Zaburi 71:14-15. Mungu anatupatia nini hata pale tunapokuwa dhaifu? (Anatupatia tumaini na wokovu.)

 

  1.     Soma Mathayo 10:26-28. Uwezo wa kweli uko wapi? (Kwenye uzima wa milele. Waoga wanaweza kuwaua wadhaifu, lakini uwezo wa kweli upo kwenye karama ya uzima wa milele.)

 

  1.     Soma Mithali 4:10-13. Tunaweza kufanya nini ili kuwa na majira bora maishani? (Sura hii ya Mithali inafundisha kuwa ikiwa tutaupokea mwongozo wa wazazi wenye busara, na kuifanya busara kuwa sehemu ya maisha yetu, basi tutakingwa dhidi ya matatizo.)

 

  1.     Soma Mithali 4:7-9. Ni jambo gani jingine ambalo busara itatutendea maishani mwetu? (Sio tu kutupatia kinga, bali pia itatuinua.)

 

   1.     Hii ni busara ya namna gani? (Busara itokayo kwa Mungu.)

 

 1. Vipingamizi

 

  1.     Soma Ayubu 1:1. Je, huyu ni mtu mwenye busara? (Soma Ayubu 1:2-3. Tunaona kwamba kuzifuata njia za Mungu kulimfanya atajirike na kuwa maarufu.)

 

  1.     Soma Ayubu 1:8-12. Je, hii inakiuka kanuni za kawaida za ulimwengu? (Tunakifahamu kisa hiki chote, Ayubu anateseka vikali. Uzoefu wake unakiuka kanuni za kawaida za utii na baraka.)

 

  1.     Soma Ayubu 42:12-16. Hii inatuambia nini kuhusu kanuni za kawaida?

 

  1.     Soma Matendo 8:1-3. Je, unadhani Sauli aliamini kwamba alikuwa anayatenda mapenzi ya Mungu?

 

  1.     Soma Matendo 9:1-4. Kitu gani kinaendelea mawazoni mwa Sauli?

 

  1.     Soma Matendo 9:5-6 na Matendo 9:15-17. Maisha ya Paulo yameingiliwaje (yamevamiwaje)?

 

   1.     Je, Sauli (ambaye baadaye aliitwa Paulo), ataishia, baada ya vipingamizi, kuwa na maisha kama yale ya Ayubu? (Kauli juu ya kiwango ambacho lazima Sauli ateseke, pamoja na uelewa wetu wa maisha yake, inatuambia kuwa jibu ni “hapana.”)

 

    1.     Kwa nini hivyo?

 

  1.     Katika maisha ya Sauli na maisha ya Ayubu kuna kipingamizi kisicho cha kawaida kilicho zaidi ya uelewa wa mwanadamu. Je, vipingamizi vyote viwili vina lengo moja?

 

   1.     Je, maisha yako yamepata kipingamizi? Unadhani kipingamizi hicho ki zaidi ya uelewa wa kawaida, au ni kushindwa kwako tu kufuata kanuni za Mungu za ulimwengu?

 

 1.   Marekebisho (Ubadili)

 

  1.     Hadi kufikia hapa tumeona kwamba Mungu wetu anaweka mpango wa utaratibu. Kuna utaratibu katika dunia inayotuzunguka, na kuna utaratibu wa asili katika maisha yetu. Hata hivyo, wakati mwingine utaratibu wa maisha yetu unapata kipingamizi. Hilo linaweza kutokana na matokeo ya asili ya kushindwa kwetu kufuata kanuni za Mungu, au linaweza kutokana na nguvu isiyo ya kawaida kuingilia kati. Soma Marko 4:24-25. Ni kwa namna gani nyingine mwelekeo wa maisha yetu unaweza kubadilika? (Kipimo tunachokitumia kwa watu wengine kitatumika kwetu! Kama tu wakarimu kwa watu wengine, Mungu atakuwa mkarimu kwetu. Kama tutakuwa wanyimi kwa watu wengine, Mungu atakuwa mnyimi kwetu.)

 

  1.     Soma Marko 4:26-28. Tulipojadili juu ya Mungu kuwa mkarimu au mnyimi kwetu, je, tunazungumzia fedha pekee? Vifungu tulivyovisoma hivi punde vinaashiria nini? (Muktadha wa vifungu hivi ni kuukuza Ufalme wa Mungu. Nahisi kwamba fedha si mada ya msingi kwenye vifungu vya “ukarimu/unyimi.” Badala yake, nahisi vinahusu talanta zetu.)

 

   1.     Ni kwa jinsi gani kazi yetu ya injili inaeneza juhudi zetu mara moja? (Mungu anaibariki na kuiongeza hata kama tunalala!)

 

   1.     Miaka mingi iliyopita, nilipokuwa ninatafakari kuhusu “kustaafu,” mpango wangu ulikuwa ni kununua basi, kulibadilisha kuwa nyumba inayotembea, na kisha kusafiri kutoka kanisa moja hadi jingine nikifundisha na kuhubiri. Nilidhani kwamba ningefurahia kufanya hivyo na kitendo hicho kingewabariki wengine. Je, unaweza kubashiri kwamba kuandika somo hili kunalingana na ule mpango? (Kwa hesabu zangu ni kwamba “mpango wa basi” ungenifanya kuwafikia watu 400 kwa mwezi – kwa kuzingatia kiwango cha kati cha makanisa. Somo hili linawafikia makumi kwa maelfu ya watu kwa mwezi.)

 

    1.     Ni kazi gani ya injili unayoweza kuifanya, kazi inayoendelea wakati ukiwa umelala?

 

  1.     Rafiki, unafanya sehemu gani katika utaratibu wa Mungu? Kama huna uhakika, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, ili akuoneshe kile Mungu anachokifikiria?

 

 1.     Juma lijalo: Chaguzi Tunazozifanya.