Nafsi Tatu Katika Umoja

(Kumbukumbu la Torati 6:4, Mathayo 26:63-64, Wakolosai 2:13-15)
Swahili
Year: 
2012
Quarter: 
1
Lesson Number: 
1

Utangulizi: Nilipoanza kutumia kompyuta kwa kweli ilikuwa inanichanganya sana. Nilitaka kujua jinsi zinavyofanya kazi (kwenye sehemu zake za mashine). Mtu yeyote anaweza kuandika na kuchapa nyaraka, kama vile jinsi ambavyo mtu yeyote anavyoweza kuendesha gari. Lakini je, nini kinachotokea “chini ya zulia?” Ili kujibu swali hilo nilisoma sana vitabu na, kwa maelekezo ya mwanangu mdogo, nilitengeneza kompyuta. Sasa nimeridhika kuwa ninafahamu vitu vya msingi hata kama maarifa yangu bado siyo makubwa sana (hayajakamilika). Somo letu juma hili linafanana na hilo. Tutajifunza vitu vya msingi kumhusu Yesu na Utatu Mtakatifu, lakini maarifa kamili kuhusiana na hayo ni zaidi ya upeo/ufahamu wetu. Kwa sababu sidhani kama unaweza kuwa Mkristo bila kuwa mfuasi wa Utatu Mtakatifu, basi hebu tuzame kwenye Biblia zetu na kuona kile tunachoweza kujifunza!

  1. Fumbo/Kitendawili
    1. Soma Kumbukumbu la Torati 6:4-5 na Marko 12:28-30. Je, hii inatuambia nini kumhusu Mungu? (Kwamba “Bwana ni mmoja.”)
      1. Je, unadhani ni kwa nini Mungu anaanzisha amri ya “unipende kwa moyo wako wote” na kauli ya “Bwana ni mmoja?” (Kumpenda Mungu kwa ukamilifu ni amri chanya, na kutoipenda miungu mingine ni amri hasi.)
      2. Tafsiri Mpya ya Biblia inatuambia kuwa Kumbukumbu la Torati 6:4 ni “ombi la msingi katika dini ya Kiyahudi.” Inaitwa kuwa “Shema” kwa sababu inaanza na neno “sikiza,” neno ambalo ndilo linalomaanishwa na neno shema kwa Kiebrania. Kama hili ndilo lililokuwa ombi la msingi la dini ya Kiyahudi, je, inapaswa kumaanisha nini kwetu tunaoamini katika uvuvio wa Agano la Kale?
    2. Je, uligundua kuwa alikuwa ni Yesu ambaye aliyarudia yale maneno katika Marko 12:29 kwamba Mungu ni “mmoja?” Wayahudi na Waislamu wanasema kuwa Wakristo hawamwamini Mungu mmoja (wale wanaoamini katika Mungu mmoja) kwa sababu tumaanini kwamba Mungu Baba, Roho Mtakatifu na Yesu wote ni Mungu. Kama Wayahudi na Waislamu wapo sahihi, kwa nini Yesu avute usikivu kwa Shema na kusema kuwa amri ya upendo “ni ya muhimu kuliko zote?”
    3. Hivi karibuni, kitabu kilichouzwa kwa mauzo ya juu kabisa (ambacho pia kiliigizwa sinema) kilielezea kisa kilichoegemea kwenye wazo kwamba Kanisa Katoliki lilipindisha injili ili kuifanya ionekane kuwa Yesu alidai kuwa yeye ni Mungu, wakati ambapo kimsingi Yesu hakuwa na hayo madai. Je, injili ndizo chanzo pekee cha madai ya kwamba Yesu ni Mungu?
  2. Msingi wa Utatu Mtakatifu
    1. Soma Mwanzo 1:1-2. Mungu alipojitambulisha katika Biblia, je, alifunua nini kuhusu asili yake? (Alifunua kwamba “Mungu mmoja” alikuwa na “Roho!” Kwa hiyo, tangu mwanzo kabisa wa utangulizi wake Mungu anatujulisha kuwa yupo na anaye Roho Mtakatifu ambaye pia yupo.)
    2. Soma Mwanzo 1:26-27. Je, hili suala la “na tumfanye mtu kwa mfano wetu” ni kitu gani? Je, hii inapendekeza nini kuhusu Mungu? (Kwamba yeye ni “uwingi” wa namna fulani hivi.)
      1. Angalia tena fungu la 27. Je, hiyo inapendekeza nini kuhusu asili ya Mungu? (Kwamba inajumuisha “mwanamume na mwanamke.”)
      2. Hebu tusome Mwanzo 2:22-24. Je, ni kitu gani ambacho Mungu anakiita kuwa “mwili mmoja?” (Adamu na Hawa, na wale wote wanaooana baada ya hapo.)
    3. Je, mafungu haya kutoka katika kitabu cha Mwanzo yanatufunulia nini kuhusu mtazamo wa Mungu wa neno “mmoja?” (Kwamba ana mtazamo mpana wa neno “mmoja!” Adamu na Hawa walikuwa na haiba yao wenyewe, lakini Mungu aliwaita “mwili mmoja.” Tangu mwanzo kabisa, Mungu anafunuliwa kuwa na Roho “anayetulia juu ya uso wa maji.” Unaweza kusema kuwa Mungu ni Roho tu, lakini hiyo haiendani sana na kauli iliyofuatia ya “na tumfanye mtu kwa mfano wetu.” Tunaweza kuona kuwa Msingi wa Utatu Mtakatifu haukuanzia kwenye injili, badala yake ulianzia katika kitabu cha Mwanzo.)
    4. Soma Waamuzi 3:9-10 na Waamuzi 6:34. Je, hii inakukumbusha juu ya kile unachokiona mara kwa mara katika Agano Jipya? (Ndiyo. Agano Jipya linaendeleza wazo la Roho wa Mungu kuwa kitu kilicho tofauti na Yesu na Mungu Baba. Tunaona kitu cha aina hiyo hiyo katika Waamuzi.)
  3. Madai ya Yesu ya Uungu/Umungu
    1. Kwenye utangulizi, nilisema kuwa mtu sio Mkristo kama haamini katika Utatu Mtakatifu. Je, hiyo ni kauli isiyokuwa ya haki? Hebu tusome Yohana 8:58. Je, madai ya Yesu ni yapi hapa?
    2. Soma Yohana 6:35-40 na Yohana 6:51. Je, madai ya Yesu ni yapi hapa?
    3. Soma Yohana 8:12. Je, madai ya Yesu ni yapi hapa?
    4. Soma Yohana 11:25-27. Je, madai ya Yesu ni yapi hapa?
    5. Soma Yohana 10:30. Je, madai ya Yesu ni yapi hapa?
    6. Soma Yohana 10:32-33 na Luka 5:21-24. Je, wasikilizaji wa Yesu walielewa kuwa madai ya Yesu yalikuwa yapi?
    7. Soma Marko 14:61-62. Je, Yesu analeta madai gani hapa?
    8. Soma Mathayo 3:16-17. Je, hii inatufundisha nini kuhusu Utatu Mtakatifu?
    9. Soma Yohana 1:1-4 na Yohana 1:14. Je, hii inatufundisha nini kumhusu Yesu?
  4. Kwa Nini Inajalisha
    1. Kwenye haya mafungu uliyoyasoma hivi punde Yesu kwa wazi kabisa anaudai Uungu. Anajiita mwenyewe kuwa “MIMI NIKO AMBAYE NIKO!” Hivi ndivyo ambavyo Yehova anavyojielezea (Kutoka 3:13-14). Kama Yesu sio Mungu, je, hii inasema nini kumhusu yeye? (Kwamba yeye ni mwongo au mlaghai. Yeye sio wa kuaminiwa, achilia mbali kuabudiwa.)
      1. Soma Zaburi 73:7-9 na Yeremia 23:34. Je, mafungu haya ya Agano la Kale yanatuambia nini kuhusu madai ya uongo? (Yanatoka kwa mwovu.)
    2. Soma Mathayo 26:63-64. Upeo wote wa Agano la Kale ni kuhusu kafara ya mwanakondoo kwa ajili ya dhambi ya wanadamu. Watu wa Mungu walimtarajia Masihi aje na kuwakomboa. Je, Kuhani Mkuu anamuuliza Yesu kama yeye ni Masihi? (Ndiyo. Yesu anadai kuwa yeye ni Masihi – Masihi aliyeahidiwa ambaye anatoka kwa Mungu, atarejea kwa Mungu na atakuja tena kuwakomboa watu wake.)
    3. Soma Yohana 8:23-30. Je, Yesu anafundisha kitu gani ambacho ni suala nyeti linapokuja suala la uungu wake? (Tutakufa dhambini mwetu! Yesu anatuambia kwa dhahiri kabisa kwamba kama tusipomkubali yeye kama Masihi, Kristo, Mwana wa Mungu, basi hatuna Masihi, hatuna Mwanakondoo wa Mungu, na tutakufa kwa ajili ya dhambi zetu! Suala linaweza lisiwe tete zaidi au la msingi zaidi kwenye tumaini letu kama Wakristo!)
  5. Kwa Nini Paulo Anadhani Kuwa ni Muhimu
    1. Kumbuka kitabu maarufu na sinema iliyohoji ujinga wa Biblia kwamba Yesu hakufikiri kuwa alikuwa na uungu – kwamba hili ni jambo ambalo lilibuniwa baadaye na Kanisa Katoliki ili kuunga mkono umuhimu wake? Tumeona kwamba msingi wa Utatu Mtakatifu unapatikana katika kitabu cha Mwanzo, na tumeona kuwa Yesu alidai kuwa yeye ni Mungu na Masihi. Hebu tuangalie kile ambacho Paulo aliandika kumhusu Yesu na uungu wake. Soma Wakolosai 2:9-10. Je, Paulo ansema nini kuhusiana na Uungu wa Yesu?
    2. Soma Wakolosai 2:13-15. Je, Paulo anasema nini kumhusu Yesu kama Masihi azichukuaye dhambi zetu? (Hivyo ndivyo ambavyo Paulo anavyomwelezea Yesu.)
  6. Kwa Nini Petro Anadhani Kuwa ni Muhimu
    1. Soma Matendo 1:1-5. Je, maelekezo ya Yesu kwa wafuasi wake kwa ajili ya siku zijazo ni yapi?
    2. Soma Matendo 2:1-4. Je, hiki ndicho alichokiahidi Yesu?
    3. Soma Matendo 2:29-36. Je, Petro anasema nini kumhusu Yesu?
      1. Je, Petro anadai kuwa ni nani aliye chanzo cha kauli yake? (Roho Mtakatifu.)
    4. Rafiki, kitabu cha Mwanzo kinaweka msingi wa Utatu Mtakatifu. Yesu anadai kuwa Masihi na “MIMI NIKO AMBAYE NIKO.” Petro na paulo wanadai kuwa Yesu ni Masihi – na Petro ansema kuwa kauli hii inatokana na uvuvio wa Roho Mtakatifu. Agano Jipya, kwa ujumla wake, linatoa hoja yake kuwa Yesu ni Mungu. Agano la Kale linamtaja Yesu kama Masihi. Hili sio suala la kughushi/kubuni la viongozi wa awali wa kanisa kutaka kujiongezea umaarufu/umuhimu wao. Huu ni ujumbe wa msingi wa Biblia. Kama hatukiri/hatukubali kuwa Yesu ni Mungu na kwamba alikufa badala yetu kwa ajili ya dhambi zetu, basi tumepotea. Je, utakubali hivi leo kwamba Yesu ni Bwana wetu na Mungu wetu?
  7. Juma lijalo: Hapo Mwanzo.