Patakatifu pa Mbinguni

(Ufunuo 4 & 5, Waebrania 8)
Swahili
Year: 
2013
Quarter: 
4
Lesson Number: 
1

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Chukulia kwamba unao uwezo wa kubuni nyumba yako na kazi yako kwa namna yoyote unayoitaka. Je, utazibunije? Bila shaka ubunifu wa nyumba yako, na aina ya kazi umbayo utaifanya vitaakisi vipaumbele vyako maishani. Kama nikikuuliza, “Je, ni muhimu kiasi gani kufahamu kuhusu patakatifu pa mbinguni,” je, utajibuje? Wengine wanahoji kwamba patakatifu pa mbinguni ni kizuizi na ni suala la kitaalam lisilo na umuhimu wowote katika wokovu wetu. Lakini, hebu fikiria kidogo tu kwamba patakatifu pa mbinguni ni makao ya Mungu na kwamba makao hayo yanaakisi kile Mungu anachokifanya. Lazima makao hayo yaakisi vipaumbele vya Mungu! Kwa taarifa yako tu ni kwamba, wewe ndio kipaumbele cha Mungu! Hebu tuzame kwenye mfululizo wetu mpya wa masomo yanayohusu patakatifu pa mbinguni na kile inachomaanisha kwetu!

  1. Kwenda Kwenye Kiti cha Enzi kwa Kupitia Mlangoni
    1. Soma Ufunuo 4:1. Je, tukio hili linakukumbusha mchezo wa sinema? Unajikuta upo mahali maalum kabisa pasipojulikana, mbele yako kuna mlango ulio wazi, na sauti kutoka kwenye kitu kisichoonekana inakuambia, “Njoo!”
      1. Je, sauti hii ni laini? (Fungu linasema kuwa sauti hiyo ilikuwa kama ya “baragumu.”)
      2. Je, mlango ulio wazi unaashiria nini? (Mwaliko wa kuingia.)
      3. Je, kitu gani kinachofurahisha juu ya huu mwaliko? (Sio tu kwamba unavutia udadisi wako kutaka kufahamu kile kilicho nyuma ya mlango, bali mwaliko huo unakuambia kuwa endapo utaingia, utajifunza kuhusu mambo yajayo. Hebu twende!)
    2. Soma Ufunuo 4:2. Je, inamaanisha nini kuwa “katika Roho,” na hilo linahusikaje na suala la kuingia kupitia mlangoni? (Yohana, mwandishi wa Ufunuo, anatuambia kuwa huu si mchezo wa sinema, Roho wa Mungu anayaelekeza mawazo yake. Anathibitisha kwamba kuingia kupitia mlangoni ni sehemu ya maono kutoka kwa Mungu.)
      1. Je, Yohana anaona nini katika upande mwingine wa mlango? (Kiti cha enzi - na kimekaliwa.)
  2. Mungu Katika Kiti Chake cha Enzi
    1. Soma Ufunuo 4:3. Yohana anasema “mtu” amekaa kwenye kiti cha enzi, na kisha anaelezea jinsi huyu “mtu” anavyofanana. Je, ni nani ambaye anaweza kuwa amekaa kwenye kiti cha enzi cha mbinguni? (Mungu!)
      1. Kwa nini Yohana hasemi hivyo tu?
      2. Kwa nini Yohana anasema kwamba Mungu anafanana na miamba? (Utabaini kwamba Yohana anasema kuwa “alionekana mithili ya.” Hii haimaanishi kuwa Mungu anafanana na miamba.)
        1. Tunajifunza nini Yohana anaposema “upinde wa mvua” mithili ya “zumaridi?” (Dhana ya Yohana ni kwamba mawe haya “yanang’aa.” Yana ung’avu utokao kwenye mawe hayo. Mungu ana uzuri na utukufu ung’aao kutoka kwake.)
    2. Soma Ufunuo 4:4. Viti vingine ishirini na vinne vimekizunguka kiti cha enzi cha Mungu. Je, watu gani wamevikalia viti hivyo? (Wasaidizi wa Mungu. Washauri wa Mungu. Wazee ishirini na wanne.)
      1. Tofauti na mbingu, na kiti cha enzi cha Mungu, je, ni mahala gani hapa anapopaona Yohana? (Panaonekana kuwa makao makuu ya ulimwengu.)
      2. Linganisha maelezo kuwahusu wazee na maelezo kumhusu Mungu? (Yanaonekana kuwa ya “kawaida” kwetu, mavazi meupe, mataji ya dhahabu, na vichwa. Wanatambulishwa kama wazee – kitu tunachoweza kukitambua!)
    3. Soma Ufunuo 4:5. Fikiria maelezo haya. Kiti cha enzi cha Mungu kinaunguruma, kinatoa ngurumo na kina kinatoa umeme. Je, hii inaashiria nini? (Kiti cha enzi cha Mungu ni chanzo cha nishati (nguvu). Kama kiti hiki kingekuwa hapa duniani, ningeogopa sana kukikaribia kwa kuogopa kuuawa na hiyo (nguvu) nishati.)
      1. Hapa utabaini kwamba Roho wa Mungu anaelezewa kama taa iwakayo. Neno hili hili ndilo linatumika katika Ufunuo 8:10 kuelezea nyota iangukayo. Je, hii inaashiria nini? (Kwa mara nyingine inaashiria uwezo – uwezo ulio ndani ya Roho Mtakatifu.)
      2. Soma Matendo 2:3-4. Je, moto uliotokea, Roho wa Mungu aliposhuka na kuja duniani, unakushangaza? (Hapana. Roho Mtakatifu anao uwezo, kama nyota iangukayo kutoka mbinguni, inayowaka kama taa!)
    4. Soma Ufunuo 4:6. Je, Mungu anaweza kutazama vizuri kutokea kwenye kiti chake cha enzi? (Bahari ya kioo! Ndio maana ninapenda sana kuangalia maji ya bahari.)
    5. Soma Ufunuo 4:7-8. Je, tunaambiwa nini kuhusu utambulisho wa mtu ambaye anakaa kwenye kiti cha enzi mbinguni? (Viumbe wanne wanamtambulisha huyo mtu kuwa ni Mungu. Inaleta mantiki kwamba Yohana anasita kumtambulisha Mungu. Badala yake, anatumia utambulisho wa wale wanaoishi katika uwepo wa Mungu.)
  3. . Ibada Katika Chumba Chenye Kiti cha Enzi
    1. Soma Ufunuo 4:9-11. Je, ni sababu gani mahsusi ambayo hawa viumbe hai pamoja na wazee ishirini na wanne wanaitoa ya kumsifu Mungu? (Mungu anastahili kwa sababu alituumba na anatutunza.)
      1. Je, nadharia ya uibukaji inaathirije huu msingi wa kumpa Mungu utukufu?
      2. Soma Ufunuo 14:6-7. Je, msingi wa “injili ya milele” ni upi? (Ni madai ya Mungu kuwa Muumba wetu. Kuna mambo ambayo ni ya msingi sana, na mojawapo ni la kumpa Mungu utukufu kama Muumba wetu. Hili ndilo jambo la msingi – ambalo bila shaka ndio sababu Shetani anashambulia suala hili.)
    2. Soma Ufunuo 5:1-4. Hii ni mbingu! Tunawezaje kuwakosa watu wanaostahili? Nilidhani kwamba kila aliye mbinguni anastahili!
    3. Soma Isaya 11:1 & 10 na Ufunuo 5:5-6. Je, ni nani huyu? (Yesu!)
    4. Soma Ufunuo 5:7-9. Sasa tunapata taswira kamili kuhusu ustahili. Kwa nini Yesu anastahili na wala si mtu mwingine yeyote yule? (Kwa sababu Yesu alichinjwa kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa sababu “alitununua” kutoka kwa Shetani na kutoka kwenye kifo.)
    5. Hebu turudi nyuma kidogo. Soma tena Ufunuo 4:6 na Ufunuo 5:6. Je, Yesu yuko wapi? (Amesimama kwenye kiti cha enzi cha Mungu.)
      1. Je, hii inamaanisha nini? (Hii inamtambulisha Yesu kwa Mungu. Huu ni ushahidi zaidi wa Utatu Mtakatifu.)
      2. Angalia sehemu ya mwisho ya kitabu cha Ufunuo 5:6. Je, hii inaashiria nini kuhusu Utatu Mtakatifu na Roho Mtakatifu? (Inamuunganisha Roho Mtakatifu na Yesu.)
        1. Je, unafikiria nini kuhusu pembe saba, macho saba na Roho saba? (Soma 1 Samweli 2:10 na Zekaria 4:1. Saba ni namba kamili na yenye utimilifu. Pembe ni ishara ya uwezo wa kifalme, macho yanaashiria uwezo wa kuona au maarifa. Kwa hiyo, Yesu ana uwezo kamili na timilifu, maarifa kamili na timilifu na uhusiano kamili na timilifu pamoja na Roho Mtakatifu.)
    6. Soma Ufunuo 5:11-12 kisha usome tena Ufunuo 4:11. Je, ni mambo gani mawili yanayojenga msingi wa sisi kumwabudu Mungu? (Yeye ni Muumba wetu na Mkombozi wetu. Kiti cha enzi cha Mungu, utukufu wa Mungu, unafungamanishwa na hizo imani mbili.)
      1. Je, Sabato inaendanaje na hili wazo? (Sabato ni ukumbusho wa Uumbaji (Mwanzo 2:2-3), na Yesu alipumzika msalabani siku ya Sabato (Mathayo 28:1-6). Kwa hiyo, Sabato inaakisi msingi wa ibada katika kiti cha enzi cha Mungu!)
  4. Kazi ya Patakatifu
    1. Soma Waebrania 8:1-2. Je, ni nani huyu aliye katikati ya kiti cha enzi? (Jesu yupo hapo akiwa pamoja na Mungu Baba.)
      1. Je, Yesu anafanya nini hapo? (Anahudumu kama Kuhani Mkuu.)
    2. Soma Waebrania 8:3-5. Utakumbuka kwamba katika Ufunuo 5:6 Yesu yupo kwenye chumba chenye kiti cha enzi cha mbinguni akionekana kama mwanakondoo aliyechinjwa. Unadhani ni kwa nini Yesu anaonekana kama mwanakondoo aliyechinjwa kwenye chumba chenye kiti cha enzi cha mbinguni? (Patakatifu pa duniani palihusisha kafara ya kondoo. Mafungu yaliyomo kwenye kitabu cha Waebrania yanatuonyesha kuwa patakatifu pa duniani ni pa msingi kutufundisha juu ya patakatifu pa mbinguni. Panaakisi kile kinachoendelea mbinguni.)
    3. Soma Waebrania 8:6. Kitu gani kinaendelea mbinguni?(Yesu anahudumu kama Kuhani Mkuu!)
    4. Utakumbuka kwamba tulianza somo letu kwa kufikiria namna ambavyo tutabuni nyumba zetu au kazi yetu kama tungekuwa na uwezo huo. Je, makao ya Mungu na kazi ya Mungu vinaakisi nini? (Kazi yake mbinguni ni kuhudumu kwa niaba yetu! Kwa kuwa tumesoma kwamba patakatifu pa duniani ni sampuli ya patakatifu pa mbinguni, hata ubunifu wa makao ya Mungu unaakisi kisa cha ukombozi! Juma lijalo tutajifunza patakatifu pa duniani ili tuone jambo jingine tunaloweza kujifunza.)
    5. Rafiki, madai ya Mungu kutaka kuabudiwa yanaibuka kutokana na yeye kuwa Muumba na Mkombozi wetu. Kwa sababu wewe ndiye uliye vipaumbele vya Mungu, je, unafanya yote yaliyo ndani ya uwezo wako kusimama upande wa Mungu katika haya masuala?
  5. Juma lijalo: “Mbinguni” Duniani.