Siku ya Upatanisho Wakati wa Hukumu ya Mwisho

(Danieli 8-9)
Swahili
Year: 
2013
Quarter: 
4
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kama unakuna kichwa chako kujua maana ya neno “Eschatological,” neno hili linamaanisha “matukio ya siku za mwisho.” Kama tulivyojifunza, Siku ya Upatanisho ilikuwa inarejea siku moja katika kila mwaka ambayo dhambi zote zilihamishwa kutoka kwa watu wa Mungu kwenda patakatifu na hatimaye zilihamishiwa kwa mbuzi. Kisha mbuzi alipelekwa jangwani ambako alifia huko. Siku ya Upatanisho iliwakilisha badiliko la moja kwa moja la dhambi zilizotendwa na watu katika kipindi cha mwaka mzima. Kwa hiyo unauliza kuwa, “Kitu gani hicho kinachoweza kuwa cha muhimu sana juu ya badiliko la moja kwa moja la dhambi katika siku za mwisho?” “Siku za mwisho” zinatukumbusha hukumu ya mwisho. Je, unataka dhambi zako zisogezwe mbele au unataka kuwa kama yule mbuzi? Danieli alipoomba juu ya tatizo la dhambi la watu wa Mungu, Mungu alimpa ujumbe maalum juu ya mpango wake mkuu wa kukabiliana na dhambi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

  1. Shauku ya Danieli
    1. Soma Danieli 9:1-3. Jambo gani lililomo mawazoni mwa Danieli? (Unabii wa Biblia ulifunua kwamba wakati wa mabadiliko ulikuwa umefika. Mabadiliko haya yataruhusu Yerusalemu iweze kujengwa upya.)
    2. Soma Danieli 9:4-6. Je, Danieli anaanzaje ombi lake? (Kwa kutoa sifa! Hivi ndivyo ambavyo kila ombi linapaswa kuanza. Angalia Luka 11:1-2.)
      1. Je, mada kuu ya ombi ni ipi? (Ungamo la dhambi. Watu wana tatizo la dhambi.)
    3. Soma Danieli 9:11-14 na Danieli 9:17-19. Unadhani kwa nini kimahsusi kabisa Danieli anapabainisha patakatifu? (Chukulia jambo hili katika mtazamo wa Danieli. Watu wake wametenda dhambi. Mungu ametoa hukumu juu yao kwa njia ya utumwa na kuharibiwa kwa Yerusalemu na patakatifu. Patakatifu ni sehemu ya kuhamisha dhambi na hapana kazi tena. Danieli pamoja na watu wamejaa dhambi!)
    4. Hebu tuangalie suala la hukumu. Je, Danieli anajihusisha na hukumu ya aina gani? (Hali aliyokuwanayo Danieli inayaakisi maisha yetu. Kutoitii sheria ya Mungu huleta utekelezaji wa hukumu kivitendo katika kipindi tulichopo. Mara kwa mara huwa tunateseka kutokana na dhambi zetu. Lakini, suala kuu linahusu hukumu inayotokana na kutokuwa na uwezo wa kupokea msamaha wa dhambi. Kutokuwa na uwezo wa kuhamisha dhambi kutoka kwa watu kwa njia ya mfumo wa patakatifu.)
    5. Kwa kuwa sasa tunafahamu kilichokuwa kikiendelea mawazoni mwa Danieli, hebu sasa tuyageukie maono aliyopewa.
  2. Ujumbe
    1. Soma Danieli 8:1-4. Ungefikiria juu ya jambo gani endapo ungekuwa katika matembezi ya asubuhi nawe ukaona jambo hili? (Ningeogopa, hadi pale ambapo nigetambua kwamba yalikuwa ni maono.)
      1. Kwa kuwa haya ni maono, unadhani Mungu anampa Danieli ujumbe gani? (Juma lililopita tulijifunza kuwa Danieli aliona wanyama wa kutisha waliowakilisha falme ambazo zingeibuka siku zijazo. Hili linaonekana kuwa hivyo.)
    2. Soma Danieli 8:15-20. Kondoo anamaanisha nini? (Danieli anaambiwa na mjumbe kutoka mbinguni kwamba huu ni ufalme wa Umedi na Uajemi. Hii inaendana na ujumbe tuliojifunza juma lililopita!)
    3. Soma Danieli 8:5-8 na Danieli 8:21-22. Je, mbuzi anawakilisha nini? (Nguvu ya ufalme wa Uyunani. Kama ilivyokuwa katika maono yaliyotangulia, hapa Danieli anaoneshwa juu ya siku zijazo.)
    4. Soma Danieli 8:9-12. Tulipoangalia pembe zilizobainishwa katika Danieli 7, ziliwakilisha mamlaka ya hapa duniani. Je, mamlaka gani ya kidunia inaweza “kulifikilia jeshi la mbinguni?” Je, mamlaka gani ya kidunia inaweza kuangusha baadhi ya majeshi ya mbinguni?
      1. Soma Ufunuo 12:7-9. Je, hii inaashiria kuwa pembe hii ni nani? (Shetani! Kumbuka kwamba jambo hili ni la kiishara. Bila kujalisha maana ya hii pembe, katika hali ya kawaida kabisa pembe hii inawakilisha kazi ya Shetani.)
    5. Angalia tena Danieli 8:11-12. Fikiria ombi la Danieli. Kwa nini Mungu aliamua kumpatia Danieli “historia” ya masomo yanayojirudia kuhusu siku zijazo? (Mungu anamwambia Danieli kwamba Yeye (Mungu) anashughulika hata katika matukio yanayotisha.)
      1. Danieli aliposikia rejea ya patakatifu, unadhani jambo gani lilimjia mawazoni mwake mara moja? (Hiki ndicho ambacho Danieli alikuwa akikiombea! Hekalu la Mungu, patakatifu pa Mungu pa duniani palikuwa pameangamizwa na Watu wa Babeli. Lazima tafakari ya jambo hili ilikuwa inafadhaisha.)
    6. Soma Danieli 8:13-14. Je, Danieli anapewa matumaini gani? (Anapewa matumaini kwamba patakatifu, mfumo wa kukabiliana na dhambi, vitarejeshwa!)
    7. Soma Danieli 8:23-25. Hii inatoa taswira nyingine juu ya hii pembe. Je, inamaanisha nini kwamba atakuwa mwenye nguvu, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe?
      1. Je, inamaanisha nini kwamba ataangamizwa, lakini si kwa uwezo wa mwanadamu? (Marejeo yote mawili yanatuambia kwamba hii ni vita ya kiroho. Hii ni vita kati ya Shetani na Mungu.)
      2. Je, unaona umuhimu gani katika jambo hili? (Kama ilivyo kwa Danieli, ulimwengu wetu unaweza kuonekana kutokudhibitika. Huenda tunahisi kwamba tunapata mateso ya hukumu kutokana na dhambi za zamani. Ujumbe wa Mungu kwa Danieli ni kwamba “nimeshashughulikia jambo hili.”)
    8. Soma Danieli 8:26-27. Je, Danieli aliupokeaje huu ujumbe? Je, alifurahia kutambua kwamba Mungu ndiye alikuwa mdhibiti? (Hapana. Alikuwa anaumwa. Hakuelewa. Huenda sehemu ya tatizo ilikuwa ni kwamba maono yalionekana kuashiria kwamba Mungu hatashughulikia jambo hili hadi mwisho wa wakati.)
  3. Ushindi
    1. Hebu tusome tena Danieli 9:1-3. Sasa tuna taarifa za kina zaidi. Maono aliyopewa Danieli yamenza kutimizwa. Babeli imeanguka, na Umedi na Uajemi zimeinuka na kuwa na nguvu. Je, Danieli anataka nini? (Anataka jambo lile lile ambalo amekuwa akilitaka siku zote – kwamba taifa lake na patakatifu pake vitarejeshwa. Anafahamu kwamba unabii juu ya kipindi cha urejeshwaji umekaribia.)
    2. Soma Danieli 9:20-23. Je, hii inatufundisha nini juu ya maombi na Mungu wetu? (Mungu ni msikivu. Anajali.)
      1. Je, mbingu ipo karibu kwa kiasi gani? (Gabrieli aliondoka maombi yalipoanza.)
      2. Kwa nini Gabrieli ametumwa? (Ili kumpatia Danieli “utambuzi na uelewa.”)
      3. Uelewa juu ya nini? (Mfululizo wa maono. Utakumbuka kwamba katika Danieli 8:14-15, Danieli aliambiwa kwamba patakatifu pataangamizwa “nyakati za jioni na asubuhi” 2,300. Hiki ndicho kiini cha mahangaiko ya Danieli.)
    3. Soma Danieli 9:24-25. Je, habari njema juu ya Yerusalemu na patakatifu ni ipi? (Yerusalemu itajengwa upya!)
      1. Je, tunaona habari gani njema nyingine tena? (Dhambi itaishilizwa! Uovu utapatanishwa! Mtakatifu sana atatiwa mafuta. Haki ya milele italetwa!)
        1. Je, hii inaonekana kuwa kama patakatifu na Siku ya Upatanisho? (Ndiyo. Utakumbuka kwamba “patakatifu pa patakatifu” panarejea sehemu ya patakatifu palipoingiwa katika Siku ya Upatanisho.)
    4. Soma Danieli 9:26-27. Jambo hili linaonekana kuwa la kutisha, sawa? Yesu (Mtiwa Mafuta) anakatiliwa mbali! Siingii kwa kina kwenye tarakimu au kwenye mahesabu, lakini Wakristo wengi waliofanyia utafiti jambo hili kwa kina wanabaini kwamba kwa kufanyia mahesabu tarakimu hizi, unabii huu unatabiri tarehe ya Yesu kufanyika mwanadamu, kuteswa kwake na angamizo la pili la hekalu la Yerusalemu.)
      1. Wakristo wachache waliendelea na mahesabu na kuhitimisha kwamba mwaka 1844 ndio tarehe ya kuanza kwa kipindi ambacho tumekuwa tukijifunza: hukumu ya mwisho, utume wa Yesu mbinguni kwa niaba yetu, “Siku ya Upatanisho” mbinguni. Juma lililopita, tulisema kuwa mwanzo wa kipindi hiki ulikuwa ni takriban mwaka 1806, na kipindi hicho kinaendana na tarehe mahsusi ya mwaka 1844. Je, unaupa umuhimu gani mfululizo wa hizi tarehe? (Wengine wanazipa umuhimu mkubwa hizi tarehe, hususan tarehe ya kuanza kwa utume wa Yesu kwa niaba yetu katika hukumu ya mwisho. Nadhani hizi tarehe zina malengo mawili. Kwanza, zinatupatia ujasiri kwamba Mungu ndiye mtendaji mkuu na kwamba tunaweza kumtumaini. Pili, zinatufariji kwamba mpango wa wokovu haujafungwa, unasonga mbele kwa mujibu wa mpango wa Mungu.)
    5. Rafiki, unafanana na Danieli, ukijihusisha sana na jinsi maisha yanavyokwenda? Je, unajali sana dhambi iliyopo maishani mwako na kwa wale wanaokuzunguka? Mungu ana mpango na tunaishi katika awamu ya mwisho ya mpango huo. Mungu anaikomesha dhambi. Yesu anatenda kazi kwa niaba yetu ili kufunika dhambi zetu kwa damu yake. Je, utafanya uamuzi leo kustarehe kwa ujasiri anapokuwa akitenda kazi kwa niaba yako – badala ya kujikita kwenye mambo yanayokuhangaisha maishani mwako?
  4. Juma lijalo: Ujumbe Wetu wa Unabii.