Kuwafanya Watoto Kuwa Wanafunzi

(Yeremia 7, Kumbukumbu la Torati 6, Mathayo 18)
Swahili
Year: 
2014
Quarter: 
1
Lesson Number: 
4

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Tulipata wakati mgumu kuondoka hospitali tupopata mtoto wetu wa kwanza. Tulipomweka mtoto kwenye kiti cha gari mke wangu alishawishika kuwa kiti kitamwua mtoto. Nami nilishawishika kwamba endapo tusipomweka kwenye kiti cha gari basi mtoto angefariki. Hayakuwa majibizano mazuri, na nina uhakika wahudumu wa hospitali walitamani tuondoke mahali pale – kitendo ambacho hatukuweza kukifanya hadi pale tulipopata ufumbuzi wa suala hili. Hatimaye mke wangu alishinda mpambano. Tulipokuwa njiani kuelekea nyumbani, tulidhani kuwa watu wa pale hospitalini walimwandikia mwanetu kimiminika maalum ambacho tulitakiwa kukinunua, lakini hakuna duka la dawa lililokuwa likiuza kimiminika hicho. Kwa mara nyingine tulipata wasiwasi kwamba tungeweza kutenda kosa ambalo lingemdhuru mtoto wetu. Hakuna aliyetupatia kitabu chenye maelekezo kwa ajili ya masuala kama haya. Je, wewe pia ulijisikia hivyo ulipompata mwanao wa kwanza? Biblia inatupatia maelekezo ya jinsi ya kuwalea watoto. Maelekezo hayo hayahusishi viti vya gari, lakini yanaokoa uhai. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

  1. Kuwapatia Watoto Uzima
    1. Soma Yeremia 7:30. Nyumba ipi inabeba jina la Mungu? (Mungu anazungumzia hekalu lake. Katika mfululizo wa masomo yetu yaliyopita tulijifunza juu ya patakatifu hekaluni na jinsi palivyokuwa kiini cha ondoleo la dhambi. Tulijifunza kuwa patakatifu pa patakatifu ndipo mahali alipokuwepo Mungu.)
      1. Je, watu wa Mungu wamefanya nini? (Wameweka sanamu katika nyumba ya Mungu.)
    2. Soma Yeremia 7:31. Badala ya kutoa kafara ya mnyama kwa ajili ya ondoleo la dhambi, je, watu wanafanya nini? (Wanawatoa watoto wao kafara!)
      1. Je, Mungu anasema nini juu ya jambo hili? (Hata haikumwingia akilini kwamba uovu wa aina hiyo unafanyika.)
      2. Kwa nini jambo la kutisha kama hilo liliingia mawazoni mwa watu wa Mungu? (Walidhani kwamba kwa kuwatoa watoto wao kafara kwa kuwateketeza motoni, miungu ingewabariki na kuboresha maisha yao.)
        1. Kwa nini siku hizi watu wanatoa mimba? (Ni kwa sababu zile zile, isipokuwa tu mungu sio sanamu, bali ni mungu yule yule wa ubinafsi.)
    3. Soma Yeremia 7:32-34. Jambo gani litatokea kwa taifa la watu wanaowatoa watoto wao kafara kwa ajili ya ustawi wao wenyewe, watu wanaotumikia miungu badala ya kumtumikia Mungu wa kweli? (Watapoteza kila kitu walichotarajia kukipata – ikiwemo maisha yao na staha/mwenendo wao. Baadhi ya wafu wataliwa na wanyama. Huu si mwisho mzuri.)
  2. Kuwafundisha Watoto Habari Njema za Mungu
    1. Soma Kumbukumbu la Torati 6:1-3. Je, hapa Mungu anatoa jambo gani? (Jambo lile lile ambalo kundi la awali lililitafuta – maisha bora.)
      1. Je, Mungu anapendekeza njia gani ya kupita ili kuyafikia maisha bora? (Kuyafuata maagizo na amri za Mungu.)
    2. Soma Kumbukumbu la Torati 6:4-5. Je, amri ya kwanza ambayo Mungu anatupatia ni ipi? (Soma Mathayo 22:36-40. Mada yenye kufanana katika Agano la Kale na Agano Jipya ni kwamba tunatakiwa kumpenda Mungu kwanza, na tunatakiwa kuwapenda majirani wetu.)
    3. Soma Kumbukumbu la Torati 6:6 na Waebrania 8:10. Tunaona hii rejea ya sheria kuwa “katika nia zao” au kuandikwa “katika mioyo yao.” (Sheria inakuwa sehemu ya maisha yetu. Inakuwa sehemu ya mapenzi yetu na asili yetu.)
    4. Soma Kumbukumbu la Torati 6:7-9. Ni kawaida kwa Wayahudi wenye itikadi kali kuwa na “mezuzah,” chombo kidogo ambacho fungu la Biblia linapatikana, na chombo hiki kinawekwa kwenye mlango wa nyumba. Unapoyatafakari mafungu haya, unadhani yanaleta mantiki gani? Kuyagundisha mambo kichwani, mikononi na mlangoni mwako? (Labda. Lakini, mantiki ya kina juu ya jambo hili ni kuwajaza wanao neno la Mungu. Lengo ni kuyafanya mapenzi ya Mungu yakae mioyoni mwao.)
      1. Je, hili linawezekana? Je, wanao wataasi na kumchukia Mungu endapo utazungumzia habari za Mungu wakati wote?
      2. Hebu tubadili jambo hili hadi kwenye televisheni. Wajaze wanao na mambo mbalimbali ya televisheni. Zungumzia juu ya televisheni muwapo ndani ya gari, mnapotembea na mnapokuwa mkila. Weka alama za televisheni mikononi mwako na kichwani mwako. Uwe na fulana yenye picha ya televisheni. Je, unaweza kufanya hivyo? Je, unafanya hivyo?
      3. Vipi kama tukibadili suala hili hadi kwenye intaneti? Uwe na simu yako yenye kufanana na kompyuta mikononi mwako na kichwani mwako. Vaa miwani ya jua. Je, unaweza kufanya hivyo?
      4. Inaweza kuonekana kuwa haiwezekani au si rahisi kuwajaza watoto wetu sheria ya Mungu, bali kwa hakika kabisa Shetani ametimiza jambo hili kwa ujumbe wake. Watoto wangu walipokuwa bado wakiishi pamoja nasi nakumbuka jinsi nilivyohitaji kuwaelekeza ili waongoke juu ya mapenzi ya Mungu. Hiyo ilikuwa changamoto.
    5. Soma Kumbukumbu la Torati 6:20. Je, umewahi kuulizwa swali hili na wanao? Je, umewahi kuulizwa, kwa nini jambo hilo ni la muhimu? Kwa nini niwe na mashaka juu ya taratibu za Mungu? Je, hiyo inaleta utofauti gani?
    6. Soma Kumbukumbu la Torati 6:21-24. Je, jibu gani lenye kufanana unaloweza kuwapatia wanao? (Zungumzia juu ya historia yako na Mungu. Waambie jinsi ambavyo kutembea na Mungu huleta uzima na ustawi. Je, wanataka kufanikiwa maishani? Mtiini Mungu!)
      1. Kati ya fursa zilizokosekana ambazo nilizizungumzia na wanangu juu ya Mungu, eneo mojawapo nililofanikiwa lilikuwa ni kwamba tulikuwa tukisoma Biblia wakati wa jioni. Tulianza kwa kusoma Agano Jipya kisha tukasoma Agano la Kale. Nilichagua tafsiri ya Biblia iliyokuwa rahisi kusomeka na kueleweka, watoto walisoma, na tulijadiliana kile tulichokisoma. Ilikuwa inapendeza sana. Je, uko radhi kufanya hivyo?
  3. Kuwakaribisha Watoto
    1. Soma Mathayo 18:1-4. Endapo utakuwa umetumia muda wako mwingi na watoto, je, unadhani kuwa watoto ni wanyenyekevu? (Kwa kiasi kikubwa kabisa hapana! Watoto ni wabinafsi – ni kama kwa wanafunzi waliotaka kuwa wakuu.)
      1. Kama inavyoonekana, hii ni Biblia na Bwana wetu anazungumza, kwa hiyo hatuwezi kusema, “Huo ni uongo!” Je, unadhani Yesu anamaanisha nini? (Watoto hawakuwa na hadhi maishani ikilinganishwa na watu wazima. Wanafunzi walikuwa wakitafuta hadhi miongoni mwao. Yesu anatuambia kwamba hatupaswi kugombania kuwa na hadhi.)
    2. Soma Mathayo 18:5. Ni kwa jinsi gani jambo hili kimantiki linalinganishwa na mafungu tuliyoyasoma? (Unaweza kupendelea kutumia muda wako kuwa na watu watakaokupatia hadhi zaidi. Lakini, Yesu anasema kuwa kutumia muda mwingi na watoto “katika jina la [Yesu]” ni jambo lisilo na kifani na la muhimu.)
      1. Je, jambo gani la kujifunza kivitendo unaloweza kulipata kutokana na suala hili? (Kwa hakika tunatakiwa kuwakaribisha watoto kanisani. Tunatakiwa kuhakikisha kuwa programu za watoto zinaandaliwa na kupangiwa watu wa kutosha kuzisimamia.)
      2. Unadhani watoto watajisikiaje endapo watakwenda katika kipindi cha Shule ya Sabato na mwalimu asiwepo? Je, watajisikia kuwa wamekaribishwa?
    3. Soma Mathayo 18:6. Je, ushawishi wetu kwa watoto ni wa muhimu kiasi gani?
    4. Soma Mathayo 18:7. Je, umewahi kumsikia mtu akisema, “Endapo nisingeuza [kitu chenye athari mbaya kwa watoto] basi mtu mwingine angefanya hivyo?” Je, Yesu anakiri kwamba patakuwepo na mtu fulani wa kuwadhuru watoto? (Ndiyo. “Mambo kama hayo lazima yawepo.”)
      1. Je, Yesu anasema nini juu ya kisingizio “endapo nisipofanya hivyo mtu mwingine atafanya hivyo?” (Anasema kuwa hicho si kisingizio. “Ole kwa mtu yule.”)
    5. Soma Marko 10:13. Unadhani lengo la kumwomba Yesu awaguse watoto wadogo ni lipi? (Wazazi walikuwa wakitafuta mbaraka kwa watoto wao.)
      1. Unadhani kwa nini wanafunzi waliwakemea wazazi? (Huenda walidhani kwamba Yesu alikuwa na mambo ya msingi zaidi aliyopaswa kuyashughulikia.)
    6. Soma Marko 10:14. Je, Yesu alichukuliaje ukemeaji wa wanafunzi? (Alichukizwa sana. Lugha ya Kiyunani inaonesha hisia za ndani. Yesu alisikitika sana.)
      1. Je, hiyo inaonekana kuwa ni kukasirika kupita kiasi? (Hapana! Tunatakiwa kuelewa jambo hili: Yesu anaweka kipaumbele kikubwa katika kuwakaribisha watoto!)
    7. Soma Marko 10:14-16. Kumbuka kwamba katika Mathayo 18:4 Yesu alisema kwamba tunatakiwa kuwa kama watoto wadogo ili kuweza kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. Sasa Yesu anasema kuwa lazima “tuukubali” Ufalme wa Mungu “kama mtoto mdogo” la sivyo hatuwezi kuupokea kabisa? Je, hii inamaanisha nini? Je, mtoto mdogo anawezaje kuipokea injili? (Watoto wanaweza kuwa na tabia nyingi zenye dosari/upungufu, lakini sifa moja ya jumla ya watoto ni kutumaini [imani ya kawaida].)
      1. Je, maisha yako yataborekaje endapo utaonesha imani ya kawaida tu kwa Mungu?
    8. Rafiki, tunatakiwa kuwapa watoto kipaumbele nyumbani kwetu na kanisani kwetu. Tunatakiwa kufanya kila tuwezalo ili kuwaelekeza kwenye njia sahihi, na si kuwaelekeza upotevuni. Je, utajitoa kulipatia suala hili umuhimu? Pengine utazawadiwa kuwa na mtazamo wa kitoto zaidi, ule wa kuwa na imani ya kawaida!
  4. Juma lijalo: Kuwafanya Wagonjwa Kuwa Wanafunzi.