Kuwafanya Wenye Nguvu Kuwa Wanafunzi

(Warumi 13, Matendo 4, Mathayo 26)
Swahili
Year: 
2014
Quarter: 
1
Lesson Number: 
9

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, serikali ni nzuri? Mungu anatuambia kuwa serikali ni nzuri. Kama hilo ni kweli, kwa nini basi serikali inafanya uovu mwingi? Mamlaka ya serikali yalimwua Yesu! Je, Wakristo wanapaswa kuhusianaje na watu waliopo kwenye mamlaka? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!

  1. Wakristo na Serikali
    1. Soma Warumi 13:1. Je, Mungu ndiye aliyefanya Ronald Reagan achaguliwe kuwa rais? Je, Mungu ndiye aliyefanya Barack Obama achaguliwe kuwa rais? Kama umepata wakati mgumu kujibu kuwa, “ndiyo,” kwenye maswali yote mawili, je, unadhani fungu hili linamaanisha nini? (Hawa ni Marais wawili wa Marekani wenye mitazamo tofauti kuhusu wajibu wa serikali.)
      1. Sote tunaweza kufikiria mamlaka kama vile Hitler na Stalin walioua maelfu (mamilioni?) ya raia wao wenyewe. Kwa sasa Korea ya Kaskazini inawaua raia wake. Je, Mungu ndiye aliweka mamlaka hizo? (Nadhani fungu hili linamaanisha kuwa kwa ujumla Mungu huweka mamlaka za kiserikali.)
    2. Soma Warumi 13:2. Kanisa nchini Ujerumani limekuwa likilaumiwa kwa kutosimama kinyume na mauaji ya mamilioni ya Wayahudi katika kipindi cha utawala wa Hitler. Je, unalielewaje na kulitumia fungu hili?
      1. Kamwe tusingekuwa na mapinduzi ya Marekani endapo fungu hili lingefuatwa. Je, vuguvugu hilo lilikuwa kinyume na Biblia?
      2. Endapo umesema kuwa, “Mungu anaziunga mkono mamlaka zingine na hasaidii mamlaka zingine,” basi unajiingiza kwenye Warumi 13:1 inayosema kuwa Mungu huweka mamlaka zote. Je, kuna namna nyingine ya kuyaangalia haya mafungu?
    3. Soma Warumi 13:3-5. Tutaangalia mashtaka ya Yesu mwishoni mwa somo hili. Je, ni sahihi kusema kuwa “watawala hawawatishi wale wanaoenenda vyema?” Paulo alifahamu kilichomtokea Yesu. Yesu alikuwa sahihi na alikabiliana na vitisho! (Kuna mambo mawili. Kwanza, ni muktadha. Ilikuwa muhimu kwa washiriki wa kanisa wa awali kutoonekana kama maadui wa Rumi. Ujumbe huu ulisaidia katika mantiki hiyo. Pili, nadhani hapa Paulo anazungumza kwa ujumla. Tunafahamu kwamba mara zote huu sio uhalisia kutokana na kile kilichomtokea Yesu. Hata hivyo, kwa ujumla jambo hilo ni la kweli.)
      1. Je, Paulo anaandika juu ya mambo halisi pekee? (Hapana. Anasema kuwa anaandika kutokana na mambo halisi yaliyotokea (adhabu) na “pia ni kutokana na dhamiri.”)
    4. Soma Warumi 13:6-7. Je, Wakristo wanatakiwa kulipa kodi hata kama hawakubaliani na sera za serikali? (Ndiyo.)
      1. Je, Wakristo wanatakiwa kumheshimu Nancy Pelosi (au mwanasiasa [mbainishe] mwenye ubishani nchini mwako)? (Ndiyo. Miaka michache iliyopita, nilisoma mafungu haya tena na yakanishawishi kuacha kumnukuu/kumrejea mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa kwa namna isiyo ya haki.)
    5. Soma Warumi 13:8-10. Kwa nini madeni na upendo ni sehemu ya fundisho hili? Je, yanaendanaje na ulipaji wa kodi na kuepuka mapinduzi? (Yote haya yanahusika na wajibu wa Wakristo. Wana wajibu wa kulipa ankara zao, wana wajibu wa kujiepusha kumdhuru jirani yao, wana wajibu wa kuwa raia wema. Wajibu wote huu unaibuka kutokana na wajibu wa upendo.)
      1. Hebu subiri kidogo! Kama msingi ambao kanuni zote hizi nyingine zinaibuka ni kanuni ya upendo, je, hiyo inasema nini kuhusu Wayahudi waliokuwa chini ya mamlaka ya Hitler na kuishi chini ya mamlaka ya Stalin? (Endapo kanuni inayotawala ni upendo, basi Wakristo wangewatetea Wayahudi na wangepinga mauaji yaliyofanywa na Stalin.)
  2. Wanafunzi na Serikali
    1. Soma Matendo 4:1-3. Muda mfupi uliopita tumesoma Warumi 13:3 inayosema kuwa wale wanaotenda matendo mema hawana hofu na serikali. Je, hiyo ni kweli hapa? (Hapana. Perto na Yohana wanahubiri injili.)
    2. Soma Matendo 4:4. Je, hii inatufundisha nini kuhusu kama Petro na Yohana walikuwa wakitenda jambo sahihi? (Maneno yao yaliwaongoa wadhambi!)
    3. Soma Matendo 4:5-12. Warumi 13:7 inasema kuwa waheshimu na kuwatii wale wanaostahili. Hawa ni viongozi halali, je, Petro anawatii na kuwaheshimu?
      1. Je, ni heshima kusema, “Je, tulitiwa mbaroni kwa kuwa wema na kumponya kiwete?’ “Mnajidai kuwa na uwezo wa kututia mbaroni, lakini mlimwua Masihi!”
    4. Soma Matendo 4:13-14. Je, Petro amechagua mkakati wa ushindi? (Ndiyo! Wapinzani wake hawajui wajibu nini, na wanaamua kujipanga upya kwenye makundi.)
      1. Je, hii inaashiriaje uelewa wetu wa Warumi 13? (Tupo ndani ya kanuni ya upendo kuipinga serikali pale inapotupinga kuiendeleza injili.)
      2. Tunatakiwa kusimama kidogo hapa. Tunapotumia neno “kuipinga serikali,’ je, hiyo ina maana sawa kwenye demokrasia kama ilivyo kwenye serikali ya kiimla – kama Rumi? (La hasha, hapana. Mamlaka yapo mikononi mwa wapiga kura katika serikali ya kidemokrasia. Kwa hiyo, upinzani kwa mujibu wa sheria ni sehemu ya kuunga mkono utendaji halali wa serikali.)
    5. Soma Matendo 4:15-17. Watawala wanakutana kupanga mkakati. Je, lengo ni nini? (“Kuzuia jambo hili lisienee.” Kuzuia injili.)
    6. Soma Matendo 4:18-20 kisha soma Warumi 13:5. Petro na Yohana wanauliza endapo wanapaswa kumtii Mungu au wanadamu. Je, wanawezaje kuweka mazingira hayo ya utofauti ilhali Mungu anasema kuwa tuwaheshimu waliopo kwenye mamlaka? Mtawala anapotoa amri, unaifuata! (La hasha, hapana.)
    7. Soma Matendo 4:25-26. Huu ni mtazamo tofauti kwa watawala na serikali tofauti na ule tuliousoma kwenye Warumi 13:1. Mtazamo huu unabainisha kuwa serikali zinafanya njama na ghasia dhidi ya kazi ya Mungu, wakati Warumi inasema kuwa mamlaka zinawekwa na Mungu. Kipi ni kipi kati ya hii mitazamo miwili?
    8. Soma Matendo 4:27-28. Je, mafungu haya yanasema nini juu ya uwezo na mapenzi ya Mungu na matendo maovu ya watawala? (Yanasema kuwa uovu mkubwa kupita yote – mauaji na mateso ya Yesu – ni jambo ambalo Mungu alikuwa amepanga tangu zamani kuwa “linapaswa kutokea.”)
      1. Je, Mungu yu nyuma ya uovu unaofanywa na watawala kama Hitler na Stalin? (Hapana. Katika jambo hili, Mungu alifanya uamuzi kuwa atakufa kwa ajili ya dhambi zetu. Shetani na wakala wake wa kibinadamu waliamua kufanya tukio hilo liwe lenye maumivu makali.)
      2. Je, unaweza kuona mlingano kati ya mjadala wa Warumi kuhusu Mungu na mamlaka ya kidunia na mjadala huu kuhusu Mungu na kifo cha Mwanaye? (Nadhani mlingano upo. Ni mapenzi ya Mungu kuwepo kwa mamlaka duniani. Yalikuwa ni mapenzi ya Mungu, mara tulipotenda dhambi, kufa badala yetu. Ukweli kwamba Mungu anayo mapenzi ya jumla kwa jambo fulani kutendeka haimaanishi kuwa Mungu anaidhinisha uovu unaofanywa kutokana na uhuru wa mwanadamu wa kutenda mambo yake.)
  3. Soma Matendo 4:29-30. Je, wanafunzi wanamwomba Mungu awasaidie kutotii mamlaka? (Ndiyo.)
    1. Ni jambo gani basi, linalopaswa kuwa kanuni ya Wakristo kuhusu uovu unaofanywa na mamlaka? (Hatupaswi kuwa sehemu ya uovu huo. Lakini tambua kwamba tunaweza kuadhibiwa kwa kutokuwa watiifu: “yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako.” Tafadhali, Mungu, tusaidie ili tuwe na uwezo wa kuvumilia mateso kutokana na kuyatenda mapenzi yako.)
  4. Yesu na Serikali
    1. Soma Mathayo 26:59-62. Kwa wazi kabisa, hapa serikali haina lengo la kutenda jambo jema. Je, Yesu alipaswa kujibu? Je, mamlaka ya juu haimtaki Yesu atoe jibu? (Soma Kumbukumbu la Torati 19:15. Biblia inabainisha kanuni dhidi ya mtu kujiponza/kujitia hatiani mwenyewe. Huwezi kuadhibiwa kutokana na kauli yako pekee. Kwa hiyo hili halikuwa swali sahihi.)
    2. Soma Mathayo 26:63. Je, Yesu alitumia “Mabadiliko/marekebisho ya Tano?” (Naam! Kwa wale ambao si Wamarekani, Marekebisho ya Tano ya Katiba ya Marekani yanawalinda raia dhidi ya kujiponza/kujitia hatiani wenyewe.)
    3. Soma Mathayo 26:63-66. Je, kuhani mkuu anakiuka sheria? (Ndiyo. Hakupaswa kusihi kwa jina la Mungu kwamba Yesu anajiponza/anajitia hatiani wenyewe, na alifahamu kuwa ushahidi wa Yesu pekee haukutosha kumtia hatiani.)
      1. Je, hii inatufundisha nini juu ya kukabiliana na mamlaka? (Si mara zote mamlaka inakuwa nzuri, na mamlaka haitendi haki mara zote.)
      2. Tunapokabiliwa na mamlaka ya serikali isiyotenda haki, je, tunapaswa kutegemea juu ya nini? (Soma Danieli 2:44. Mungu anawadhibiti wafalme na falme. Hatimaye ataangamiza falme zote hizi za kidunia.)
    4. Soma tena Matendo 4:27-28. Je, tunaweza kuwa na ujasiri juu ya nini? (Hata kama mambo yasiyo ya haki yanaweza kututokea, tunafahamu kuwa Mungu ndiye mwenye udhibiti na kwamba hatimaye mapenzi yake lazima yawe juu ya vyote (yashinde).)
    5. Rafiki, je, nini mtazamo wako juu ya serikali? Kama mtazamo wako ni wa kiuhasama, kwa nini leo usitambue kwamba Mungu huweka mamlaka za kibinadamu. Ingawa serikali/mamlaka inaweza isienende vizuri, Mungu anatusihi tuiheshimu serikali isipokuwa tu pale ambapo suala lisilo la kimaadili linajitokeza.
  5. Juma lijalo: Kuwafanya Mataifa Kuwa Wanafunzi.