Kristo, Mwisho wa Sheria

(Warumi 5 - 8)
Swahili
Year: 
2014
Quarter: 
2
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, nini maana ya “mwisho wa sheria?” Mtu akikwambia “mwisho wako,” unaweza kuwa na wasiwasi sana kwamba “mwisho” maana yake ni “kifo.” Je, neno hilo linaweza kuwa na maana gani nyingine? Ikiwa una bosi wako anayeondoka kwenye kampuni, unaweza kusema kuwa, “Huo ndio mwisho wake!” Je, hicho ndicho kinachomaanishwa na Biblia (Warumi 10:4) kwamba “Kristo ndiye mwisho wa sheria?” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuweze kuangalia suala hili!

  1. Adamu Aliye Bora Zaidi
    1. Soma Warumi 5:12-13. Je, huyu “mtu mmoja” ni nani? (Fungu hili linamrejea Adamu.)
      1. Sheria gani ilikuwa inatumika Adamu alipotenda dhambi? Hii inasema kuwa dhambi haihesabiwi isipokuwa sheria, na Musa alipewa Amri Kumi muda mrefu sana baada ya dhambi ya Adamu! (Soma Mwanzo 2:15-17. Mungu alimpatia Adamu sheria dhidi ya kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Yumkini Mungu alimpatia sheria nyingine, lakini angalao kwa mahsusi tunaifahamu sheria hii aliyoitoa.)
    2. Soma Warumi 5:14. Je, dhambi ya Adamu ilileta nini? (Kifo, kama alivyoonya Mungu katika kitabu cha Mwanzo 2.)
      1. Je, ni nani huyu “ambaye atakuja,” na ni kwa jinsi gani Adamu ni mkondo ambao mtu huyo atapitia? (Jambo hili linamrejea Yesu. Kwa namna kadhaa ambazo Yesu alifananishwa na Adamu, njia inayohusika zaidi hapa ni kwamba wote wawili walikuwa na athari kubwa kwenye maisha na kifo kwa watu waliofuatia.)
      2. Kwa nini tunaona rejea ya kifo ikitawala “kuanzia kipindi cha Adamu hadi kipindi cha Musa?” Kwa nini Musa anaingizwa kwenye mjadala? (Hii inaweka bayana kwamba sheria inayozungumziwa ni Amri Kumi.)
  2. Kinga ya Dhambi
    1. Soma Warumi 5:15-16. Je, ni kwa namna gani “kosa” la Adamu na “karama” ya Yesu vinatofautiana sana? (Adamu alisababisha kifo na Yesu analeta uzima!)
    2. Soma Warumi 5:17-19. Katika vita, tunapenda kujisifu kuhusu idadi ya askari wa adui wanavyoweza kulinganishwa na askari mmoja wa upande wetu. Je, hapa kauli “yenye ulinganifu” ni ipi? (Dhambi moja ya Adamu ilileta kifo kwa kila mtu aliyefuata. Karama ya Yesu ilileta neema kwa kila mtu. Karama hiyo inaondoa dhambi nyingi na kuleta kuhesabiwa haki kwa wote “wanaoipokea.” Ni neema ya ajabu.)
    3.  
    4. Soma Warumi 5:20-21. Adamu alitakiwa kuepuka agizo moja na mti mmoja, angalao ndivyo inavyoonekana. Kwa nini Mungu aliongezea Amri Kumi ili kuongezea wingi wa dhambi? (Lengo ni kuongeza maarifa yetu. Utakumbuka kwamba Mungu mwenye upendo alitupatia sheria ya maadili ili kutuepusha kudhuriwa na utendaji wa sheria ya asili. Sasa tunafahamu zaidi kuhusu mwelekeo sahihi wa kuufuata, sasa tunao mwongozo wa kuepuka kutenda makosa ya kutisha maishani, na habari njema zaidi ni kwamba neema inaongezeka kutokana na wingi wa sheria.)
    5. Chukulia kwamba wewe ni mzazi na unampa mwanao utaratibu wa kufuata. Tuchukulie kwamba utaratibu huo ni kwa mtoto huyo kuwepo nyumbani ifikapo saa nne za usiku. Je, utakuwa mzazi mzuri? Je, utakuwa na mtoto mzuri? (Mwanao atakuwa na fursa ndogo sana ya kutokukutii. Lakini, mwanao atakuwa kwenye vihatarishi vya maswahibu yote anayokabiliana nayo kila mtoto – isipokuwa tu mwanao hatakuwa na mwongozo kutoka kwako!)
  3. Sheria na Neema
    1. Soma Warumi 6:1. Tumejifunza kuwa Yesu alitupatia uzima, na kwamba neema yake inafunika dhambi nyingi, na kwamba sheria ilitolewa ili dhambi iongezeke. Tunaweza kusamehewa kwa kufikiri kuwa dhambi si jambo baya kivile. Je, tuendelee kutenda dhambi ili neema iendelee kuongezeka? (Tukiwapatia watoto wetu zaidi ya kanuni moja, je, hiyo inamaanisha kuwa wanapaswa kukiuka kanuni nyingi kwa kadri tunavyowapatia?
    2. Soma Warumi 6:2-4. Je, “tulikufaje” dhambini? Ikiwa kukiuka sheria ya maadili inamaanisha kuwa tunajiweka kwenye hatari ya kudhuriwa na utendaji wa sheria ya asili, tunawezaje basi kuifia dhambi? (Hili ni jambo la muhimu. Dhambi inatuathiri kwa namna mbili. Njia ya kwanza ni ya dhahiri zaidi ya inatendeka mara moja: unatenda dhambi na unajiingiza kwenye matatizo. Sheria ya asili inaingilia kati. Unapata hasira na kumpiga mtu, kuna uwezekano mkubwa kwa mtu huyo kujibu mapigo. Njia ya pili ni madhara ya muda mrefu ya dhambi. Dhambi huleta kifo cha milele. Tunapobatizwa, kiishara tunakufa katika Yesu. Kama Yesu alivyolipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu kwa kifo chake, vivyo hivyo tunakufa katika Yesu kwa ajili ya dhambi zetu. Tunapoibuka kutoka kwenye maji ya ubatizo, tunaibuka na kuishi maisha mapya pamoja na Yesu. Adhabu ya kifo cha milele tayari imeshalipwa kwa njia ya Yesu.)
      1. Je, huu ndio mwisho wa sheria? Kama ndivyo, ni kwa namna gani? (Ni mwisho wa uwezo wa sheria kutuua milele kwa ajili ya dhambi zetu. Kama jinsi mwenzi aliyefariki asivyofungwa na kiapo cha ndoa, vivyo hivyo tunapokufa katika Yesu adhabu ya dhambi inalipwa. Hata hivyo, kwa kuwa dhambi ilisababisha kifo cha Yesu (na, katika yeye, kifo chetu) kwa nini tunataka kutenda dhambi? Kwa nini tunataka kuwa wapumbavu sana kiasi cha kupuuzia matatizo yanayoletwa na dhambi mara moja?)
  4. Ramani na Utumwa
    1. Soma Warumi 6:5-7. Je, umewahi kuyasikia madubwana? Hapa Marekani tuna mambo ya kubuniwa ya ajabu yasiyo ya Kibiblia yaliyopo kwenye vitabu, televisheni na sinema kuhusu watu waliokufa, lakini bado wanaendelea kuishi bila ukomo. Wanaitwa “madubwana (zombies).” Endapo ungekuwa dubwana, je, ungeogopa kufa? (Hapana. Tayari ulishakufa. Kitabu cha Warumi kinatuambia kwamba kwa kuwa tayari tulishakufa katika Yesu, hatuhitaji kuogopa kifo kutoka dhambini. Tunaingia kwenye maisha mapya pamoja na Yesu kwa njia ya ufufuo wake.)
    2. Soma Warumi 6:15-18. Jambo gani linapaswa kutuhamasisha kujitahidi kuishi kwa mujibu wa sheria hata kama haiwezi tena kutuua tunapoungana na Yesu? (Je, umewahi kuwa na mazoea mabaya (kutawaliwa/“addiction”) ya kitu fulani? Je, umewahi kudhuriwa na dhambi zako? Sheria za asili bado ziko hai (zinafanya kazi) na ni nzuri. Ikiwa unataka kuepuka utumwa unaotokana na dhambi, basi unatakiwa kuepuka dhambi.)
    3. Soma Warumi 6:19. Sisi ni wadhaifu, je, tunaepukaje utumwa wa dhambi? (Tunafanya uamuzi. Tunaamua kujitoa “kwenye uchafu na uasi unaoongezeka kwa kasi” au “kujitoa utumwani na kuingia kwenye haki tupate kutakaswa.” Mnaokolewa kwa neema. Mlikufa katika Yesu kwa ajili ya dhambi zenu. Sasa chagua utakayemtumikia!)
      1. Wangapi kati yenu mnaweza kuthibitisha (kushuhudia) ukweli kwamba dhambi huleta mazoea mabaya (addiction)? Na kwamba dhambi inasababisha “kuongezeka kwa uasi?” (Ikiwa unaona kuwa jambo hili ni kweli, basi inaonyesha jinsi ilivyo muhimu kuachana na dhambi.)
  5. Neema Safi!
    1. Soma Warumi 7:14-20. Je, unaweza kulihusianisha jambo hili na sisi?
    2. Soma Warumi 7:21-23. Je, unaweza kulihusianisha jambo hili na sisi?
      1. Utagundua kwamba mjadala huu unafuatia mjadala juu ya kuifia dhambi tuliojadili katika sura iliyopita (Warumi 6). Je, Paulo anaelezea maisha ya mtu aliyeokolewa kwa neema? (Paulo anajielezea yeye mwenyewe! Kwa dhahiri mtu aliyevuviwa na Mungu kuandika sura ya 6 ya kitabu cha Warumi ni mtu aliyeokolewa kwa neema.)
    3. Soma Warumi 7:24-25. Muda mfupi uliopita nimekuhamasisha kuchagua kuwa mtumwa wa haki. Je, tunaweza kuwa watumwa wa mambo yote mawili? (Paulo anasema kuwa akili yake ni mtumwa wa Mungu na asili yake ya dhambi ni mtumwa wa dhambi.)
    4. Soma Warumi 8:1-3. Ikiwa unajisikia kama Paulo, je, ujumbe wa Biblia kwako ni upi? (“Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.” Sifa kwa Mungu!)
    5. Soma Warumi 8:4-5. Je, Paulo anajichanganya? Nilidhani kwamba akili yake ni mtumwa wa Mungu na asili yake ya dhambi ni mtumwa wa dhambi? Paulo ametuambia kuwa alitenda mambo ambayo hakutaka kuyatenda. Anawezaje kusema kuwa hatutakiwi “kuishi kwa mujibu wa asili ya dhambi?” (Warumi 8:3-4 inatuambia kuwa tunatimiza matakwa ya sheria kwa njia ya Yesu. Hata hivyo, tunaona vita vinavyoendelea maishani mwetu, kama ilivyo kwa Paulo. Ingawa vita vinaendelea, tumeokolewa! “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.” (Warumi 8:1) Lakini, lazima tuchague kuishi kwa mujibu wa sheria ya Mungu.)
    6. Unawezaje kufanya uchaguzi sahihi? (Soma Warumi 8:9 na Warumi 8:5. Unamwomba Roho Mtakatifu akae ndani yako. Unaiweka akili yako kwenye kile ambacho Roho anakitamani!)
    7. Hilo bado haliko wazi. Tayari Paulo alituambia (Warumi 7:22-25) kuwa akili yake ilikuwa mahali sahihi, lakini mwili wake haukuwa mahali sahihi. Tayari akili yake imewekwa “kwenye kile ambacho Roho anakitamani.” Je, tunaweza kutenda jambo gani jingine? Au je, “tunachokitenda” kinatuweka nje ya msitari? Je, hiki ni “anachokitenda Mungu” tu?
    8. Soma Warumi 8:12-14. Je, mafungu haya yanasema nini juu ya wajibu wetu? (Tunayo sehemu ya muhimu katika jambo hili. Lakini sehemu yetu ni kuwa na ubia na Roho Mtakatifu “kuyafisha matendo ya mwili.”)
  6. Je, huu ni muhtasari sahihi? Sheria si tishio tena la kifo kwetu, kwa sababu katika ubatizo wetu tulikufa kwa ajili ya dhambi katika Yesu na kuibuka katika maisha mapya. Hata hivyo, sheria bado ni ya muhimu kwetu. Miongoni mwa mambo mengine, sheria ni mustakabali unaotuepusha kuwa watumwa wa mazoea yetu mabaya ya dhambi. Hata katika maisha mapya, tunaona kuwa pambano la wazi dhidi ya dhambi linaongezeka kila siku. Lakini, ufumbuzi wa jambo hili ni kuchagua kumwomba Roho Mtakatifu kila siku ili atusaidie kuziweka akili zetu kwenye mambo ambayo Mungu anayataka na kuizika dhambi maishani mwetu.
    1. Rafiki, je, utaikubali changamoto hii? Je, utaikubali karama ya bure ya uzima wa milele, na kukubali changamoto ya kila siku kuishi maisha yenye kuongozwa na Roho Mtakatifu, maisha ambayo unachagua kuishi kama mwana au binti wa Mungu?
  7. Juma lijalo: Sheria ya Mungu na Sheria ya Kristo.