Alama/Kinga Kilichonyakuliwa Kutoka Motoni

(Zakaria 1-3
Swahili
Year: 
2011
Quarter: 
2
Lesson Number: 
9

Utangulizi: Habari kubwa juma hili ni kwamba mkuu wa Shirika la Fedha Duniani, na mtu anayeongoza kwenye kura za maoni za uchaguzi wa Urais nchini Ufaransa, alimshambulia kijinsia mwanamke aliyekuwa akisafisha chumba chake hotelini. Chukulia kwamba hii ni kweli, je, ni kwa nini kitu kama hiki kinatokea? Je, ni kwa jinsi gani mtu wa kisasa, muhimu, mstaarabu ajihusishe kwenye tabia ya kutisha kama hiyo? Je, tunaweza kucheka kwa kujiamini na kunyooshea kidole? Au, je, wewe na mimi tuna uwezo dhidi ya mambo kama hayo? Jibu la Mungu ni “ndiyo,” huu unapaswa kuwa wakati wa ukweli kwetu sisi sote. Katika Warumi 3:10-18 Paulo ananukuu kauli ya Agano la Kale kwamba sisi sote “hatustahili.” Hakuna mwenye haki hata mmoja. Mwisho wetu sote ni kuunguzwa (Malaki 4:1). Somo letu juma hili ni kuhusu kunyakuliwa kutoka katika ule moto. Hilo linaonekana kuwa kama lengo muhimu! Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na kubaini zaidi.

I. Njia Kuelekea Kwenye Nyumba ya Mungu

    A. Soma Zekaria 1:1. Je, Dario ni nani? (Soma Danieli 5:30-6:2. Ni mfalme wa Wamedi aliyeishinda Babeli.)

    B. Soma Zekaria 1:2-6. Je, nini kilitokea pale Mungu alipowakasirikia baba zao? (Walichukuliwa utumwani na Babeli na utumwa huo uliendelezwa na Wamedi/Waajemi.)

1. Je, wangapi kati yetu, kwa sababu ya chaguzi duni, tunajikuta kuwa tu watumwa wa dhambi?

 C. Soma Hagai 1:1. Baini kipindi cha muda unaohusika. Je, unafananaje na ule wa Zekaria? (Ni mwaka uo huo! Tuna manabii wawili wa Mungu wanaotoa ujumbe kwa watu wake.)

D. Soma Hagai 1:2-6. Je, ni mpangilio/mwelekeo gani tunaouona kwenye ujumbe wa hawa manabii wawili? (Pale ambapo hatumsikilizi/hatumjali Mungu, tunakuwa na matatizo. Ni vigumu kufanikiwa.)

E. Sehemu ya mwisho ya Zakaria 1:6 inasema kuwa watu wa Mungu walikiri kuwa walistahili mambo mabaya waliyoyapata – na walitubu dhambi zao. Soma Zekaria 1:16-17. Je, mtazamo wa Mungu kwetu ni upi pale tunapotubu? (Anataka kutuonyesha rehema zake. Anataka kutubariki.)

F. Je, lengo mahsusi la Mungu kwa Yerusalemu ni lipi? (Unabii wa Zekaria na Hagai unazungumzia kuhusu kujenga upya nyumba ya Mungu (hekalu). Mungu atawaunganisha watu wake.)

II. Kuingia Katika Nyumba ya Mungu

A. Soma Zekaria 2:10-13. Fungu la 11 linaposema “mataifa mengi” linamzungumzia nani? (Mungu anasema kuwa watu wa Mungu sio tu kwamba ni Wayahudi. Badala yake, mataifa yote na makabila “watajiunga na Bwana katika siku ile, nao watakuwa watu wangu.” Tunaweza kuingia katika nyumba ya Mungu na kuishi pamoja naye!)

1. Swali ni kwamba, tunaingiaje kwenye nyumba ya Mungu?

B. Soma Zekaria 3:1. Je, Yoshua ni mtu mwema au mbaya? (Soma Ezra 3:2-4. Yoshua sio tu kwamba ni Kuhani Mkuu, anazirejesha kafara na sikukuu mahali pake kama ilivyoelekezwa na Musa. Kwa hakika ni mtu mzuri/mwema.)

1. Kama yeye ni mtu mwema, kwa nini Shetani anamshtaki? (Soma Waebrania 9:7. Kuhani Mkuu alibeba dhambi za watu. Kimsingi, tunashtakiwa na Shetani.)

C. Soma Zekaria 3:2-3. Je, Shetani yuko sahihi kumshtaki Yoshua? (Ndiyo. Sio tu kwamba amevaa nguo “chafu sana,” lakini pia nywele zake zi motoni. (Sehemu ya mwili wake ipo motoni).)

1. Je, kuwa “mchafu sana” na kuwa motoni kunamaanisha nini? (Soma Ufunuo 20:15. Yoshua ni mdhambi – mdhambi sana. Anakaribia kuunguzwa/kuchomwa kutokana na dhambi zake.)

 2. Je, kuna hoja yoyote kwamba Shetani hayuko sahihi kumshtaki Yoshua? (Shetani ni mbaya zaidi! Hata hivyo, Shetani hayupo kwenye suala lisilokuwa na umuhimu.)

3. Je, Mungu anajibuje hizi tuhuma dhidi ya mtu mchafu kwa dhahiri kabisa? (Mungu anamkemea Shetani!)

 4. Fikiria kuhusu hili kwa muda kidogo. Kama hali hii sio ya muhimu, na Mungu ni hakimu na Shetani ni mshitaki, kwa nini Shetani amtuhumu Yoshua kama naye atakemewa kutokana nayo (Ninatia shaka kwamba Shetani anadhani anashinda hoja zake kwa Mungu. Swali ni kama anashinda alama nyingi kwako?)

D. Soma Zekaria 3:4. Je, ilimgharimu nini Yoshua kuwa huru dhidi ya dhambi? (Tamko la mbingu.)

1. Je, mavazi ya “thamani nyingi” aliyopewa Yoshua ni yapi? (Soma Mathayo 22:11 na Ufunuo 7:9. Ni alama ya haki.)

2. Je, Yoshua ana wajibu gani kwenye msamaha wa dhambi zake na dhambi zetu? (Kuhani Mkuu alikuwa mwombezi. Alisimama mbele za Mungu katika nyumba ya Mungu (hekalu) akibeba dhambi za watu.)

E. Soma Waebrania 8:1-2 na Waebrania 9:24-26. Je, kisa cha Yoshua na uelewa wetu wa patakatifu pa mbinguni unajihusishaje kwetu hivi leo? (Tunaokolewa vivyo hivyo. Sisi tu wachafu sana. Tunakuja mbele za Bwana tukikiri dhambi zetu na kuomba uombezi wake. Anatuondolea dhambi zetu kiurahisi kama vile kuvua nguo. Anatupatia haki yake kiurahisi kama vile kuvaa nguo.)

 

F. Soma Zekaria 3:5. Nani anazungumza? (Zekaria.)

1. Je, ana mamlaka gani ya kuamuru kwamba Yoshua apewe “kilemba kizuri?” (Watoa maoni wanadokeza kuwa hii ilikuwa sala, au ombi, kinyume na amri.)

 

 2. Ni ishara gani unayoiona kwenye mfululizo wa mtu anayeomba kilemba kisafi (kizuri) baada ya kuwa amepewa vazi la haki? (Sijampata mtoa maoni yeyote anayekubaliana nami, lakini hili ni wazo langu. Ni kitu gani cha kwanza unachotaka kukifanya baada ya kuwa umeonyeshwa neema? Unataka badiliko kwenye mtazamo wako, fikra yako. Wazo lako lipo kwenye pale dhambi inapoanzia. Kama Mfalme Daudi unataka “moyo safi” (Zaburi 51:10).)

G. Soma Zekaria 3:6-7. Juma lililopita tulijifunza kisa cha Yesu kuhusu Msamaria Mwema. Yesu alielezea kisa cha Msamaria kikiwa ni jibu la swali (Luka 10:25), “Nifanye nini niurithi uzima wa milele?” Je, haya ni maelekezo mengine ya jinsi ya kufika mbinguni? (“Wale wanaosimama hapa” ni viumbe wa mbinguni.)

1. Je, tumerejea kwenye wokovu kwa matendo? Msamaria Mwema chaweza kuwa kitu cha kale ambacho hakikuwepo, lengo linaoonekana kutofikiwa. Lakini, lugha hii ni ya wazi – tunaitiwa kwenye aina fulani hivi ya matendo.)

2. Je, unadhani inamaanisha nini “kuongoza nyumba ya [Mungu] na kuwa na mamlaka ya mahakama za [Mungu]? (Kuhani Mkuu “aliongoza” nyumba ya Mungu. Hakimu mkuu alikuwa na mamlaka na mahakama za Mungu. Lakini angalia, 1 Wakorintho 6:2.)

a. Je, hii inabadili maana ya fungu ya “kwenda mbinguni”? (Mungu hatuambii tu jinsi ya kwenda mbinguni, anatuambia jinsi ya kufikia ngazi ya  juu mbinguni. Wale “wanaosimama hapa” walikuwa kwenye uwepo wa Mungu.)

3. Je, tumeitiwa kwenye matendo gani? (Kutembea na kushika matakwa/mahitaji.)

a. Je, ishara ya “kutembea” inapendekeza nini? (Sio uchanganuzi/uchambuzi wa mara kwa mara wa  matendo yako, badala yake ni mwelekeo wa jumla wa maisha yako.)

                   b. Je, “kuyashika matakwa/mahitaji” kunapendekeza nini? (Kutii amri za Mungu.)

H. Je, tunapaswa kuhitimishaje kuhusu njia ya kuuelekea wokovu? (Msamaha wa dhambi na vazi la haki havitegemeani na matendo yetu. Yanategemeana na sisi kuja mbele za Mungu kwa ajili ya msamaha, na kisha Mungu anatupatia haki. Muda. Hata hivyo, maisha yetu hayaishii hapa. Tuna akili safi. Tunahitajika kuitikia upendo wa Mungu kwa maisha ambayo kwa ujumla yanaendana na mapenzi yake. Tunahitajika kuwa makini kwenye amri zake na kujaribu kuzishika.)

1. Je, maisha yetu ya haki yanaleta tofauti yoyote? (Matendo yetu hayatatuokoa, lakini hii inapendekeza kuwa yanaathiri hadhi yetu mbinguni! Hili sio fungu pekee la namna hii. Baini, pamoja na mengine, Mathayo 5:19 na Mathayo 6:19-20.)

I. Soma Zekaria 3:8-9. Mungu anatuambia tuwe makini zaidi kuhusiana na hili suala. Kwa nini? (Kwa sababu kisa hiki kinaashiria mambo yajayo. Mungu anakaribia kutuambia mambo yetu yajayo.)

1. Je, “Tawi” hili ni nani? (Soma Yeremia 23:5-6. Yesu!)

2. Je, “Jiwe” ni nani? (Soma Danieli 2:44-45. Jiwe pia linaweza kumrejea Yesu.)

 a. Baini kuwa Jiwe lina “macho saba.” Je, hiyo inatufundisha nii kuhusu siku zijazo? (Ya kwamba Yesu ana maono makamilifu. Anaangalia maisha yetu, anaangalia kwa ajili yetu.) 

3. Katika siku zijazo, “dhambi ya hii nchi” itaondolewa kwa siku moja. Je, hiyo ilitokea? (Ndiyo! Wakati Tawi, Jiwe, linapokufa kwa ajili yetu na kufufuka kwa uzima wa milele! Bwana asifiwe!)

J. Rafiki, juma lililopita na juma hili tumezungumzia jinsi ambavyo unaweza kuokolewa kwa neema pekee. Hakuna unachoweza kufanya kuupata wokovu. Baada ya wokovu wetu, Mungu anatuita kutembea katika njia zake na kuwa watiifu kwa amri zake. Katika mwanga wa kile ambacho Yesu amefanya kuokoa maisha yako, na maisha ya wale unaowapenda sana, je, utadhamiria hivi leo kuomba kwa ajili ya kuwa na akili safi ili kwamba matendo safi yatafuatia?

III. Juma Lijalo: Mavazi Mapya ya Mwana Mpotevu.