Nyuma ya Barakoa [Kinyago]
Somo la 10: Nyuma ya Barakoa [Kinyago]
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Katika kusoma kwangu juma hili nimekutana na msemo unaosema kwamba: “Mtu mwenye historia ya kupitia mambo magumu hutoa ushauri mzuri.” Mithali tulizojifunza hadi sasa zinaashiria kwamba watu waliokuwa na hekima siku za nyuma ni chanzo bora cha hekima. Lakini, msemo huu unaashiria jambo muhimu: maonyo na changamoto maishani vinakuza hekima yetu. Somo letu juma hili linaangalia jinsi tunavyoweza kupata hekima zaidi. Hebu tuchimbue somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!
- Siri na Wafalme
- Soma Mithali 25:2. Mwitikio wangu wa kwanza katika fungu hili ulikuwa ni wa kufurahia kwa sababu Mungu hafunui dhambi zangu zote! Lakini, soma Marko 4:11. Je, hii inaashiria nini juu ya kile ambacho Mungu anakificha? (Mungu anafunua mambo ya muhimu kwa wafuasi wake, lakini anayaficha kwa watu wengine.)
- Soma Marko 4:12. Nilidhani kwamba Yesu alizungumza kwa njia ya mifano ili mafunzo yake yaeleweke kwa urahisi! Unaelezeaje jambo hili?
- Angalia tena Mithali 25:2. Utukufu wa wafalme ni upi? (Kuchunguza jambo.)
- Hebu tutumie jambo hili kwenye mifano. Kwa nini wafuasi wa Yesu waelewe mifano yake na walimwengu wasielewe? (Kwa sababu walitafuta kufahamu maana ya mifano.)
- Unadhani jambo gani linazungumzwa kwenye Mithali 25:2? (Mungu ni mkuu sana na mwenye utukufu mwingi kiasi kwamba hatuwezi kuelewa njia zake zote. Lakini, ni kwa ajili ya utukufu wetu kujaribu “kuchunguza” asili ya Mungu na mafunzo yake kwetu.)
- Soma Mithali 25:3. Wafalme sio wagumu sana kufahamu mambo yao kuliko ilivyo kwa Mungu. Kwa nini tunaweza kumchunguza Mungu na si wafalme? (Mungu anatenda kazi kwa mujibu wa kanuni ile ile ya upendo, wakati wanadamu wanaongozwa na hisia mchanganyiko zenye kukinzana.)
- Soma Mithali 25:4-5. Je, jambo hili pia linahusika kwako? Je, unatakiwa kuondoa kilicho kiovu mbele zako? (Ikiwa tunataka kuishi maisha ya haki, tunatakiwa kuondoa kilicho kiovu.)
- Soma Mithali 25:6-7 na Luka 14:7-11. Mara ngapi unakabiliana na masuala yanayohusu mahali pa kukaa wakati wa chakula?
- Kama si mara nyingi, je, unawezaje kuweka suala hili kivitendo leo? (Huwa ninatumia ushauri huu kivitendo kwenye uhusiano wangu kazini na kwenye taasisi nyingine, kama vile kanisani.)
- Kwa nini mtu anadai nafasi ya kwanza kazini au kanisani? (Yumkini ni majivuno.)
- Je, hii inaonekanaje kutokana na majivuno yako? (Unajisikia kudhalilika ikiwa utaambiwa kushuka chini [kurudi nyuma]. Kwa upande mwingine, ikiwa utaambiwa kupanda juu [kusogea mbele], kitendo hicho kitakukweza.)
- Soma Mithali 25:7 (sehemu ya mwisho) na Mithali 25:8. Inamaanisha nini kusema “court?” (Nadhani inamaanisha kuwa mbele ya mtu mwenye mamlaka.)
- Je, jambo la kujifunza maishani leo ni lipi kutokana na muktadha huo? (Inaweza kumaanisha jambo la kimahakama, lakini jambo la kawaida zaidi linaloweza kutumika ni pale unapomshitaki mtu mwingine kazini au kanisani.)
- Kwa nini utakuwa unajihatarisha kupata fedheha? (Hukufanya uchunguzi wa kutosha, hufahamu kweli zote zilizopo [huna ushahidi wa kutosha], na jirani yako atakufanya uonekane mpumbavu.)
- Chukulia muktadha tofauti kidogo. Unapendekeza wazo (ushauri) jipya kazini. Unatoa ushauri huo haraka haraka ili uweze kumshinda kila mtu kwa huo ushauri ulioutoa. Je, mithali hii inahusika hapa? (Ndiyo. Hili ni jambo la kujifunza ninalojikumbusha mara kwa mara. Tafakari mambo kwa makini sana kabla hujawasilisha wazo jipya au mpango mpya.)
- Soma Mithali 26:27. Je, mbinu gani nyingine za kawaida kazini tunazopaswa kuziepuka? (Adhabu. Ikiwa mtu atakudhuru, hatupaswi “kuwachimbia shimo.” Shimo hilo litaishia kutudhuru sisi wenyewe.)
- Soma Mithali 25:2. Mwitikio wangu wa kwanza katika fungu hili ulikuwa ni wa kufurahia kwa sababu Mungu hafunui dhambi zangu zote! Lakini, soma Marko 4:11. Je, hii inaashiria nini juu ya kile ambacho Mungu anakificha? (Mungu anafunua mambo ya muhimu kwa wafuasi wake, lakini anayaficha kwa watu wengine.)
- Maneno
- Soma Mithali 25:11. Je, hili ni jambo zuri au halina maana? Huwezi kula matufaa (apples) ya dhahabu! (Fumba macho yako kisha ujaribu kufikiria matufaa ya dhahabu yaliyo kwenye vyombo vilivyotengenezwa kwa madini ya fedha. Ni mazuri sana, sawa? Maneno yako yanaweza kuwa mazuri kiasi hicho – na kuinua mioyo ya watu wengine.)
- Soma Mithali 25:12. Je, unapenda kukaripiwa? Je, unapenda kuonywa? (Hakuna mtu anayependa kuonywa.)
- Ingawa hatupendi karipio, je, tunapaswa kufanya nini? (Ikiwa karipio linatoka kwa mtu mwenye hekima, tunapaswa kulisikiliza.)
- Je, kusikiliza maonyo kwa makini kutatufanya tuonekane watu bora? (Naam. Kipuli cha dhahabu kinapendezesha sikio. Kusikiliza kwa makini maonyo kutoka kwa watu wenye hekima kunatufanya kuwa watu wazuri zaidi.)
- Soma Mithali 27:5-6. Je, mara zote rafiki wa kweli tena mwenye hekima anakupatia ushauri unaopenda kuusikia? (Hapana. Mara zote “adui” wako anakubaliana nawe. Makaripio ni mazuri kwetu ikiwa yanatoka kwa marafiki wenye hekima.)
- Soma Mithali 26:23-26. Je, adui wako atakuambia maneno yenye kukutia moyo? (Ndiyo.)
- Je, tunajifunza nini kutokana na jambo hili? (Hatupaswi kuwahukumu watu kwa kuangalia kama wanakubaliana nasi au wanatukemea. Baadhi ya maneno yanayokubalika yanalenga kutudhuru, wakati ambapo karipio la hekima ni jambo la baraka.)
- Soma Mithali 27:17. Je, “chuma” ni nini kwenye uhusiano? (Chuma ni kigumu. Kwa hiyo changamoto ngumu na makaripio makali, yanatufanya kuwa watu bora zaidi – ikiwa tuna hekima.)
- Soma Mithali 25:15. Unapotaka kubadili mawazo ya mtu, unatumia njia gani kutimiza azma hiyo? Je, unatumia njia ya kubishana? Je, unatumia amri? Je, unapaza sauti? Je, fungu hili linaashiria nini? (Kwamba matokeo ya upole na uvumilivu ni makubwa – matokeo yenye kuvunja mifupa!)
- Mawazo ya nani yanabadilishwa? (Mawazo ya mtawala. Jambo hili ni la muhimu, kwa sababu mtu anayeshawishiwa ana mamlaka juu yako.)
- Soma Mithali 25:20. Je, hii inatufundisha nini kuhusu kutoa ushauri? (Muda wowote mke wangu anapojihisi vibaya, huwa ninaweka tabasamu kubwa usoni mwangu na kumwambia, “Tafakari vizuri!”)
- Je, watu wanaojisikia vibaya huwa wanataka kusikia nini? (Huruma. Kumwimbia (furaha?) nyimbo mtu mwenye masikitiko au anayejisikia vibaya haisaidii. Kimsingi kitendo hicho kinamwongezea maumivu.)
- Soma Mithali 25:24. Unapotafuta kupata mwenzi, je, ni muhimu kiasi gani kumfahamu mtu huyo? (Fungu hili linazungumzia jambo muhimu juu ya uwezo wa ulimi. Hakuna mtu apendaye kuishi darini, achilia mbali katika pembe ya darini. Lakini hiyo ni bora zaidi kuliko kuishi na mwenzi mgomvi.)
- Soma Mithali 25:28. Kwa nini kuta zinazunguka mji? (Kuukinga dhidi ya wavamizi.)
- Je, kujidhibiti kunakulindaje – tofauti na kuwalinda watu wengine? (Unaposhindwa kujidhibiti, unajiweka kwenye hatari ya matatizo ya aina yote. Ulinzi wako unakuwa umetoweka.)
- Kushughulika na Wapumbavu
- Soma Mithali 26:4-5. Wale mnaosema kwamba Biblia haijipingi, mnaelezeaje jambo hili? (Kwa wazi kabisa mwandishi wa hii mithali alitambua ukinzani wa dhahiri. Fungu la nne linatuambia tusifuate njia za mpumbavu katika kubishana na mpumbavu. Kwa upande mwingine, fungu la tano linapendekeza kwamba, kumwacha mpumbavu pasipo kumjibu kunamfanya mpumbavu adhani kwamba yuko sahihi. Hii inaonekana kuashiria kwamba wapumbavu wanapaswa kupewa jibu la hekima.)
- Soma Mithali 23:9. Sasa, tunapaswa kuwajibuje wapumbavu? Je, unaweza kuupata ukweli unaoendana na mafungu yote haya? (Usishindane na mpumbavu pembeni. Jibu lako ni kwa wale wanaosikiliza ubishani.)
- Soma Mithali 26:7 na Mithali 26:9. Je, kila mtu atanufaika na haya masomo ya Mithali? (Hapana.)
- Tatizo ni lipi? (Mithali hazina maana kwa wapumbavu, zinaweza kuwa hatarishi.)
- Soma Mithali 26:10. Je, unapaswa kumwajiri mpumbavu? (Hapana. Huwezi kubashiri madhara awezayo kuyafanya mpumbavu.)
- Soma Mithali 26:12. Je, panaweza kuwepo na jambo baya zaidi linalozidi upumbavu wa mtu? (Ndiyo! Kuwa na hekima machoni pako mwenyewe.)
- Kwa nini wapumbavu wana matumaini zaidi? (Mpumbavu anaweza kutambua upumbavu wake, lakini majivuno yanakupofusha usiweze kujiona jinsi ulivyo katika mwanga bora zaidi.)
- Rafiki, kama wewe ni mwanafunzi mwenye bidii katika kujifunza kitabu cha Mithali, na si mpumbavu, basi utafurahia kuwa na maisha bora. Kwa nini usiafiki, sasa hivi, kuishi kutokana na ushauri unaopatikana kwenye kitabu cha Mithali?
- Soma Mithali 26:4-5. Wale mnaosema kwamba Biblia haijipingi, mnaelezeaje jambo hili? (Kwa wazi kabisa mwandishi wa hii mithali alitambua ukinzani wa dhahiri. Fungu la nne linatuambia tusifuate njia za mpumbavu katika kubishana na mpumbavu. Kwa upande mwingine, fungu la tano linapendekeza kwamba, kumwacha mpumbavu pasipo kumjibu kunamfanya mpumbavu adhani kwamba yuko sahihi. Hii inaonekana kuashiria kwamba wapumbavu wanapaswa kupewa jibu la hekima.)
- Juma lijalo: Kuishi kwa Imani.