Mmisionari Asiyetarajiwa

(2 Wafalme 5)
Swahili
Year: 
2015
Quarter: 
3
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Unapofikiria mustakabali wako wa siku zijazo, je, huwa unapenda jambo gani litokee? Unapenda mambo mazuri yatokee! Afya njema, kazi nzuri, mahusiano mazuri ndio mambo tunayoyataka. Kwa wengine, matumaini ndio ya msingi zaidi: chakula cha kutosha, uhuru wa kuongea, uhuru wa kufanya kazi, uhuru wa dini (kuabudu). Na badala yake mambo mabaya yanapotokea, tunapata wakati mgumu kuelewa jinsi Mungu mwenye upendo anavyoweza kuyaruhusu mambo hayo yatokee. Yohana 9:1-3 inaelezea mjadala unaomhusu kipofu. Yesu alielezea kwamba mtu huyo alikuwa kipofu “ili kazi za Mungu zidhihrishwe ndani yake.” Tunapokabiliana na nyakati ngumu, hiyo ni fursa kwa Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi kuhusu jambo hili lenye kuvutia!

  1. Naamani na Mwanamke Kijana
    1. Soma 2 Wafalme 5:1. Nani aliyekuwa nyuma ya mafanikio ya Naamani? (Mungu alikuwa amempatia mafanikio kijeshi.)
    2. Soma 2 Wafalme 5:2. Kwa nini mwanamke huyu kijana alikuwa mateka? Je, haya si matokeo na mibaraka kwa Naamani?
      1. Ikiwa mwanamke huyu kijana anatokea Israeli, je, Mungu amempa ushindi Naamani dhidi ya Israeli? (Kimsingi, mambo hayako hivyo. Shamu (Syria) ilifanikiwa kuwazuia Washami – taifa kubwa katika eneo lile. Shamu inajihusisha kuivamia Israeli, lakini haijaishinda Israeli.)
      2. Utamchukuliaje Mungu wako ikitokea kwamba mibaraka yake kwa Naamani ilifanikisha kukufanya wewe kuwa mateka?
    3. Je, ungependa kuwa Naamani? (Yeye ni kiongozi wa juu nchini, bwana (mkubwa) wake anampenda, wananchi wanampenda, na yeye ni mwerevu na mwenye mafanikio. Hata hivyo, anao ugonjwa wa kutisha: ukoma.)
    4. Soma 2 Wafalme 5:3-4. Mwanamke huyu kijana ana mtazamo gani dhidi ya watu waliyemshika mateka? Je, unaweza kuwa na mtazamo kama huo?
      1. Unadhani Naamani anapokea ushauri kiasi gani kutoka kwa watumwa vijana wa kike?
      2. Utagundua kwamba ushauri wa binti mtumwa unapelekwa hadi kwa Mfalme! Unaelezeaje jambo hili? (Naamani ana shauku kubwa! Vinginevyo jambo hili halina mantiki yoyote.)
    5. Soma 2 Wafalme 5:5. Kwa nini Mfalme wa Shamu pamoja na Naamani wanapeleka dhahabu na fedha ikiwa waliitawala Israeli? (Hii inathibitisha kwamba Shamu haiitawali Israeli. Zinaweza kuwa nchi zenye mambo makubwa, lakini hazina udhibiti.)
  2. Mfalme wa Israeli
    1. Soma 2 Wafalme 5:6-7. Linganisha fikra ya mtumwa wa Naamani ambaye ni binti wa Kiisraeli na fikra ya Mfalme wa Israeli?
      1. Je, unakabiliana na matatizo magumu kama jinsi ambavyo Mfalme wa Israeli alivyokabiliana nayo?
      2. Mwanamke kijana ambaye ni mtumwa ni mmisionari wa Mungu. Ikiwa tunataka kuwa wamisionari wa Mungu, mwitikio wetu wa kwanza katika kila jambo maishani unapaswa kuwaje?
    2. Soma 2 Wafalme 5:8. Je, ungeuandika ujumbe wa Elisha kwa namna iyo hiyo?
      1. Linganisha maneno yanayopatikana katika 2 Wafalme 5:3? (Mungu anaelekeza namna ya kuandika hiki kisa. Ingawa inanisumbua akili kwamba mshale wa usikivu unaelekezwa kwa nabii badala ya kuelekezwa kwa Mungu, yumkini kitendo hiki kinaakisi mapenzi ya Mungu. Huenda huku ni kutokuelewa kwangu juu ya kile kinachosemwa.)
  3. Kiburi/Majivuno
    1. Soma 2 Wafalme 5:9-12. Je, Naamani ana mtazamo wenye mantiki?
      1. Soma Warumi 13:7. Naamani ana barua kutoka kwa Mfalme wa Shamu. Mfalme wa Israeli pia amemtuma kwa Elisha. Na kwa kuongezea, Naamani pia ni mtu muhimu. Kwa nini Elisha anampuuza na kukataa kumpa heshima?
      2. Hebu tutafakari upya jambo ambalo tumelijadili hapo kabla. Nilidhani kwamba Mungu ndiye anayepaswa kuwa kiini na si Elisha, nabii wa Mungu. Lakini, ikiwa kiini cha kisa hiki ni kwamba wote wawili waonekane kuwa kitu kimoja – nabii wa Mungu ni mwakilishi wa Mungu – basi hiyo inaleta mantiki kwamba “Mungu” hatahitajika kutoka nje kukutana na mwanadamu.)
      3. Je, kiburi chako kimeshawahi kukunyima mbaraka?
    2. Soma 2 Wafalme 5:13-14. Nani anayeongea maneno yenye mantiki kwa Naamani? Hii inatufundisha nini kumhusu Naamani? (Naamani ni mtu mwenye majivuno - na tunaweza kuelewa sababu za majivuno hayo. Lakini, hii inaakisi mwelekeo wa maisha yake: yuko radhi kupokea ushauri kutoka kwa watu walio “chini” yake. Utakumbuka kwamba alianza safari ya tukio hili lisilo la kawaida kwa sababu alikuwa radhi kupokea ushauri kutoka kwa mwanamke kijana ambaye ni mtumwa.)
    3. Hebu tuangalie tena 2 Wafalme 5:11. Je, jambo hili lingetimia endapo Mungu angeamua kutumia njia aliyoitaka Naamani? (Naam, ndiyo.)
      1. Je, kutimiza na kutekeleza kwa namna ambayo Naamani aliitaka kungeongeza manufaa ya kujikita kwa Mungu? (Maoni ya Adam Clarke yana mtazamo mzuri. Clarke anabainisha kuwa Naamani alitarajia Elisha “atoke na kuja kwangu” – msisitizo upo kwenye neno “kwangu.” Elisha anapaswa kusimama mbele ya Naamani (ambaye yupo kwenye gari lake la kijeshi) ili amwombe Mungu. Hii inawaweka wote wawili, yaani, Elisha na Mungu, katika kumhudumia Naamani. Uponyaji unapaswa kufanyika kwa namna ambayo Naamani anadhani kuwa ni sahihi.)
        1. Je, ni mara ngapi unataka Mungu atende mambo kwa namna unayoitaka wewe?
  4. Utukufu kwa Mungu
    1. Soma 2 Wafalme 5:15. Linganisha na 2 Wafalme 5:9. Jambo gani limebadilika? (Naamani ameshuka kutoka juu ya farasi na magari yake. Elisha ametoka ili kumwona Naamani.)
      1. Je, hizi jitihada za kimisionari zimefanya kazi? (Ndiyo, na Mungu na Elisha hawakumtendea Naamani kwa uungwana.)
        1. Je, kuna cha kujifunza hapa kuhusu utume? Si mara zote Mungu mwenye upendo ni mkarimu?
    2. Soma 2 Wafalme 5:16. Linganisha na 1 Timotheo 5:17-18. Ikiwa mfanyakazi anastahili ujira wake, kwa nini Elisha hakuchukua ujira wake? (Unakumbuka nilivyokuwa ninachukulia kuhusu kuweka msisitizo kwa nabii badala ya Mungu? Hii ni kauli ya wazi kuhusu nani anayewajibika na uponyaji. Ikiwa Elisha alimponya Naamani, basi angepata ujira wake. Lakini, Mungu mkuu wa mbinguni ndiye aliyemponya Naamani. Kitendo cha Elisha kupokea ujira kingechukua sifa kwa kazi ya Mungu.)
    3. Soma 2 Wafalme 5:17. Unawezaje kuelezea ombi hili lisilo la kawaida? Kwa nini Naamani anahitaji uchafu? (Hii inaakisi kasoro kwenye teolojia ya Naamani. Anadhani kuwa miungu ina himaya – kwamba kila taifa lina mungu wake. Anataka uchafu kutoka Israeli, ili aweze kumwabudu Mungu wa kweli katika udongo utokao Israeli.)
    4. Soma 2 Wafalme 5:18-19. Je, utampa Naamani alama kwa jambo hili? Naamani anamwelezea Elisha kwamba kazi yake inamtaka amsujudu mungu wa kipagani. Mara kwa mara katika kazi yangu ya sheria huwa nina wateja wanaokataa kukana imani zao za dini ili kukubaliana na matakwa ya kazi zao!
      1. Hebu tujadiliane jambo hili: Kwanza, Naamani ana uelewa mdogo sana wa kiteolojia ambao kwa dhahiri unadidimiza mamlaka ya Mungu. Pili, anaomba ruhusa ili aendelee kutenda dhambi katika siku zijazo. Majibu ya Elisha kwa haya matatizo mawili makubwa ni kwamba “Mungu ni amani.” Kwa nini?
      2. Kuna mjadala mrefu unaoendelea kuhusu kama ni vyema kuhakikisha kuwa mtu anafahamu “kanuni” zote kabla hajabatizwa au asibatizwe. Tunapowabatiza bila kuwaelezea kanuni, kuna mtu ambaye huwa anachukua hatua za haraka kuwarekebisha waumini wapya. Je, jibu la Elisha linatufundisha nini kuhusu suala hili?
      3. Soma Luka 23:40-43. Mtu huyu sio tu kwamba hakuhudhuria darasa la ubatizo, bali pia hakuweza kubatizwa! Je, huu ni “upendeleo wa mara moja” unaotokana na mazingira yaliokuwepo? (Jibu kwa mfululizo wa maswali haya ni kwamba mara nyingi huwa tunaingilia kazi ya Roho Mtakatifu. Ikiwa mtu anataka kubatizwa, tunapaswa kumsaidia abatizwe bila kuweka vizingiti vingi visivyo vya msingi. Mara mtu anapomkiri Yesu, kama alivyofanya mwizi pale msalabani, basi Roho Mtakatifu ndiye anayepaswa kuwa na msukumo mkubwa wa kumbadili mdhambi kuyafuata mapenzi ya Mungu.)
        1. Je, hii inamaanisha kuwa hatuna wajibu wa kuwaelekeza na kuwafundisha Wakristo wapya? (Soma Mathayo 28:19-20. Kwa dhahiri tunao wajibu wa kufundisha na kuelekeza. Hata hivyo, utagundua kwamba hata katika Utume Mkuu wa Yesu, anatanguliza ubatizo kabla ya mafundisho.)
    5. Unadhani Naamani atakuwa na umuhimu gani katika kushuhudia siku zijazo? (Mfalme anavutiwa naye na watu wanampenda. Anaweza kuwa na athari kubwa chanya katika kuuendeleza Ufalme wa Mungu katika nchi ya Shamu.)
      1. Matokeo haya makubwa na yenye kupendeza yalianzaje? (Yalitokana na mwanamke kijana aliyekuwa mtumwa.)
        1. Endapo mwanamke huyu asingechukuliwa mateka, je, tungekuwa na matokeo haya ya kupendeza?
    6. Rafiki, nyakati ngumu zinaweza kutoa fursa ya kuuendeleza Ufalme wa Mungu kwa kiwango kikubwa. Je, utamwomba Roho Mtakatifu akufanye uwe makini na fursa hizi?
  5. Juma lijalo: Sakata la Yona.