Kuteseka kwa Ajili ya Kristo

Swahili
(1 Petro 4:12 - 19)
Year: 
2017
Quarter: 
2
Lesson Number: 
6

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Nani anayetaka kupata mateso? Hakuna mtu hata mmoja! Kuna mvutano mkubwa kwenye dhana mbalimbali katika kujadili mada ya Mkristo na mateso. Kwa upande mmoja Mungu anatupatia amri zake ili tuweze kuwa na maisha mazuri na ya yenye furaha. Kwa upande mwingine, Yesu aliteseka mikononi mwa Shetani. Ikiwa Bwana wetu aliteseka, basi hatupaswi kushangazwa na mateso. Tunazielewaje hizi dhana mbili zinazokinzana? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1. Manufaa ya Mateso

 

  1. Soma 1 Petro 1:6-7. Vifungu hivi vinasema kuwa manufaa ya mateso ni yapi? (Imani yetu inathibitishwa kuwa halisi, na tunampa Mungu utukufu.)

 

   1. Nilipokuwa ninakua, nilikuwa ninaelewa kwamba Mungu anaweka mateso kwenye mapito yetu ili kwamba imani yetu iweze kukua. Unadhani hiyo ni kweli?

 

  1. Soma Ayubu 1:8-12. Mojawapo ya mafunzo katika kitabu cha Ayubu ni kwamba wanadamu wana wakati mgumu sana kuelezea kwa nini mambo mabaya yanatokea. Matokeo yake, tunatakiwa tu kumtumaini Mungu. Nani aliye chanzo cha matatizo, anayesababisha madhara kwa Ayubu? (Shetani. Ndiye anayependekeza kumdhuru Ayubu.)

 

   1. Pitia uelewa wako wa kisa cha Ayubu katika 1 Petro 1:7. Nani aliyekuwa anatoa ubishani juu ya uhalisia wa imani ya Ayubu? (Shetani.)

 

   1. Je, Ayubu alihitaji changamoto hii kwa kadiri ya uelewa wa Mungu? (Si kwa mujibu wa Ayubu 1:1. Shetani ndiye aliyetoa ubishani juu ya imani ya Ayubu.)

 

   1. Nani aliyetukuzwa kutokana na uzoefu wa Ayubu? (Mungu alithibitishwa kuwa mkweli kuhusu Ayubu, na uongo wa Shetani ulidhihirishwa.)

 

  1. Una maoni gani kutokana na hii nadharia mbadala (Mbadala wa kile nilichokielewa nilipokuwa mdogo): 1) Shetani ndiye anayetutupia mateso maishani mwetu; 2) Shetani anafanya hivi kwa sababu anaamini tunamtumikia Mungu kwa sababu tu za ubinafsi; na 3) Tunapoendelea kuwa waaminifu tunaonesha kuwa Shetani hayuko sahihi na tunampa Mungu utukufu?

 

 1. Mvutano/Mgogoro

 

  1. Soma 1 Petro 4:12-14. Tunaambiwa kwamba mateso si jambo ambalo ni “geni.” Bali, ni jambo ambalo tunapaswa kulifurahia. Kwa nini mateso ni chanzo cha furaha? Mimi sitaki kupata mateso!

 

 

   1. Kwa nini Ayubu aliteseka? Kwa nini Yesu aliteseka? (Wote wawili walikuwa walengwa wa Shetani kwa sababu walikuwa wema. Yesu aliweka kiwango cha ubora kwa ajili ya wema. Furaha huja unapotambua kwamba umeteuliwa kwa sababu wewe ni mtu unayempa Mungu utukufu.)

 

  1. Soma 1 Petro 2:12 na usome tena 1 Petro 4:14. Hapa tunaona mateso ya aina gani yanayoelezewa? (Watu wanasema mambo mabaya kukuhusu na wanakukashifu.)

 

   1. Ninapoyafikiria mateso, ninafikiria juu ya mateso makali au ugonjwa wenye maumivu. Kimsingi hilo limewatokea Wakristo kwa miaka mingi, angalia Waebrania 11:36-38. Kuna hatari kuyafikiria mateso kwa namna ya ukali wa mateso pekee? (Ndiyo. Tunasahau ukweli kwamba tunapodhihakiwa, hiyo ni fursa ya kudhihirisha upendo wa Mungu.)

 

  1. Soma 1 Petro 4:15. “Mdukizi/mdakuzi” ni kitu gani? (Ni mtu anayejishughulisha na mambo ya watu wengine.)

 

   1. Je, unawafahamu Wakristo walio “wadakuzi?” Wale ambao wanadakua kwa sababu wanadhani kuwa Mungu anawataka wafanye hivyo?

 

  1. Angalia tena 1 Petro 4:15. Hii inadhihirishaje mgogoro uliopo kati ya dhana mbalimbali nilizozitaja kwenye utangulizi? (Nahisi Wakristo wengi wanapata mateso kwa sababu wanafanya maamuzi mabaya kuliko wale wanaoteseka kwa sababu ya maamuzi mazuri. Tatizo ni kwamba wale wanaoteseka kutokana na maamuzi mabaya wanataka kuyahusianisha mateso hayo na kuwa Wakristo.)

 

   1. Je, unapaswa kuwasahihisha watu wanaodai kimakosa kuwa wanateseka ikiwa ni matokeo ya matendo yao mema, wakati kiuhalisia ni kutokana na maamuzi yao mabaya? (Hili ndio lililokuwa jukumu la marafiki wanne wa Ayubu – kumshawishi kuwa alikuwa anateseka kwa sababu ya dhambi zake. Mungu aliwakemea marafiki watatu kwa kufanya hivi. Ayubu 42:7.)

 

   1. Je, kuteseka kutokana na maamuzi mabaya linaweza kuwa jambo zuri? (Bado unaweza kumpa Mungu utukufu kwa mjibizo (reaction) wako kwenye mateso.)

 

   1. Petro anabainisha sababu mbili za mateso – maamuzi yetu mabaya na maamuzi yetu mazuri. Je, kuna sababu nyingine zinazosababisha mateso? (Ndiyo. Dhambi zetu za jumla zinasababisha kuwepo kwa ulimwengu wa dhambi. Hii, pamoja na dhambi mahsusi na makosa ya watu wengine, inasababisha sababu ya tatu ya mateso. Ayubu anatufundisha kuwa makini juu ya kujaribu kubainisha sababu halisi za mateso.)

 

 1. Wakristo Wanateseka Kidogo

 

  1. Soma 1 Petro 4:17-18. Vifungu hivi vinatuambia kuwa nani anateseka zaidi: Wakristo au wasio Wakristo? (Hii inaashiria kwamba kuwa Mkristo ni njia ya kuelekea kwenye mateso kidogo.)

 

   1. Tafakari jambo hili kidogo. Je, hii inaashiria kuwa Mungu ndiye mwanzilishi wa mateso haya?

 

   1. Hebu turejee nyuma na tupitie habari za rafiki yetu Ayubu. Soma Ayubu 1:9-1 Je, Mungu angeweza kusema, “Hapana, sikubaliani na changamoto yako kwa Ayubu?” (Naam. Endapo Mungu angeweka “ukigo” Shetani asingekuwa na uwezo wowote juu ya Ayubu.)

 

 

   1. Vipi kama Ayubu asingekuwa mfuasi wa Mungu na asingekuwa na “ukigo wa Mungu pande zote?” Je, Shetani anapaswa kumwomba Mungu ruhusa ya kuwadhuru wale wanaoyatoa maisha yao kwa shughuli za Shetani?

 

  1. Soma Waebrania 11:32-35. Je, hii ni mifano ya mateso? (Nasema “ndiyo.”)

 

   1. Kuna jambo gani zuri juu ya mifano hii ya mateso? (Wote walishinda! Unapolitafakari jambo hili, Yesu na Yakobo walishinda. Badala ya kuyafikiria tu mateso kama “kushindwa” na nguvu za uovu, mateso yanajumuisha mapambano ambapo tunashinda! Wakati wa ujio wa Yesu Mara ya Pili, hatimaye tutashinda kila jaribio la mateso.)

 

  1. Hebu turejee kwenye 1 Petro 4:17. Petro hamtaji anayeleta hukumu katika 1 Petro 4:17, lakini maelezo juu ya mateso ya Ayubu yanambainisha Shetani kama mwanzilishi wa hii “hukumu.” Je, Mungu wetu pia ndiye anayeleta hukumu kwa wanadamu? (Soma Mwanzo 18:25-26, Zaburi 96:13, Yohana 5:22-23 na Matendo 17:31. Yesu ndiye atakayekuwa hakimu wa mwisho kwa wanadamu wote. Visa vya gharika na Sodoma na Gomora vinatuonesha kuwa Mungu pia anaingia kwenye hukumu dhidi ya waovu sasa hivi, lakini nadhani (bila msingi wa kisayansi kutetea hoja yangu) kwamba Shetani ndiye anayeleta mambo mengi mabaya yanayowatokea wanadamu.)

 

   1. Utaona kwamba nimekiita kile anachokifanya Shetani kuwa “hukumu.” Je, hilo ni kweli? (Ni sahihi zaidi kukiita kile anachokileta Shetani kama “majaribu,” na kile anachokileta Mungu kama “hukumu.” Mungu haleti mateso kwa watu, Yeye anatekeleza hukumu – kwa kutoa uamuzi kutokana na kuendelea kuwepo kwake.)

 

  1. Soma 1 Petro 4:19. Nimekuwa nikijenga hoja kwamba Shetani ndiye anayeleta majaribu. Kifungu hiki kinaonekana kusema kwamba watu wanateseka kutokana na mapenzi ya Mungu (“kwa mapenzi ya Mungu.”) Tunapaswa kuelewaje kifungu hiki?

 

   1. Palikuwepo na mateso Edeni? (Soma Ayubu 2:3. Mungu anamwambia Shetani kwamba hapakuwepo na sababu za msingi kumfanya Ayubu ateseke. Mungu hatati tuteseke. Petro anaposema “kwa mapenzi ya Mungu” anamaanisha kuwa Mungu ana uwezo juu ya kila kitu. Tunaweza kuwa na uhakika kwamba Mungu anadhibiti yale mambo mabaya yanayotujia.)

 

   1. Utaona kwamba katika 1 Petro 4:19 Petro anamwita Mungu “Muumba mwaminifu.” Kwa nini? (Anatilia mkazo [anaunga mkono] zaidi kwamba Mungu ni mwaminifu kwetu, hata pale tunapoteseka. Mungu alituumba na anatupenda!)

 

  1. Rafiki, ikiwa leo unapitia mateso, angalia vizuri sababu ya mateso hayo. Kama mateso hayo yanatokana na matendo yako ya haki, basi msifu Mungu na uyakubali kwa furaha kwa sababu unateseka kama Bwana wako. Ikiwa unateseka kutokana na maamuzi mabaya, basi mwombe Mungu akusaidie ili ujue nini cha kufanya ili kupunguza madhara na kuongeza zaidi namna unavyomshuhudia Mungu. Ikiwa huwezi kutambua sababu ya mateso yako, basi kisa cha Ayubu kinatufundisha tu kumwamini Mungu. Bila ya kujali sababu ya mateso yako, ikiwa utaendelea kuwa mwaminifu kwa Mungu, basi Mungu atayachukua mateso yote hayo atakapokuja tena!

 

 1. Juma lililopita: Uongozi wa Utumishi.