Somo la 4: Haki kwa Imani

(Warumi 3:1-9, 19-28)
Swahili
Year: 
2017
Quarter: 
4
Lesson Number: 
4

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, kuna mtu ambaye amewahi kutokukuheshimu? Je, umewahi kutowaheshimu watu wengine? Miaka mingi iliyopita, nilikuwa ninajaribu kusuluhisha tatizo moja gumu sana lililoibuka kati ya washiriki wa kanisa. Ilifikia mahala fulani mshiriki mmoja wa kanisa alinitusi. Najua hakumaanisha kwa kuwa alikuwa amefadhaika. Majuma machache baadaye, mshiriki huyo alinijia na kuniomba msamaha. Mwanzoni sikujua anazungumzia jambo gani kwa kuwa nilikuwa nimefutilia mbali suala lile kutoka mawazoni mwangu. Kwa upande mwingine, bado ninaweza kukumbuka matukio machache ambapo mtu fulani alidhamiria kunitukana. Kwa nini ninakuuliza juu la suala la heshima katika somo linalozungumzia haki kwa imani? Ni katika kusaidia kuyafungua mawazo yako kwenye dhana ya kwamba haki kwa imani sio tu kwamba inatupatia ufunguo wa kuingia kwenye uzima wa milele, bali pia ni katika jitihada za kubadili mtizamo wetu dhidi ya watu wengine. Hebu tujifunze zaidi juu ya jambo hili kwa kuzama kwenye somo letu la Warumi!

 

 1. Matatizo Yapaswayo Kuepukwa

 

  1. Soma Warumi 3:1-2. Majuma mawili yaliyopita tulijifunza kwamba Mataifa hawakuhitajika kutahiriwa. Hata kama haikuhitajika, kuna thamani yoyote katika kutahiriwa? (Ndiyo. Paulo anazungumzia kwa mahsusi manufaa ya kuwa Myahudi. Anasema kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu.)

 

   1. Wazo hili linakwenda mbali kiasi gani? Yote aliyoyaandika Musa yalitoka kwa Mungu. Je, kuna “manufaa” kufuata vipengele vingine vya sheria ya Kilawi?

 

  1. Soma Warumi 3:3-4. Vipi kama wale waliokabidhiwa mausia ya Mungu si waaminifu? Umewahi kumsikia mtu akimlaumu Mungu kwa matatizo yanayomkabili maishani? (Paulo anasema kuwa Mungu ni mwaminifu. Ikiwa tunadhani kuwa ahadi za Mungu zinanyumbulishwa, basi matatizo ya kushindwa kuendana nazo yapo mahala pengine na kushindwa huko hakutokani na Mungu.)
    
   1. Je, wale ambao hapo awali waliwahi kubarikiwa bado wanafurahia manufaa ya kubarikiwa? Je, bado wao ni chanzo cha mamlaka? (Ukweli kwamba wale waliobarikiwa na Mungu wanasita katika imani yao haibatilishi uaminifu wa Mungu. Tunapaswa kuchukua maelekezo kutoka kwa Mungu, na si kwa wanadamu.)

 

  1. Soma Warumi 3:5-8. Je, tunaweza kumpa Mungu utukufu kwa kuwa waovu?

 

   1. Kundi hili linajenga hoja gani ambayo Paulo anaikataa? (Kundi hili linasema kuwa ikiwa lengo ni kumpa Mungu utukufu, basi tabia yangu mbaya inauelezea wema wa Mungu.)

 

   1. Hii inaashiria nini kwa wale wanaofundisha kwamba haki kwa imani inamaanisha kuwa tunapaswa kuipuuza sheria? (Mungu bado anayajali matendo yetu.)

 

  1. Umegundua hoja mbili ambazo Paulo amezikataa? Nadhani ni muhimu kuzielewa kabla hatujaingia kwenye kauli za Paulo kuhusu haki kwa imani. Unaweza kuhitimishaje kwa usahihi kwa kutumia maneno yako mwenyewe? (1. Mara zote Mungu ni mwaminifu. Bila kujali kama tunajaribu kuelezea kwa nini jambo baya limetokea, au tunajaribu kuangalia nani aliye kiongozi mzuri wa kiroho, tunatakiwa kuweka tumaini letu kwa Yesu kwanza. 2. Njia ya kumpa Mungu utukufu ni kwa kumtii Yeye, si kwa kuonesha inamaanisha nini kuishi maisha yasiyo ya haki.)

 

  1. Soma Warumi 3:9. Vipi kama utaepuka huu uelewa wa uongo wa aina mbili, vipi kama utaelewa na kuufuata ukweli, je, wewe ni bora zaidi kuliko wale wasioelewa? (Hapana! Unaweza kuwa sahihi, lakini bado wewe ni mdhambi kwa sababu nyinginezo!)

 

 1. Sheria

 

  1. Hebu turuke hadi chini na tusome Warumi 3:19. Lengo la torati ni lipi? (Kutufanya tufumbe vinywa vyetu! Unakumbuka somo la juma lililopita lilikuwa na onyo kali kuhusu kuwa wahukumu?)

 

   1. Angalia lugha ya ajabu hapa. Paulo anasema kuwa torati huyanena inenayo “kwa hao walio chini ya torati.” Je, hiyo inaashiria kuwa baadhi hawako “chini ya sheria?”

 

   1. Ikiwa umejibu, “ndiyo,” unaelezeaje kinachofuatia Paulo anapoandika kuwa “ili kila kinywa” kifumbwe na “ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu?” Ikiwa torati inahusika kwa baadhi ya watu tu, kwa nini vinywa vyote vifumbwe na kila mtu awe chini ya hukumu ya Mungu? (Lazima Paulo atakuwa anamaanisha kuwa msimamo wa dhahiri kwa kila mtu ni kwamba sote tuko chini ya sheria.)

 

  1. Soma Warumi 3:20. Je, sheria ndio jibu kwa dhambi zetu? (Hapana. “Hakuna hata mmoja” atakayehesabiwa haki kwa “kuishika sheria.” Badala yake, sheria inatujuza kile ambacho Mungu anataka tukiepuke.)

 

  1. Ikiwa nitakomea hapa na kuuliza, “Tafakari kile tulichokijadili hadi kufikia hapa. Je, utasema kuwa bado sheria ina maana?” Utajibuje? (Jibu linatakiwa kuwa “ndiyo.” Sheria inatuonesha jinsi ya kumpa Mungu utukufu. Sheria inatuonesha njia bora ya namna ya kuishi.)

 

 1. Haki kwa Imani

 

  1. Soma Warumi 3:21. Je, kuna njia ya sisi kuwa na haki tofauti na kuishika sheria? (Ndiyo.)

 

   1. Tunajuaje kuwa hii ni kweli? Je, tunatakiwa tu kuyachukulia maneno ya Paulo kama yalivyo? (Paulo anaandika kuwa “torati na Manabii vinashuhudia” njia hii ya kupata sehemu ya haki kwa kuishika sheria.)

 

    1. Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Manabii walizungumzia ujio wa Masihi. Huduma ya patakatifu iliashiria kafara ya Yesu ijayo. Kushindwa kwetu kuishika sheria kunatuonesha kuwa tunahitaji njia bora zaidi.)

 

  1. Soma Warumi 3:22-24. Njia hii mpya ya kuhesabiwa haki iliyo “tofauti” na kuishika sheria ni ipi? (“Imani katika Yesu.”)

 

   1. Nani awezaye kuchukulia ofa ya fursa hii? (“Wote waaminio.”)

 

   1. Je, Mungu anajaribu kuwapunguza wale wanaoweza kuichukulia ofa ya fursa hii? (Hapana. “Tunahesabiwa haki bure.”)

 

   1. Je, kila mtu lazima achukulie fursa ya ofa hii ikiwa anatamani uzima wa milele? (“Wote wametenda dhambi.” Maoni ya kutokuwepo na “tofauti” inatuhabarisha kuwa hata kama tunadhani kwamba sisi ni wema kwa kiwango gani, uwepo wa dhambi maishani mwetu unamaanisha kwamba bado tunakufa isipokuwa tu kama tutaipokea ofa ya Yesu.)

 

   1. Hii inaashiria nini kuhusu kutowaheshimu watu wengine? Hii inaashiria nini juu ya mtazamo wa kujiona wa hadhi ya juu kutokana na utii wetu?

 

  1. Soma Warumi 3:25-26. Maneno “imani katika damu yake” yanaonekana kuwa ya ajabu. Hii inamaanisha nini? (Hii inatukumbusha huduma ya patakatifu ambapo mnyama alitolewa kafara ili kupatanisha (kuondoa) dhambi za mtu aliyemtoa mnyama huo. Damu ndio iliyoondoa dhambi. Angalia Waebrania 9:22 na Ezekieli 43:20. Hii inatuambia kuwa kafara iliyotolewa hekaluni (patakatifu) ilikuwa ni mfano kuwafanya watu wa Mungu waelewe kwamba Yesu alikuwa anakuja kuzichukua dhambi zao.)

 

   1. Vifungu hivi vinasema kuwa hii “inadhihirisha” haki ya Mungu. Unaelezeaje kwamba hii ni haki? (Soma Mwanzo 2:16-17. Ninaamini kwamba kuingia kwa dhambi moja kwa moja kulileta kifo. Ni sheria ya asili na Mungu alimuonya Adamu kuihusu. Yesu alipokufa kwa ajili ya dhambi zetu, kiasi cha kutufanya kuwa na fursa ya kuingia kwenye ulimwengu usio na dhambi kwa mara nyingine tena, ilituonesha kuwa haki ya Mungu hailinganishwi na kitu chochote tulichowahi kukiona kabla.)

 

  1. Soma Warumi 3:27. Unadhani kwamba wewe ni mtu mwema sana? Je, watu wengi unaowafahamu wana viwango vya chini kuliko vyako? Paulo anazungumzia nini juu ya mtazamo kama huu? (“Haujumuishwi.” Hatuna cha kujivunia kwa kuwa haki kwa imani ni zawadi ya bure.)

 

  1. Soma Warumi 3:28. Sheria ina wajibu gani katika wokovu wetu? (Haina wajibu wowote. Watu pekee wanaohesabiwa haki, ni wale wanaofanya hivyo kwa msingi wa imani katika kafara ya Yesu kwa ajili (niaba) yao. Sheria haihusiani na wokovu kivyovyote vile.)

 

  1. Rafiki, je, mtazamo wako kwa watu wengine unaakisi kikamilifu ukweli wa haki kwa imani? Sisi sote ni wadhambi. Wote tunayo njia moja tu ya kuweza kuokolewa milele, na haihusiani kivyovyote vile na matendo yetu wenyewe. Mungu apewe sifa kwa kile alichotutendea!

 

 1. Juma lijalo: Imani ya Ibrahimu.