Somo la 10: Watoto wa Ahadi

(Warumi 8:31-Warumi 9:31)
Swahili
Year: 
2017
Quarter: 
4
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, unao marafiki au ndugu wanaoyafanya maisha yako yawe magumu kwa makusudi? Je, pia wameikataa imani yako? Unajisikiaje juu yao? Unataka waokolewe na waache kujaribu kukuumiza? Hivi ndivyo Paulo anavyojisikia kuhusu Wayahudi. Anataka waokolewe – na itakuwa vyema ikiwa wataacha kujaribu kumuumiza! Hebu tuzame kwenye somo letu la Warumi 9 ili tujifunze kwa kina jinsi ya kukabiliana na marafiki na ndugu ambao kuna nyakati wanaonekana kuwa maadui.

 

 1. Faraja

 

  1. Soma Warumi 8:31. Tunafahamu kwamba Shetani yu kinyume na wale wanaomfuata Yesu. Yumkini wapo watu maishani mwako walio “kinyume” nawe. Unakielewaje kifungu hiki? (Tunaweza kuwa na wapinzani, lakini anachokimaanisha Paulo ni kwamba ni vigumu kwa watu hao kuushinda uwezo wa Mungu.)

 

  1. Soma Warumi 8:32. Tunawezaje kuwa na uhakika kwamba Mungu yuko upande wetu? Kwamba yu radhi kutusaidia dhidi ya maadui zetu? (Alimtoa Mwanaye kwa ajili yetu. Atende jambo gani jingine zaidi ya hilo kutuonesha upendo wake na anavyotujali?)

 

   1. Tunaposema kwamba Mungu yu “upande wetu,” je, hiyo inamaanisha kuwa atatenda kile tunachodhani kuwa ni bora? (Ikiwa tuna mantiki yoyote, tunataka Mungu atende kile anachodhani kuwa ni bora.)

 

  1. Soma Warumi 8:33-34. Yesu ana wajibu gani mbinguni kwa sasa? (Anatuombea! Hii inatukumbusha kitabu cha Waebrania kinachotuambia kuwa Yesu ni Kuhani wetu Mkuu katika hekalu la mbinguni akituombea.)

 

  1. Soma Warumi 8:35-39. Mjadala huu unakufanya ujisikieje? (Unapaswa kutupatia faraja kuu na ujasiri mkubwa. Mungu yu pamoja nasi, Mungu anatupenda, na mtu “anayetuhukumu” anatuombea! Sisi ni “zaidi ya washindi!”)

 

   1. Unapovitafakari vifungu hivi, je, unaona kwamba mara zote maisha ya Mkristo ni marahisi? (Hii inazungumzia mambo mengi mabaya ambayo hayatatutenga na upendo wa Mungu – hivyo kuashiria kwamba wale wanaopendwa na Mungu wanaweza kukabiliana na matatizo makubwa sana maishani.)

 

 1. Uchungu/Maumivu

 

  1. Soma Warumi 9:1-5. Baada ya kuandika kwamba sisi ni zaidi ya washindi, Paulo anawezaje kusema kwamba ana “huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma?” (Ahadi hizi za pekee, hii faraja kuu, kwa kiasi kikubwa imekataliwa na watu wake, Wayahudi. Wamekataa wazo la kwamba Yesu alikufa kwa ajili yao na anawaombea.)

 

  1. Soma Warumi 9:6. Kwa nini Paulo ajisikie hitaji la kutetea ahadi za Mungu? (Zingatia jambo la wazi, Mungu alitoa baraka zake za pekee na akayadhihirisha mapenzi yake mahsusi kwa Wayahudi – ambao baadaye walimkataa Yesu.)

 

   1. Paulo anamaanisha nini anapoandika “hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli?” (Soma Warumi 9:7-9. Israeli haihesabiwi kuwa Israeli kwa asili (mbari). Badala yake, inahesabiwa (inatambuliwa) kutokana na wale wanaojitoa na kupokea ahadi za Mungu. Ukipokea na kukubali ahadi ya Mungu, basi wewe ni Israeli.)

 

 1. Uchaguzi

 

  1. Soma Warumi 9:10-14. Unadhani hii inamaanisha nini kuhusu uwezo wa Esau kuokolewa? Je, Mungu “alimchukia” kabla hajazaliwa? (Ni vigumu kukubali kwamba hicho ndicho anachokimaanisha Paulo. Kwa nini Paulo anaonesha huzuni nyingi na maumivu (Warumi 9:2) ikiwa Mungu amefanya uamuzi mkubwa kwamba Wayahudi wengi watamkataa? Unaelezeaje mwelekeo wa Warumi hadi kufikia hapa, kwamba neema ni suala la wanadamu kuikubali? Unaelezeaje Warumi 5:18 inayosema kuwa kwa tendo moja la haki la Yesu “watu wote walihesabiwa haki ya uzima?”)

 

  1. Soma Warumi 9:15-18. Je, unadhani kuwa Mungu amekurehemu? Au, je, ameufanya mgumu moyo wako?

 

  1. Soma Warumi 9:19. Je, hili si ndilo swali letu? Je, hili sio swali la dhahiri kuhusu utendaji haki wa Mungu?

 

  1. Soma Warumi 9:20-21. Unalichukuliaje jibu la Paulo? (Kwa dhahiri liko sahihi, lakini si la kufariji. Kwanza Paulo anatuambia tufumbe vinvya vyetu (tunyamaze kimya). Kisha anasema kwamba kwa dhahiri Mungu anayo haya mamlaka. Alituumba. Kwa dhahiri anakubaliana na swali la mamlaka.)

 

   1. Je, kuwa kwenye mamlaka na kutenda haki ni jambo moja (yaani, vinafanana)?

 

    1. Au, je, ukweli kwamba Mungu alituumba ndio jibu la swali la utendaji haki?

 

   1. Hebu turejee kule tulikoanzaia. Soma tena Warumi 8:3 Hii inaendanaje na wazo la Mungu dikteta?

 

  1. Soma tena Warumi 9:3-5. Hebu tutafakari upya kinachochaguliwa na kuteuliwa. Je, kwa asili hapo awali uliteuliwa ikiwa wewe si Myahudi? (Hapana. Tukirejea mwanzoni mwa mazungumzo ya Paulo, tunaona kwamba hazungumzii wokovu, badala yake anazungumzia chombo cha wokovu. Mungu alimchagua Ibrahimu, alimchagua Isaka na aliwachagua Wayahudi kuwa wawakilishi wake wa pekee. Alimchagua Farao ili kudhihirisha uwezo wake wa kuokoa.)

 

   1. Je, hii inamaanisha kuwa Wayahudi wanaokolewa na sisi (mataifa) hatuokolewi? (Kwa dhahiri hapana! Hiki ndicho anachokimaanisha Paulo katika Warumi 9:6-8. Tunaokolewa hata kama kwa asili hatukuchaguliwa. Esau na Farao wangeweza kuokolewa.)

 

 

   1. Matendo yako yana umuhimu gani kwenye wokovu wako? (Je, huyu ni tembo chumbani? Wokovu na rehema vyote ni vya Mungu. Tunadhani matendo yetu ni ya muhimu sana. Upumbavu kiasi gani.)

 

   1. Bado unasumbuliwa na wazo kwamba Mungu anaweza kukuchagua (kama ilivyokuwa kwa Farao) kudhihirisha uwezo wako? Hebu tuchunguze jambo hilo zaidi katika sehemu inayofuata.

 

 1. Rehema

 

  1. Soma Warumi 9:22. Tunastahili nini? (Dhambi zetu zinatufanya tustahili mauti ya milele.)

 

   1. Ukitumia suluhisho hilo kuwa ndio muktadha, tunaweza kuona kwamba Mungu amewaonesha rehema kubwa wanadamu, hata wale waliomkataa. Hii ndio sababu Farao, na wale wanaofanana naye, hawana vigezo vya kulalamika. Tunachostahili sote ni kifo. Mungu ametupatia sote karama ya fursa ya uzima wa milele!)

 

  1. Soma Warumi 9:23-26. Kuna habari gani njema kubwa kwa ajili yetu? (Kwamba sasa sisi ni watu wa Mungu. Habari za Esau na Farao zinaelezea rehema ya Mungu. Hata wale ambao kwa asili hawakuchaguliwa wanaweza kufurahia baraka za kuwa “wana wa Mungu aliye hai.”)

 

  1. Soma Warumi 9:27-28. Paulo anaelezea tabia/sifa gani nyingine ya Mungu, tofauti na rehema? (Mungu pia ni Hakimu atakayetoa hukumu juu ya wale wanaomkataa. Atafanya hivyo “kwa haraka, akilimaliza na kulikata.”)

 

   1. Matumizi ya neno “kulikata” yanaashiria nini kuhusu dhana ya mwanadamu mpotevu katika jehanamu iwakayo/iunguayo milele? (Iunguayo milele haionekani kuwa hatima ya mwisho kabisa.)

 

  1. Soma Warumi 9:29. Hii inaashiria nini kuhusu dhana ya jehanamu iunguayo milele? (Kwa kuwa Sodoma na Gomora haziungui leo, inaashiria kuwa jehanamu inawala wale wanaomkataa Mungu. Kutokana na hoja kwamba tunaye Mungu wa rehema, wapotevu hawana maisha ya milele ya mateso.)

 

  1. Soma Warumi 9:30-32. Kwa nini watu wanazingatia haki kwa njia ya matendo? (Kwa sababu walidhani kuwa waliweza kufanya vizuri kuliko watu wengine. Mataifa, ambao Wayahudi waliwadhania kuwa ni wadhaifu, walipata haki!)

 

  1. Soma Warumi 9:33. Jiwe ni nani katika Sayuni? (Yesu!)

 

   1. Mungu anatuita tufanye nini linapokuja suala la Yesu? (Kumtumaini. Tukifanya hivyo, kamwe hatutafedheheshwa.)

 

    1. Vipi ikiwa hatumtumaini? (Basi “tutajikwaa” maishani na kuukosa uzima wa milele.)

 

    1. Je, unapenda amani na furaha? Je, ungependa kuepuka fedheha? Kumpokea Yesu kama Mwokozi wako ndio njia ya kupata hizo baraka!

 

 

  1. Rafiki, kumbuka kwamba tulianza somo hili kwa kuwazungumzia marafiki na ndugu wanaotuumiza. Tumemalizia na ahadi ya kwamba tukimpokea Yesu kama mwenye haki wetu, kamwe hatutafedheheshwa. Mungu huwapa ushindi wale wanaomtumaini. Kama ungependa kuwa mshindi, kwa nini usimkiri na kumpokea Yesu kwa imani ili uwe sehemu ya familia ya Mungu?

 

 1. Juma lijalo: Wateule.