Uumbaji na Anguko

(Mwanzo 1-3 & 11)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
4
Lesson Number: 
1

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Umoja linaonekana kuwa neno lililopoteza umaarufu. Uanuwai ndilo neno maarufu siku hizi. Kama yalivyo mambo mengi yanayoendelea sasa hivi, ni dhana iliyopindua juu-chini fikra iliyozoeleka. Kaulimbiu ya Marekani inasema “Kati ya watu wengi, tu wamoja.” Uanuai unapaswa kujielekeza kwenye umoja kwa mujibu wa hii kaulimbiu, na si vinginevyo. Je, hii dhana iliyozoeleka pia ni dhana na Kibiblia? Je, Mungu anatamani tuunganishwe au tuwe na uanuwai? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuweze kufanya uvumbuzi!

 

 1.    Asili Iliyoumbwa

 

  1.    Soma Mwanzo 1:26. Ni kwa namna gani tatu tunafanana na Mungu? (Sisi ni watawala, tuna “sura” na “mfanano” wa aina moja.)

 

   1.    Kuna tofauti gani kati ya sura na mfano? (Tuna mfumo mmoja wa msingi kama wa Mungu, na tunafanana naye kwa namna nyinginezo. Lazima kuwa watawala ni mojawapo ya namna hizo.)

 

   1.    Nadhani kiburi kinaongoza nadharia ya uibukaji kwa kiasi kikubwa. Je, kuna nafasi ya majivuno kwenye maelezo ya uumbaji? (Tuliumbwa ili tuwe watawala! Tofauti ni kwamba tulipewa haya mamlaka na Mungu, jambo ambalo kwa dhahiri linamfanya Mungu awe mkubwa kwetu.)

 

  1.    Soma Mwanzo 1:27. Mungu alitenda kile alichopendekeza. Kwa nini anawapa wanadamu mamlaka makubwa kiasi hicho?

 

  1.    Soma 1 Yohana 4:7-10. Yohana anaashiria kuwa sababu ya Mungu kuwapa wanadamu mamlaka hayo ni ipi? (Kwa sababu alitupenda.)

 

   1.    Kama hiyo ndio sababu, kwa nini Mungu hakutoa mamlaka haya kwa wanyama wote aliowaumba? Je, Mungu aliwapenda kwa kiwango kidogo? (Soma Mwanzo 1:28. Hii inaelezea dhana ya mamlaka na umoja. Kuwa mtawala inamaanisha kuwa unacho kitu cha kukiongoza. Mungu alitufanya kuwa watawala wa wanyama. Lakini, yeye ni mtawala wetu.)

 

    1.    Kwa nini mamlaka ni ya muhimu kwenye dhana ya umoja? (Kama kila mtu anafanya kile anachokitaka, basi “umoja” pekee tulionao ni umoja wa machafuko. Ukweli kwamba Mungu anawapenda wanadamu na wanyama, lakini akatupatia mamlaka juu yao, inaonesha kuwa asili ya utaratibu na mamlaka vinaakisi upendo.)

 

  1.    Soma Mwanzo 3:1-5. Je, utii wa mamlaka ungejibuje changamoto aliyokabiliana nayo Eva? (Nyoka Shetani alitia changamoto mamlaka ya Mungu moja kwa moja.)

 

   1.    Asili ya changamoto hiyo ikoje? (Eva atakuwa na mamlaka kama ya Mungu – kwa kuyajua mema na mabaya.)

 

   1.    Je, Eva angeweza tu kujibu kuwa “Mungu ana mamlaka juu yangu, hivyo nitamnwamini yeye na si wewe?” Je, jibu hili lina mantiki kwa kuwa Eva hakumjua nyoka na alikuwa anasema kuwa Mungu ni mwongo? (Kutii mamlaka kungemwokoa Eva. Lilikuwa jibu sahihi na lenye mantiki.)

 

  1.    Soma Mwanzo 3:9-12. Nini kimetokea kwenye umoja kati ya Adamu na Eva?

 

   1.    Nini kimetokea kwenye utii wa Adamu kwa mamlaka ya Mungu? (Jibu la Adamu linamshutumu Mungu kwa kusema kuwa Mungu amemweka Eva bustanini.)

 

  1.    Soma Mwanzo 4:3-8. Hatua ya kwanza kwenye dhambi ya Kaini ni ipi? (Hakufuata mamlaka ya Mungu alipochagua sadaka yake.)

 

   1.    Uasi huu dhidi ya Mungu ulisababisha jambo gani? (Kumwua ndugu yake. Hiki ni kitendo cha juu kabisa cha kutokuwa na umoja.)

 

  1.    Je, hapa tunaona mwelekeo? Mamlaka na umoja vinahusianishwaje? (Katika mambo yote mawili tunaona kwamba kuyakataa mamlaka ya Mungu husababisha matendo mabaya ya kutokuwa na umoja.)

 

   1.    Je, dhana ya kisasa ya uanuwai pia ni kuyakataa mamlaka? Au, je, hilo ni jambo tofauti?

 

 1.   Babeli

 

  1.    Soma Mwanzo 11:1-4. Je, wanadamu wanautafuta umoja? (Ndiyo. Wanasema kuwa hawataki kutawanyika.)

 

   1.    Kwa nini wanajenga mnara “unaofika mbinguni?” (Soma Mwanzo 9:8-11. Wanataka kuwa na umoja pasipo kuyakubali mamlaka ya Mungu. Hawaiamini ahadi ya Mungu ya kamwe kutokuleta gharika tena duniani. Hivyo, wanajitegemea wao wenyewe kujenga mnara utakaoinuka juu kuliko gharika yoyote inayoweza kujitokeza siku zijazo. Kwa kufanya hivyo itawafanya wawe maarufu.)

 

  1.    Soma Mwanzo 11:5-9. Je, Mungu yu kinyume na umoja? (Mungu anasimama dhidi ya upinzani mmoja wa mamlaka yake.)

 

   1.    Hii inazungumzia nini kuhusu dhana ya umoja dhahania? (Umoja si thamani chanya kwa umoja wenyewe. Umoja huleta nguvu na mamlaka zaidi, lakini lengo la Mkristo ni kuwa na umoja chini ya mamlaka ya Mungu.)

 

   1.    Je, hii inaonesha kuwa Mungu ni Baba wa uanuwai? (Hapa tunaona kuwa uanuwai ni jaribio ya kuingilia mafanikio ya mwanadamu. Mungu anasema kuwa “hakuna kitakachowashinda watu wamoja wanaozungumza lugha moja.”)

 

 1. Kuujenga Upya Umoja

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 7:6. Je, Mungu amebadili mbinu? Je, hauhangaikii tena umoja? (Ni sahihi zaidi kusema kuwa tuliukataa umoja aliokuwa anauwazia Mungu tulipomkataa yeye. Mungu alipunguza kasi upinzani wa pamoja dhidi yake pale Babeli. Kisha Mungu aliwachagua watu maalumu kutenda kazi yake.)

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 7:7-8. Kwa nini Mungu aliwachagua Wayahudi kuwa watu wake wa kipekee (maalumu)? (Kifungu kinazungumzia ahadi zilizotolewa kwa “babu zao.” Hii ni rejea ya Mwanzo 12 tulipojifunza kuw Mungu alimchagua Ibrahimu kuwa baba wa taifa kubwa. Kifungu kinasema kuwa Mungu “aliwapenda” watu wake maalumu.)

 

  1.    Soma Warumi 4:3. Kuna jambo gani la kipekee kwa Ibrahimu? (Alimwamini Mungu. Hii ni kinyume na Hawa, ambaye hakumwamini Mungu.)

 

   1.    Unapovitafakari vifungu hivi, nini kinaonekana kuwa mpango wa Mungu kurejea kwenye umoja wa Edeni? (Bado Mungu anatupenda! Dunia inapoonekana kuungana dhidi ya Mungu, anamchagua mtu anayemwamini Mungu, na kumtumia mtu huyo kuanza kujenga taifa kubwa ambalo lengo lake ni kuuleta tena ulimwengu pamoja kwenye umoja chini ya bendera ya Mungu.)

 

 1.   Vipengele Vingine vya Umoja Kutoka Edeni

 

  1.    Soma Mwanzo 2:2-3 na Kutoka 20:8-11. Sabato ilichangiaje mpango wa asili wa Mungu kwa ajili ya umoja? (Siku ya pumziko kwa kuacha kufanya kazi ili kumtafakari Mungu Muumbaji wetu ni kigezo kikubwa kwenye kuutangaza umoja katika kumuunga Mungu mkono. Hii ni siku ya familia yote, kwa sababu hakuna mtu hata mmoja, wala wanyama, wanaotakiwa kufanya kazi.)

 

  1.    Soma Mwanzo 2:22-24. Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke inawezaje kukuza umoja? (Rejea ya “mwili mmoja” inazungumzia ubunifu wa mwanamume na mwanamke ili kuwafanya kwa pamoja wawe waumbaji wa uhai mpya unaowaakisi wote wawili. Ndoa na familia ni zana nyingine ya umoja chini ya mamlaka ya Mungu.)

 

  1.    Unapoutafakari ulimwengu leo, je, umoja chini ya mpango wa Mungu unakua, au uko chini ya shambulizi?

 

  1.    Rafiki, yatafakari maisha yako. Je, unaujenga umoja chini ya bendera ya Mungu, au wewe ni nguvu inayotumika kuwagawa watu (uanuwai)? Kama unampinga Mungu, kwa nini usitubu na kumwomba Roho Mtakatifu akusaidie kuutangaza umoja katika Yesu?

 

 1.    Somo lijalo: Vyanzo vya Kutokuwa na Umoja.