Somo la 7: Migogoro Inapoibuka

Swahili
(Matendo 6, 10 & 11)
Year: 
2018
Quarter: 
4
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, Unafanana na mimi? Umewahi kuwa kwenye kanisa lililo na migogoro, na pia kuwa kwenye kanisa lililo na umoja? Jambo gani lilileta tofauti kati ya makanisa hayo? Mara ya kwanza nilipooa kanisa letu liligawanyika kutokana na masuala ya kiteolojia. Kwa namna mbalimbali hilo lilikuwa jambo jema kwa sababu mgogoro ulihusu habari ya neema. Ilikuwa vyema kwa washiriki wa kanisa kupata nafasi ya kutafakari jambo hilo kwa umakini. Kanisa letu lililofuatia liligawanyika kutokana na masuala ya kimbari (ubaguzi). Hapakuwepo na kisingizio chochote kwa mgogoro huo. Kanisa langu la sasa lina umoja na kanisa langu kabla ya kujiunga na kanisa hili kwa kiasi kikubwa halikuwa na mgogoro. Biblia inaandika migogoro kadhaa katika kanisa la awali. Hebu tuiangalie migogoro hiyo ili tuone kile tunachoweza kujifunza katika kutatua mgogoro ndani ya kanisa!

 

 1. Chakula

 

  1. Soma Matendo 6:1. Msingi wa mgogoro ni upi? (Inaonekana mgogoro unatokana na utamaduni. Wote ni Wayahudi, lakini wengine wana asili ya Uyunani na wengine wana asili ya Uebrania.)

 

   1. Je, Wakristo wanazuia chakula kutokana na asili ya utamaduni wa mjane? (Hilo ni shtaka kubwa sana. Maelezo yasiyo na hatia ni kwamba Wayahudi wa Kiebrania waliwafahamu wajane wao vizuri sana, na hivyo inawezekana huku kulikuwa ni kupitiwa tu. Utaona kwamba kifungu kinasema, “hata wanafunzi walipokuwa wakiongezeka.” Hiyo inaashiria matatizo halisi.)

 

  1. Soma Matendo 6:2-4. Wanafunzi kumi na wawili walitatuaje tatizo hili? (Walilihamishia kwa wengine! Walihamishia tatizo kwenye kamati ya watu saba, na waliwasilisha chaguo la wanakamati kwa wengine.)

 

   1. Unadhani hili ni wazo zuri? Kama ndivyo, kwa nini? Kama sivyo, kwa nini?

 

   1. Utaona kwamba wanafunzi wanaizungumzia kazi kama “kuhudumu mezani.” Je, wanafunzi wanasema kuwa kazi hii haiendani na hadhi yao?

 

   1. Vigezo vya kufanya kazi hii ni vipi? (Kujawa na Roho Mtakatifu na hekima.)

 

    1. Vigezo hivi vinaendanaje na kazi ya “kuhudumu mezani?” (Kwa dhahiri haviendani. Changamoto halisi kwenye kazi hii ni kutatua madai ya upendeleo wa kiutamaduni. Hiyo itamhitaji Roho Mtakatifu na hekim)

 

 

   1. Tukiangalia vifungu hivi kwa muktadha wa usasa wetu, tunaweza kuhitimisha kwamba wanafunzi hawakutaka kukabiliana na tatizo lililo chini ya hadhi yao. Je, kuna lolote kwenye vifungu hivi kuashiria kwamba huo haukuwa mtazamo wa wanafunzi? (Kifungu cha 2 kinatuambia wanafunzi “wote” walikutana pamoja ili kutatua tatizo hili. Hilo linafanya ionekane kwamba wale wanafunzi kumi na wawili walilitambua suala hili kuwa ni la msingi. Rejea ya “kuhudumu mezani” inaweza kuwa njia ya mwisho kabisa ya kutofautisha kazi ya utume ya wanafunzi, badala ya maoni juu ya hadhi ya kazi.)

 

  1. Soma Matendo 6:5-6. Inaweza isiwe dhahiri kwetu sote, lakini hawa wanakamati saba wote kati ya wajumbe wa kamati wana majina yanayoonekana kuwa ni ya Kiyunani. Utakumbuka kwamba wajane wa Kiyunani walikuwa wanalalamika kwamba walikuwa hawapati sehemu stahiki ya chakula, badala yake wajane wa Kiyahudi walikuwa wanapendelewa. Kanisani kwako kundi kubwa limetawaliwa na watu gani? Kanisani kwako ni kundi gani kubwa lililo na watu wachache? Tumia suluhisho hili kwa kutumia makundi hayo. Kundi la watu wachache wanaolalamika sasa linapewa mamlaka ya kutatua tatizo!

 

   1. Je, hii itasababisha tatizo la ubaguzi libadilishiwe kwenye kundi jingine? (Usisahau kwamba vigezo vya uchaguzi vilikuwa ni kujawa Roho Mtakatifu na kuwa na hekima.)

 

   1. Utakumbuka kwamba sababu isiyo na hatia kwa ajili ya ubaguzi ni kwamba katika kanisa lililokuwa linakua kwa kasi Wayahudi wa Kiebrania waliwajua wajane wao vizuri zaidi. Suluhisho hili lingetatuaje tatizo hilo? (Kama kweli tatizo linaibuka kutokana na kutokuwepo kwa hekima, basi kuwaleta Wayunani wanaowafahamu wajane wao vizuri zaidi ni suluhisho maridhawa, na haliibui masuala ya ubaguzi wa awali au kuugeuzia kwenye kundi jingine.)

 

 1. Ulaji

 

  1. Soma Matendo 10:1-2. Je, Kornelio ni mtu mwema?

 

   1. Je, ni mtu mwenye nguvu na ushawishi?

 

  1. Soma Matendo 10:3-4. Kwa nini askari awe na hofu kwenye haya maono ya malaika? (Hili ni jambo lisilo la kawaida. Kornelio anaweza kuwa na ufahamu wa hofu za vita, lakini hakuzoea kukabiliana na malaika.)

 

  1. Soma Matendo 10:5-8. Unadhani kwa nini malaika aliwaruhusu watu wa Kornelio waende badala ya Kornelio kwenda yeye binafsi?

 

  1. Soma Matendo 10:9-13. Ni mara ngapi unaota juu ya chakula? Utaona kwamba visa vyetu vyote viwili vya Biblia juma hili vinahusiana na chakula!

 

  1. Soma Matendo 10:14-16. Petro anaamini mzubao huu unatoka kwa Mungu. Je, Mungu atakinzana na kile alichotuambia kwenye Biblia? (Kwa nguvu zote kabisa nasema, “Hapana.” Lakini, kumbuka somo letu la hivi karibuni juu ya Kitabu cha Matendo, na kwa mahsusi maelezo ya Matendo 15 jinsi kanisa la awali lilivyotatua suala la tohara. Somo hilo linafanya jibu hili kuwa na utata zaidi.)

 

 

  1. Soma Matendo 10:17. Je, maana ya maono si bayana? (Lingekuwa bayana endapo Petro asingekuwa anafahamu Biblia inachokisema (Mambo ya Walawi 11) juu ya kula wanyama najisi. Petro alihitimisha kwamba maana ya dhahiri haikuwa juu ya kile ambacho kimsingi maono yalikimaanisha, kwa sababu kingekinzana na Biblia.)

 

  1. Soma Matendo 10:18-20. Roho Mtakatifu anamwambia Petro afuatane na wale watu waliotumwa na Kornelio. Kwa nini hili linaweza kuwa tatizo? (Soma Matendo 10:25-29. Ilikuwa ni kinyume cha sheria ya Kiyahudi kwa Myahudi kumtembelea mtu wa Mataifa.)

 

   1. Petro anarejelea sheria gani? (“Sheria” hii imetungwa na viongozi wa Kiyahudi, haipo kwenye Agano la Kale. Agano la Kale linazuia ndoa ya mseto na watu wa Mataifa au kuabudu miungu yao. Halizuii “ushirikiano” au “kuwatembelea” watu wa Mataifa.)

 

   1. Sasa Petro anaelewaje maono juu ya wanyama najisi? (Anaelewa kuwa yanawazungumzia watu “najisi.” Haihusiani na ulaji, bali inahusu kumtembelea Kornelio.)

 

  1. Soma Matendo 10:34-35. Hii inatufundisha nini kuhusu umoja ndani ya kanisa? (Kwamba Mungu anawapokea wote wanaomcha na kutenda yaliyo sahihi.)

 

  1. Soma Matendo 11:1-3. Kama ungekuwa Petro ungejibu vipi juu ya shtaka hili? Je, ungesema kwamba hakuna kitu chochote ndani ya Biblia kinachozuia jambo hilo? Je, ungeanzisha mjadala Biblia?

 

  1. Soma Matendo 11:4. Tutaruka vifungu vinavyorudia kisa cha Petro. Soma Matendo 11:18. Nini kiini cha utatuzi wa tatizo hili la umoja? (Petro alionesha jinsi Mungu alivyoenenda kwenye mazingira yake. Wale wakosoaji walikubali kuwa maelezo ya Petro ni ya kweli, na wakaukubali uongozi wa Mungu. Utaona kwamba mjadala wa kiteolojia haukuhusika.)

 

  1. Soma Matendo 11:19-21. Kwa nini vifungu hivi ni vya muhimu katika kuelewa suluhisho kwa swali hili? (Vinaonesha kuwa Mungu anabariki kushiriki ujumbe na watu wa Mataifa. Tunaona jambo hili kwa kujirudiarudia.)

 

  1. Tafakari masuala haya mawili ya umoja. Je, unaona tatizo la jumla? Suluhisho la jumla? (Visa vyote viwili vinahusisha ukosoaji. Wajane wa Kiyunani wanalalamika. Waumini wa Yerusalemu wanamkosoa Petro. Suluhisho la jumla ni uwezo wa Mungu. Wanakamati walipaswa kujawa Roho Mtakatifu. Mungu alizungumza na Petro moja kwa moja kuhusu tatizo la mfarakano kwa waumini wa Mataifa.)

 

   1. Je, kuna kipengele kingine cha jumla kati ya hii mifano miwili? (Soma tena Matendo 6:6 na Matendo 10:9. Katika mazingira yote mawili tunaona maombi.)

 

   1. Hiyo inatufundisha nini leo? (Kwa ujumla tunatakiwa kumtafuta Mungu kwa njia ya maombi na kisha kuangalia utendaji wa Roho Mtakatifu. Tunatakiwa kuheshimu kazi ya Roho Mtakatifu katika kutatua matatizo.)

 

 

  1. Soma Matendo 1:7-9. Wanafunzi walisahauje maelekezo haya ya muhimu kabisa kutoka kwa Bwana wao mara alipokuwa akipaa mbinguni?

 

   1. Je, jibu la suala la kupeleka injili kwa Mataifa mara zote halikuwa mbele yao mara zote? Je, mara zote halikuwa la dhahiri?

 

  1. Rafiki, je, unaomba na kutafuta uongozi wa Mungu pale matatizo ya umoja yanapoibuka? Ikiwa sivyo, kwa nini usijitoe kufanya hivyo leo?

 

 1. Juma lijalo: Umoja Katika Imani.