Hukumu Kabla ya Marejeo

(Danieli 7, Waebrania 9, Wagalatia 3)
Swahili
Year: 
2013
Quarter: 
4
Lesson Number: 
9

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Hukumu! Nani anayetaka hukumu? Wazo langu la jumla maishani ni kwamba kila mtu anataka watu wengine wahukumiwe, lakini wao wenyewe hawapendi kuhukumiwa. Ndiyo, askari polisi wanapaswa kuwasimamisha madereva wanaoendesha magari kwa kasi na kuwalipisha faini. Hapana, askari polisi hapaswi kunisimamisha na kunipa adhabu kwa kuendesha gari kwa kasi! “Tatizo” la hukumu ya Mungu ni kwamba ipo kwa ajili ya watu wote. Endapo tunafikiana na hukumu binafsi, je, hiyo inapaswa kuleta tofauti gani maishani mwetu? Ninapokuwa nikikabiliana na kesi mahakamani, ninahitaji kujua vipimo vya kisheria vinavyohitajika, ninahitaji kumfahamu hakimu, na ninahitaji kufahamu mchakato mzima. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone tunachoweza kujifunza kuhusu hukumu ya Mungu!

  1. Hukumu
    1. Soma Danieli 7:1. Danieli anaota ndoto. Kitu gani kinatupatia uhakika kwamba taarifa ya Danieli kuhusu ndoto yake ni sahihi? (Kwanza, Danieli anatuambia muda ambao jambo hili lilitendeka. Anatuambia juu ya mazingira ilivyotokea na baadaye aliiandika. Yote haya ni ishara ya taarifa ya kuaminika.)
    2. Pitia kwa haraka haraka Danieli 7:2-7 na usome Danieli 7:15-18. Je, wanyama hawa wanawakilisha nini? (Danieli anatupatia msingi wa kutafsiri ndoto yake. Nimesoma maoni kadhaa kutoka kwenye vitabu mbalimbali na yote yanakubaliana kwamba ndoto ya Danieli inahusu mfululizo wa mataifa yenye nguvu yaliyofuatana katika historia. Kwa hiyo, wanyama wanaoibuka wanawakilisha falme za Babeli, Uajemi, Uyunani na Rumi.)
      1. Kwa nini Mungu anafunua jambo kama hili kwa Danieli (na kwetu)? (Ili kutupatia ujasiri katika siku zijazo. Ili tutambue kwamba Mungu wetu ndiye anayetenda mambo yote na anaufahamu mustakabali wetu wa siku zijazo.)
      2. Kwa nini ujumbe ule ni wa muhimu sana kwa Danieli? (Utakumbuka kwamba Babeli iliangamiza hekalu mjini Yerusalemu, na kumchukua mateka Danieli pamoja na watu wengine wengi. Watu wa Mungu, taifa la Mungu, walikuwa kwenye tatizo kubwa. Wanaweza kuhitimisha kwamba Mungu hakuwa akiyashughulikia matukio ya hapa duniani.)
    3. Soma Danieli 7:23-24. Je, jambo hili linatuambia nini kuhusu Ufalme wa Rumi na pembe kumi? (Linatuambia kwamba falme kumi zitakuja baada ya Rumi.)
    4. Soma Danieli 7:8-9. Je, ni kipindi gani hiki kinachoelezewa hapa? (Mjadala juu ya pembe unaonesha kuwa tunayaangalia mataifa yaliyotokana na Ufalme wa Rumi. Tunafahamu kutokana na historia kwamba muungano wa mamlaka zilizoinuka na kuwa na nguvu baada ya Ufalme wa Rumi ulikuwa ni “Ufalme Mtakatifu wa Rumi.” Wanahistoria wanasema kuwa Ufalme Mtakatifu wa Rumi ulikuwepo kuanzia mwaka 926-1808 BK. Kwa hiyo, rejea ya “Mzee wa Siku” kukalia kiti chake inaonekana kufuata baada ya mwaka 1806BK.)
    5.  
    6. Hebu tuangalie suala hili kwa kina zaidi. Soma Danieli 7:9-10. Jambo gani linaendelea hapa? (Huu ni mkao wa kimahakama. Rejea ya “vitabu” kufunguliwa inaashiria kuwa shughuli za mahakama zinaendelea na hukumu za aina fulani hivi zinatolewa.)
    7. Soma Ufunuo 20:11-15. Jambo gani linaelezewa hapa? (Jambo hili linaonekana kufanana kabisa na lile linachoelezewa katika Danieli 7.)
      1. Je, kipimo cha hukumu kwa hawa watu ni kipi? (“Yale waliyoyatenda.”)
      2. Tuna alama nyingine ya muda hapa. Unadhani hukumu hii inatolewa lini? (Lazima itakuwa ni kipindi cha mwisho wa dunia. “Mauti” inatupwa katika ziwa la moto. 1 Wakorintho 15:26 inatuambia kuwa “Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti. Hii itatokea mwisho wa wakati.)
    8. Soma Danieli 7:8 na Danieli 7:20-22 na Danieli 7:24-27. Je, kuna uhusiano gani kati ya watu wa Mungu na pembe ya mwisho? (Kuna vita kati ya pembe na watakatifu. Pembe inashinda kwa muda mfupi, lakini Mungu anatangaza hukumu inayowapendelea watakatifu nao wanashinda.)
      1. Je, tunaweza kufikia hitimisho gani lenye mantiki kutoka kwenye haya mafungu yote yanayozungumzia mahakama na hukumu ya Mungu? (Tunahitimisha kwamba aina fulani hivi ya hukumu inaendelea mbinguni. Ilianza kipindi fulani hivi baada ya mwaka 1806 na inaendelea hadi mwisho wa dunia, kipindi ambacho watakatifu watashinda.)
    9. Unadhani Mungu anataka tujifunze nini kutokana na hii ndoto? (Kama ambavyo ufunuo wa siku zijazo ulivyompa Danieli ujasiri, vivyo hivyo Wakristo tunaambiwa kuwa kuna vita inayoendelea duniani ambayo itakomeshwa Mungu atakapokamilisha hukumu yake ya mwisho. Kwa uwezo wa Mungu tutashinda!)
      1. Vipi kuhusu muda wa jambo hili? Je, kuna umuhimu gani juu ya jambo hilo? (Kwa wengine inaweza kuonekana kwamba Mungu hafanyi chochote. Tupo katika kipindi cha miaka elfu mbili baada ya ufufuo. Mungu yupo wapi? Kwa nini bado hajarudi? Mafungu haya yanatuambia kuwa Mungu ana mpango, na kwamba hukumu ya mwisho ilianza miaka ya 1806 (mafungu mengine yanaweza kuboresha tarehe hiyo) na itaendelea hadi mwisho wa nyakati – watakatifu watakapouchukua ufalme. Tunaishi katika siku za mwisho.)
  2. Mwombezi
    1. Soma Danieli 7:13-14. Je, taswira gani inaingia kwenye tukio hili? (Huyu ni Yesu!)
    2. Soma Waebrania 8:1-2. Je, tumejifunza jambo gani katika masomo yaliyopita juu ya kile Yesu anachokifanya mbinguni? (Yeye ni Kuhani wetu Mkuu, akihudumu kwa niaba yetu.)
      1. Je, unaona uhusiano gani kati ya huduma ya Mungu mbinguni na hukumu iliyotabiriwa na Danieli? (Lengo la mfumo wa patakatifu lilikuwa ni kuhamisha dhambi kwa kafara ya mnyama ili muumini asife. Hukumu ya mwisho inabainisha nani anaishi na nani anakufa. Anachokifanya Yesu katika Waebrania ni sehemu ya hii hukumu ya mwisho ya Danieli 7.)
    3. Soma Waebrania 9:11-15. Je, msingi wa hukumu ya watakatifu ni upi? (Yesu alikufa ili kutuweka huru kutoka dhambini! Alilipa fidia ili kututoa dhambini.)
    4. Soma Waebrania 9:24-28. Je, Mungu anafanya nini mbinguni katika kipindi hiki cha hukumu? (Anaondoa dhambi zetu na kuleta wokovu kwa wenye haki.)
      1. Soma tena Ufunuo 20:12-14. Tuliangalia jambo hili hapo kabla. Je, hapa msingi wa hukumu ni upi? (Kwa mujibu wa matendo yao.)
      2. Soma Waebrania 10:12-14. Je, kipimo cha hukumu ya “hao wanaotakaswa” ni kipi? (Kafara ya Yesu inatufanya kuwa wakamilifu.)
      3. Je, unaweza kuelezeaje hivi vipimo viwili? (Wale wanaopotea wanahukumiwa kwa matendo yao. Wale wanaodai kafara ya Yesu kwa niaba yao wanahukumiwa kuwa wakamilifu milele!)
    5. Hivi karibuni nilisoma kuwa “matarajio ya hukumu yanawahamasisha [watu] kuishi maisha ya uaminifu na ya uwajibikaji.” Je, unakubaliana na wazo hili?
      1. Kwa mujibu wa kile tulichojifunza, je, wenye haki wanatakiwa kuogopa hukumu? Je, uoga wa hukumu unawahamasisha kuishi maisha makamilifu?
      2. Au, je, kafara aliyoitoa Yesu kwa niaba yao kwa kuwa anawapenda inawahamasisha kuishi maisha makamilifu?
      3. Je, ukweli kwamba Yesu alikufa ili kuenenda na dhana ya utawala wa sheria, badala ya kuibadili tu sheria, unawahamasisha wenye haki kuishi maisha makamilifu? (Sikubaliani na hiyo nukuu. Wakristo hawapaswi kuhamasika kuwa na tabia njema kutokana na uoga wa hukumu. Wanapaswa kuhamasika kuwa na tabia njema kwa sababu wanampenda Mungu. Wanapaswa kuhamasika kuwa na tabia njema kwa sababu wanaelewa vita kati ya wema na uovu, na wanataka kusimama upande wa wema na sheria ya Mungu!)
  3. Sheria ya Mungu na Hukumu
    1. Katika masomo machache ya mwisho yaliyopita nimekuwa nikizungumzia juu ya “Utawala wa Sheria.” Kusisitiza kujihusisha kwa Mungu katika utawala wa sheria tunapojadili suala la hukumu inaonekana kutofautiana na wazo la kuhesabiwa haki kwa imani. Hebu tuone kama mawazo haya mawili yanaweza kuendana. Soma Wagalatia 2:15-21. Je, kipimo cha hukumu kwa wale wanaomkiri Yesu ni kipi? (Yesu alipokufa “tuliifia sheria.” “Na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu.” Kipimo si sheria, badala yake kipimo ni endapo tunaiweka imani yetu kwa Yesu.)
    2. Soma Wagalatia 3:10. Kama sheria ni mbaya sana kiasi kwamba tunalaaniwa endapo tunaitegemea, ni kwa jinsi gani basi utawala wa sheria uwe jambo jema? (Tatizo halipo kwenye sheria, tatizo lipo kwetu.)
    3. Soma Wagalatia 3:11-14, Wagalatia 3:21-22 na Wagalatia 3:26-28. Sheria ni nzuri na sisi ndio wabaya. Endapo tunajielekeza kuishika sheria, basi tuna tatizo kubwa, kwa kuwa tunakuwa tupo chini ya laana inayowajia wavunja sheria. Unapofikiria jina lako kutokea katika hukumu ya mwisho, unadhani utafanya nini? (Kama umejivika Kristo, kama umetubu dhambi zako na kumwomba Yesu afunike dhambi zako kwa damu yake, basi katika hukumu ya mwisho Mungu anaangalia kile ambacho Yesu amekitenda badala ya kile ulichokitenda. Kwa upande mwingine, kama hujamkiri Yesu, basi unahukumiwa kwa msingi wa kile ulichokitenda.)
    4. Rafiki, je, unataka kusimama peke yako katika hukumu ya mwisho, ukiwajibika kwa dhambi zako? Au, je, unataka Yesu achukue nafasi yako? Sasa hivi hukumu inaendelea. Yesu anasimama katika mahakama ya mbinguni tayari kushughulika kwa niaba yako. Unatakiwa kufaya Uchaguzi leo!
  4. Juma lijalo: Siku ya Upatanisho Wakati wa Hukumu ya Mwisho.