Huduma Yaanza

(Mathayo 3-4)
Swahili
Year: 
2016
Quarter: 
2
Lesson Number: 
2

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Ungependa Yesu aseme kwamba hakuna “aliye mkuu” kuliko wewe? Unasema kuwa, siyo rahisi? Somo letu juma hili linamhusu mtu ambaye jambo hili ni kweli kwake. Yesu alimzungumzia Yohana Mbatizaji, “kati ya waliozaliwa na mwanamke hakuna aliye mkuu kuliko Yohana.” Hebu tuzame kwenye somo letu la Mathayo ili tuone Mathayo ana mafundisho gani kwetu kupitia kwa Yohana Mbatizaji!

 

I.                   Tubuni

 

A.                Soma Mathayo 3:1-2. Yohana alimaanisha nini aliposema, “ufalme wa mbinguni umekaribia?” (Hakuwa anazungumzia wakati wa mwisho, vinginevyo angekuwa nabii wa uongo. Kutokana na muktadha huo, alikuwa anazungumzia kuhusu mbingu kuja duniani kwa njia ya Yesu.)

 

1.                  Naweza kuielewa “tubuni” katika muktadha wa hukumu ya kipindi cha mwisho na wenye haki kuchukuliwa mbinguni. Lakini je, inaleta mantiki gani katika muktadha wa Yesu kuja duniani?

 

B.                 Soma Mathayo 3:3 na Isaya 40:3-4. Watu wangapi wanarejelewa katika Mathayo 3:3 (bila kujumuisha Isaya)? (Yohana Mbatizaji, yeye ndiye “sauti ya mtu aliaye.” Yesu ni “Bwana.” Wasikilizaji wake ni wale wanaonyoosha mapito.)

 

1.                  Hii inatoa nuru gani kwenye wito wa kutubu kwa sababu Yesu anakuja? (Njia bora ya kujiandaa kwa ajili ya Yesu ni kuamua kwamba muda wa mabadiliko umewadia. Uamuzi wa kufanya jambo tofauti unaurahisishia ujumbe wa Yesu kupenya moyo wako (kuyanyoosha na kuyasawazisha mapito ya Yesu.)

 

C.                 Soma Mathayo 3:4. Makoti yanayotengenezwa kwa singa za ngamia yanapendwa sana siku hizi. Je, ujumbe uliopo ni kwamba Yohana ni mtu anayevaa kwa unadhifu na ambaye anakula chakula kisicho na kemikali? (Soma 2 Wafalme 1:8 na Zekaria 13:4. Mafungu haya yanatuambia kuwa Yohana alikuwa amevaa vazi la kitamaduni livaliwalo na mtume. Kwa mara nyingine, tunaona Mathayo akiongezea habari za uhalisia wa Yesu kupitia kwenye ushuhuda wa Yohana.)

 

D.                Soma Mathayo 3:5-8. Kwa nini Yohana hawaiti viongozi wa dini waje kubatizwa, badala yake anawaita ili “wazae matunda yapasayo toba?” (Hii inaendana na wazo tulilojadili hapo awali, kwamba kuja kwa Yesu kunahusisha uamuzi wa kwamba unahitaji kubadilika. Yohana anawaita “nyoka,” anawaonya kuhusu hasira itakayokuja, na anasema kuwa mnatakiwa kubadilika.)

 

E.                 Soma Mathayo 3:9-10. Mungu anatutarajia tufanye nini? (Hajaridhika na kujihusisha kwetu na dini. Anatutaka tuwe Wakristo wazaao matunda. Hawa viongozi wa dini hawawezi kupumzika kwenye uhusiano wao na Ibrahimu. Lazima waelewe kuwa mabadiliko yanahitajika.)


 

1.                  Je, rejea inayohusu kuzaa matunda inamaanisha kuwa matendo ni ya muhimu kwenye wokovu? (Tutajadili jambo hili katika sehemu inayofuata.)

 

II.                Ubatizo

 

A.                Soma tena Mathayo 3:6 kisha usome Mathayo 3:11. Utaona kwamba kutubu dhambi pamoja na ubatizo ni mambo yanayoendana. Kwa nini?

 

B.                 Soma Wakolosai 2:11-12. Jambo gani linafanana na tohara kwa Mkristo? (Ubatizo.)

 

C.                 Soma Wakolosai 2:13-15. Yohana anapozungumzia toba na ubatizo, lengo lake ni lipi? Hapo awali niliuliza, “kwa nini toba na ubatizo vinaendana?” (Ni kwa sababu mambo hayo ni tohara mpya, ni ukubali wako wa neema, ushirika wako na Yesu katika kifo na ufufuo wake!)

 

D.                Je, umesikia habari za bidhaa ambazo ziko “tayari” kwa ajili ya teknolojia inayofuatia: “cable-ready” au “digital ready,” ili kutumia mifano ya kale? Yohana aliposema kuwa alikuwa anabatiza ili kumrahisishia Yesu (kumfanyia Yesu mapito), nadhani alikuwa anazungumzia kuhusu kuwaandaa watu tayari kwa ajili ya neema. Una maoni gani?

 

E.                 Je, umewasikia Wakristo wakisema kuwa lazima uhakikishe kuwa kila dhambi inafanyiwa toba ili uweze kuokoka? Unadhani kuwa wokovu unageuka na kuanza kuchunguza kila dhambi na kutubu? Je, kwako hiyo inaonekana kama aina ya matendo – matendo ambayo yana umuhimu katika kuwa na kumbukumbu nzuri?

 

1.                  Je, kuwa karibu na Roho Mtakatifu inaweza kufanya kumbukumbu nzuri kutokuwa na umuhimu wowote?

 

F.                  Angalia tena kile ambacho Yohana anawaambia viongozi wa dini ambao anawaita “nyoka.” Soma tena Mathayo 3:7-10. Yohana anatoa wito kwa watu wanaoonekana ni wabaya “kuzaa matunda yapasayo toba.” Wito huo unaonekana kama wito wa kutenda kazi, lakini kutokana na kile tulichojifunza, je, sasa jambo hilo linaonekana kumaanisha nini? (Unaonekana kama ni mtazamo unaotambua hitaji la mabadiliko na utayari wa kuikubali neema. Ni mtu ambaye yuko tayari kuelewa kwamba ubatizo ndio njia ambayo tunakufa kwa ajili ya dhambi zetu na kufufuka katika upya wa uzima.)

 

G.                Hebu turejee nyuma na tusome Wakolosai 2:11. Inamaanisha nini kuuvua mwili wa nyama? (Tohara huondoa nyama. Hivyo, ilikuwa ni ishara ya kuvua asili ya dhambi. Matokeo ya kuikubali neema ni kubadilika. Ili kuelewa vizuri jambo hili, soma Wakolosai 3.)

 

H.                Soma Mathayo 3:13-15. Je, Yohana yuko sahihi kwamba Yesu ndiye anayepaswa kumbatiza yeye badala ya yeye kumbatiza Yesu?

 


1.                  Ikiwa hivyo ndivyo, kwa nini Yesu anamruhusu Yohana ambatize? Kwa mahsusi zaidi, Yesu anamaanisha nini anaposema “ni sahihi kwetu sisi kufanya hivi ili kutimiza haki yote?” (Hili ni daraja kati ya huduma ya patakatifu, ambapo kuchinjwa kwa mnyama kwa ajili ya ondoleo la dhambi ilikuwa ni kitendo kinachomsonda Yesu, na mfumo mpya wa ondoleo la dhambi kwa njia ya ubatizo. Katika huduma ya patakatifu mnyama alimwakilisha Yesu. Katika mfumo wa neema, Yesu anatuwakilisha. Utakumbuka kuwa Wakolosai 2:11-12 inatuambia kuwa tunakufa na tunafufuliwa “pamoja naye” pale tunapobatizwa. Kwa njia hii maneno ya Yesu kwamba kile anachokifanya “ni sahihi… ili kutimiza haki yote” yanaleta mantiki.)

 

I.                   Soma Mathayo 3:16-17. Unadhani kwa nini Mathayo anajumuisha tukio hili kwenye kisa chake? (Nafsi yote ya Mungu iko pamoja, Yesu, Roho Mtakatifu na Mungu Baba. Je, una wasiwasi wowote kuhusu uungu wa Yesu? Wote wawili, yaani Mungu Baba na Roho Mtakatifu wanamuidhinisha yeye pamoja na kile anachokifanya!)

 

III.             Jaribu

 

A.                Pitia kwa haraka haraka 4:1-7 na usome Mathayo 4:3 na Mathayo 4:6. Shetani anampa Yesu changamoto kwenye jambo gani? (Shetani anatia changamoto ili kuthibitisha kama Yesu ni “Mwana wa Mungu.”)

 

B.                 Soma tena Mathayo 3:17. Hii inatufundisha nini kuhusu Mungu wetu na majaribu yetu? (Kwa mahsusi Mungu Baba anamuimarisha Yesu kwenye jambo lile lile ambalo Shetani analishambulia.)

 

1.                  Ikiwa u radhi, je, unadhani kuwa Mungu hatatenda hivyo kwako?

 

C.                 Soma Mathayo 4:8-10. Kwa nini Shetani hakumjaribu Yesu kuiba, kulaani, kukashifu au kutamani? (Kwa sababu hayo siyo masuala ya msingi katika maisha ya Mkristo. Suala la msingi ni endapo unamtumaini Mungu. Historia ya Wayahudi ilikuwa inahusu kutumaini sanamu/miungu au mataifa mengine na sio kumtumaini Mungu. Umuhimu wa jambo hilo haujabadilika hata leo.)

 

IV.             Utume

 

A.                Soma Mathayo 4:12 na Mathayo 4:17. Yesu amechukua nafasi kwenye ujumbe wa Yohana Mbatizaji. Kwa nini Mungu aliruhusu ujumbe wa Yohana ufupishwe? Je, bado Yohana hakuwa na kazi kubwa ya kufanya? (Hili ndilo jambo tulilolijadili hivi punde. Jambo la msingi maishani mwetu ni ikiwa tutamtumaini Mungu.)

 

B.                 Soma Mathayo 4:18-22. Badala ya kuchagua wanafunzi wapya, kwa nini asimwokoe Yohana – kwa kuwa hapakuwepo mtu bora kuliko yeye na alikuwa mhubiri mwenye uzoefu? (Mantiki inabainisha kuwa Yohana atumike. Lakini, maisha ya imani yanasema kuwa tutaukubali uamuzi wa Mungu maishani mwetu.)

 

1.                  Utagundua kuwa Yesu anawaita watu mahsusi. Hiyo inamaanisha nini kwako?

 

C.                 Soma Mathayo 4:23-25. Unawezaje kurudufu njia anayotumia Yesu kufanya uinjilisti? Au je, hilo haliwezekani? (Soma tena Mathayo 3:5. Yohana Mbatizaji hakuhitaji kutenda miujiza ili kuwavuta watu kwake. Tunatakiwa kumwomba Roho Mtakatifu kutuonesha tunachopaswa kukifanya ili kuwaleta watu maishani mwetu na kushiriki nao ujumbe.)

 

1.                  Kwa nini Yohana hakutenda miujiza? (Kwa mara nyingine, jambo hili linahusiana na ukuu wa Mungu. Tunatakiwa kushukuru kutokana na fursa tunazopewa ili kueneza injili. Si kila mtu anaeneza injili kwa njia ile ile.)

 

D.                Rafiki, je, unahitaji mabadiliko maishani mwako? Je, uko radhi kuyatumaini maelekezo ya Mungu kwa ajili ya maisha yako? Kwa nini usitubu sasa hivi na kuufungua moyo wako kwa ajili ya mabadiliko ambayo Mungu anayataka maishani mwako?


 

V.                Juma Lijalo: Fundisho Mlimani.