Somo la 5: Imani ya Ibrahimu

(Warumi 4:1-17)
Swahili
Year: 
2017
Quarter: 
4
Lesson Number: 
5

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, unayo imani moja inayokinzana na imani zako nyingine zote? Kwa mfano, je, magari yako yote yametengenezwa na Chevrolet, lakini mara zote unanunua gari aina ya Ford? Hivyo ndivyo ambavyo wengi wenu mnaweza kulichukulia somo la juma hili. Baba yangu alinifundisha kufanya kazi kwa bidii na kwa haraka kuliko mtu yeyote anayenizunguka. Ni vigumu kwangu kupumzika kwa muda mrefu sana, ninapata msukumo wa kufanya jambo fulani. Mtazamo huu unakinzana na haki kwa imani. Ni karama kutoka kwa Mungu nisiyoweza kuifanyia kazi ili kuipata. Lakini pia, nikitafakari jambo hili kwa umakini zaidi, ninatambua kwamba kuwa na baba aliyekuwa na maadili thabiti ya kazi haikuwa uamuzi wangu. Mibaraka na maelekezo ya Mungu maishani mwangu vimekuwa ni karama. Huenda hii inaendana na mtazamo sahihi wa neema? Hebu tuchimbue kile anachotufundisha Paulo kuhusu neema, ili tuweze kujifunza kwa usahihi mafundisho ya Mungu kwenye hilo somo la muhimu kabisa!

 

 1. Majisifu ya Ibrahimu?

 

  1. Soma warumi 4:1-2. Ikiwa Ibrahimu alikuwa mwema sana kiasi cha kuweza kuhesabiwa haki kwa matendo yake, kwa nini kujisifu kwake kuzuiliwe kwa wanadamu wengine? Kuhesabiwa haki ni kuhesabiwa haki, sasa kwa nini asijisifu kwa Mungu?

 

  1. Soma Warumi 4:3. Ibrahimu alihesabiwaje haki? Nani aliyemhesabia haki? (Hili ni jibu kwa swali la awali. Ibrahimu hawezi kujisifu mbele ya Mungu kuhusu matendo yake mwenyewe, kwa kuwa Mungu alimhesabia haki kwa imani. Ilikuwa vigumu sana kwa Ibrahimu kumwambia Mungu kwamba alihesabiwa haki kwa matendo yake.)

 

   1. Katika Warumi 4:1 Paulo anasema “Ikiwa, kimsingi, Ibrahimu alihesabiwa haki kwa matendo.” Paulo anapotumia neno “ikiwa,” je, hiyo inamaanisha kuwa inawezekana Ibrahimu hakuhesabiwa haki kwa matendo yake? (Haswaa! Sidhani kama Paulo anasema kuwa kweli Ibrahimu alihesabiwa haki kwa matendo yake. Tunafahamu habari nyingi za Ibrahimu kiasi cha kufahamu kwamba hii haiwezi kuwa kweli. Angalia Wagalatia 20.)

 

 1. Matendo v. Karama

 

  1. Soma Warumi 4:4. Kuna tofauti gani kati ya ujira na karama? (Una wajibu wa kulipa ujira, lakini huna wajibu wa kutoa karama (zawadi).)

 

  1. Soma Warumi 4:5. Mungu anawahesabia haki watu wa namna gani? (“Waovu.”)

 

   1. Nakumbuka kuna kipindi fulani ilikuwa maarufu sana kuwauliza watu kama walikuwa “salama kwa ajili ya kuokoa.” Dhana iliyokuwepo ni kwamba usingeweza kuokolewa kama ungejioanisha na dhambi unapokwenda mbinguni. Paulo anasema nini kuhusu nadharia hii? (Kwa dhahiri, haiwezi kuwa kweli ikiwa Mungu anawahesabia haki watu “waovu.” Nadharia ya “salama kwa ajili ya kuokoa” ni hoja nyingine tu ya kuhesabiwa haki kwa njia ya matendo.)

 

   1. Kinyume na kuwa “waovu,” Paulo anabainisha kipengele gani kingine cha watu wenye haki? (Hawafanyi kazi, wanamtumaini Mungu. Je, unamtumaini Mungu?)

 

  1. Angalia tena Warumi 4:5. Asubuhi ya leo nilikuwa ninasoma dondoo kutoka kwenye makala moja yenye kukatisha tamaa iliyojenga hoja kwamba wale waliookolewa hawakuwa kama Wakristo wa kawaida. Badala yake, walikuwa na mwenendo mzuri na tabia nzuri isivyo kawaida. Ilifanana na kauli nyingine nilizokuwa nikizisoma nilipokuwa kijana mdogo zilizoandikwa na mwandishi huyu huyu, na zilionekana kuweka viwango vya juu sana vya wokovu kiasi kwamba hata nilijiuliza kwa nini nilijaribu kuutafuta wokovu. Unadhani kuwa kauli za aina hii ni za uongo kabisa?

 

  1. Soma 1 Yohana 3:4-8 na kisha uilinganishe na Warumi 7:14-20. Yohana anatuambia kuwa “akaaye ndani yake hatendi dhambi.” Paulo anatuambia kuwa hawezi kujizuia kutenda dhambi – ingawa hataki kutenda dhambi. Je, makala yenye kukatisha tamaa niliyoisoma iko sahihi? Ikiwa sivyo, unazielewaje kauli za wazi kabisa zilizoandikwa na Yohana? Unaelezeaje mkanganyiko wa dhahiri wa Paulo? (Kuna mambo mawili ambayo ni rahisi sana kuyachanganya. Jambo la kwanza ni wokovu. Wokovu ni zawadi inayotolewa tofauti na matendo yetu. Suala la pili ni tumaini. Kama unamtumaini Mungu, basi utachukulia kwa dhati kile anachokisema kuhusu namna bora unayopaswa kuyaishi maisha yako.)

 

  1. Soma tena 1 Yohana 3:8. “Kazi ya ibilisi” ambayo Yesu alikuja kuiangamiza ni ipi? (Uasi dhidi ya Mungu. Kazi ya Shetani ya kukudhuru pamoja na kila mtu unayemfahamu. Tunapopokea zawadi ya neema, tunachagua upande. Bado utaona dhambi inajiingiza maishani mwako, lakini umechukua uamuzi kwamba unataka kutembea na Mungu. Angalia tena kaulimbiu ya “salama kwa ajili ya kuokoa,” sio katika mtazamo wa wewe kuiambukiza mbingu dhambi yako, bali katika mtazamo wa endapo unataka kuishi mahali pasipo na dhambi.)

 

  1. Soma Warumi 4:6-8. Kwa nini Paulo anawanukuu Ibrahimu na Daudi, wakati waliishi kipindi kirefu sana kabla neema haijatimizwa kwa maisha ya Yesu, kifo chake na ufufuo wake katika uzima wa milele? (Paulo anajenga hoja kwamba mara zote huu ndio ulikuwa uelewa wa kile ambacho Mungu atakwenda kukifanya kwa ajili ya watu wake.)

 

   1. Unajisikiaje kujua kwamba unaposamehewa, kamwe Mungu “hatahesabu” dhambi ulizozitenda?

 

 1. Nani Anayestahili Karama (Zawadi)?

 

  1. Soma Warumi 4:9-10. Je, neema ipo kwa ajili ya watu wote? (Ndiyo. Haipo kwa ajili ya Myahudi au asiye Myahudi. Haipo kwa ajili ya aliyetahiriwa au asiyetahiriwa.)

 

  1. Soma Wakolosai 2:11-12. Paulo analinganisha ubatizo na tohara. Je, hii inamaanisha kuwa tunaweza kuhesabiwa haki kwa imani bila kujali kama tumetahiriwa au la? Kuna tofauti moja kubwa kati ya tohara na ubatizo. Tohara ilikuwa ni alama iliyowekwa kwa wana wote wa Ibrahimu bila kujali mwelekeo wao wa kiroho. Wakolosai 2:11 inaelezea “tohara” ya ubatizo kama “kuvua asili ya dhambi.”  Huo unaonekana kama uchaguzi wa hiari.)

 

  1. Soma Warumi 4:11-12. Hii inazungumzia nini kuhusu kipengele cha kiakili cha neema? (Inamwita Ibrahimu “baba yao wote waaminio.” Hii inatuambia kuwa kichocheo cha neema ni imani katika kile alichotutendea Yesu.)

 

  1. Soma Warumi 4:13-15. Paulo anatuambia kuwa Ibrahimu hakuahidiwa kwamba atakuwa “mrithi wa ulimwengu” kwa sababu aliishika sheria. Paulo anasema nini katika kufuatilia kifungu cha 15 anapodai kuwa “sheria hufanya hasira” na pasipokuwepo sheria hapana kosa? (Anasema kamwe sheria haiwezi kuwa njia ya kuifikia haki. Mara zote inasonda upungufu wetu. Hata hivyo, ikiwa hakuna sheria, hakuna kuwajibika kwa dhambi. Ni kwa jinsi gani kafara ya Yesu kwa ajili (niaba) yetu inaweza kuwa na maana ikiwa sheria haipo?

 

  1. Soma Warumi 4:16-17. Nani anayestahili kupokea haki kwa imani? (“Wote.”)

 

   1. Hii inatenda nini kwenye madai kwamba baadhi ya watu hatima yao (ambayo tayari wameshapangiwa) ni upotevuni na wengine hatima yao hi kuokolewa? (Ibrahimu “ni baba yetu sote” na “uzao wote wa Ibrahimu umehakikishiwa” neema. Unao uhakikisho wa Mungu kwamba haki kwa imani ipo kwa ajili yako!)

 

 1. Kuyataja Yale

 

  1. Hebu tuangalie tena Warumi 4:17. Ni mambo gani mawili ambayo Mungu anatutendea? (“Anawahuisha wafu” (ikimaanisha kuwa anatupatia uzima sisi tunaostahili mauti ya milele), na “anayataja yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.”)

 

   1. Ni kitu gani ambacho Mungu anakielezea kwa namna tofauti kinyume na jinsi kilivyo? (Maana ya dhahiri ni kwamba Mungu anakuita wewe na mimi kuwa wenye haki ingawa hatuko “salama kwa ajili ya kuokoa.”)

 

   1. Niliwahi kumsikia mhubiri aliyetumia kifungu hiki kumaanisha kuwa ikiwa umemwomba Mungu kitu ambacho huna kwa sasa, Mungu atakupatia. Je, huo ndio uelewa sahihi wa kifungu hiki?

 

   1. Kama wewe ni mwanafunzi wa kujifunza Biblia, unafahamu kuwa Biblia inawaelezea Ibrahimu, Daudi na Samsoni kwa ukarimu mkubwa. Hii inaniliwaza kwamba Mungu anao mtazamo chanya dhidi yao. Unadhani Mungu ana mtazamo chanya namna hii dhidi yako? (Ndiyo, anakuita mwenye haki ingawa hauko hivyo.)

 

  1. Rafiki, mtazamo wako ni upi? Hauwezi kuwa kwamba matendo yako yanakuokoa. Hauwezi kuwa kwamba unahitaji neema pekee ili kupata uzima wa milele. Lazima mtazamo huo utakuwa ni kwamba unaamini kuwa Yesu anayo njia sahihi ya maisha na unamchagua yeye kama Bwana wako. Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, ikiwa hujachukua uamuzi huo, akubadili mtazamo wako umchague Yesu leo?

 

Juma lijalo: Adamu na Yesu.